Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Asema hawezi kuishi na fukara, sasa naogopa kufilisika

July 23rd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina mpenzi ambaye ninampenda kwa dhati, lakini nimeanza kushuku iwapo kweli mapenzi yake kwangu ni ya dhati. Sababu ni kuwa amekuwa akiniambia hawezi kuishi na mwanamume maskini. Kwa sasa ninamtimizia mahitaji yake ya kifedha na nahofia siku ambayo nitashindwa ataniacha. Nishauri.

Kupitia SMS

Msimamo wa mwenzako kupitia matamshi yake ni ishara kuwa hajali mapenzi bali pesa. Ninaamini kwamba unataka mpenzi wa dhati ambaye atakupenda ukiwa na pesa na pia ukikosa. Huyo amekwambia wazi kuwa hawezi kuishi na mtu asiye na pesa. Ushauri wangu ni kuwa umuondokee mapema kisha utafute aliye tayari kukupenda kwa dhati bila masharti.

 

Ana uwezo ila hatoi nimueleze vipi ajue nina mahitaji?

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 28 na nina uhusiano na mwanamume ambaye ninampenda kwa dhati. Tatizo pekee ni kuwa ameshindwa kunitimizia mahitaji yangu ya kifedha ingawa ninajua ana uwezo. Nimeshindwa kumwambia asije akadhani kuwa nia yangu ni kumnyonya pesa zake. Nifanyeje nini?

Kupitia SMS

Ni vyema kwa wapenzi kusaidiana kwa hali na mali. Kwa upande mwingine, si vyema kuchukulia kama kwamba ni lazima kwa mpenzi wako kugharamia mahitaji yako ya kifedha. Inawezekana pia kuwa mpenzi wako hajui shida yako hiyo kwa hivyo inafaa umuelezee. Kama ana uwezo na anakupenda ninaamini atakusaidia.

 

Jumbe za mahaba zanitia kiwewe sana

Kwako shangazi. Juzi nilipata ujumbe wa kimapenzi katika simu ya mpenzi wangu. Nilimuuliza akadai ulitumwa kimakosa lakini nashuku ana uhusiano na mwanamke mwingine. Nishauri.

Kupitia SMS

Inawezekana kwamba mpenzi wako ana mwingine ama iwe ni kweli kwamba alitumiwa ujumbe huo kimakosa. Kama umeweka nambari hiyo, mpigie mwanamke huyo anajuana na mpenzi wako.

 

Namtamani sana mwanamume huyu lakini hana habari

Vipi shangazi? Kuna mwanamume tunayefanya kazi pamoja ambaye ameteka moyo na hisia zangu lakini hajui. Natamani sana awe mwenzangu maishani na nahofia nikikawia atanyakuliwa na mwingine. Nifanye nini ili nimpate?

Kupitia SMS

Itakuwa vigumu kwa mwanamume huyo kujua unavyohisi usipomwambia ama kuonyesha dalili hizo. Kwa sababu si rahisi kwako kumwambia moja kwa moja, jaribu kujenga urafiki wa karibu naye ili uone kama naye anavutiwa na labda atakufungulia moyo wake.

 

Nilimpenda kumbe tuna ukoo, nifanyeje?

Nilikuwa nimechumbia mwanamke fulani lakini nilipomjulisha kwa jamaa zangu nikaambiwa tuna uhusiano wa kifamilia. Tuliachana muda si mrefu akaolewa na mwanamume mwingine. Ninaumwa sana moyoni kwani sidhani nitapenda mwingine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Iwapo kweli kuna uhusiano wa kifamilia kati yako na mwanamke huyo, ni wazi kuwa huwezi kumuoa kwa hivyo huna budi kutafuta mwingine. Inaonekana yeye alielewa kuwa haiwezekani na ndiyo maana alitafuta mwingine akaolewa.

 

Naona amenitupa!

Shangazi pokea salamu zangu. Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa miezi miwili sasa. Siku za hivi majuzi amenishangaza kwani nikimpigia simu ama kumtumia SMS ananyamaza tu. Nishauri.

Kupitia SMS

Si lazima mtu akwambie ndipo ujue hakutaki. Hali kwamba anapuuza simu na jumbe zako za SMS ni ishara kamili kwamba ameamua kukuacha na labda ameshindwa kukwambia hivyo. Kwa nini uendelee kupoteza wakati wako?

 

Hana muda nami

Shikamoo shangazi! Nina mpenzi tunayependana sana. Tatizo ni kuwa ninatamani kuwa naye karibu kila wakati lakini mara nyingi yeye huwa na shughuli nyingi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi hujengwa na kudumishwa kupitia kila mmoja kumpenda mwenzake kama anavyojipenda. Ni vigumu kumpata mwenzako kila unapotaka kwani ana shughuli zingine maishani. Mnahitaji kupanga pamoja wakati wa kuoanana.