Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ataka kujua hali ya mwanawe na hagharimii malezi

August 1st, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina umri wa miaka 21 na nilizaa mtoto na mwanamume aliyekuwa mpenzi wangu lakini tukaachana. Amekuwa akinipigia simu karibu kila siku kuuliza hali ya mtoto ilhali amekataa kugharimia malezi yake. Nimepata mwanamume mwingine tunayependana sana na yuko tayari kunioa na nahisi kuwa baba ya mtoto ananisumbua. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ingawa mpenzi mliyeachana ndiye baba ya mtoto wako, hafai kuulizia hali yake kama hashughuliki kugharamia malezi yake. Kama unahisi amekuwa kero, muondoe katika maisha yako kwa kubadilisha namba yako ya simu. Na iwapo uliye naye yuko tayari kukuoa, itakuwa vyema kwa sababu atakuwa baba ya mwanao na mpenzi wako wa awali atakoma kukufuata.

 

Nimegundua kuwa analisaliti penzi letu kuwa na jicho la nje

Nina mpenzi ambaye tumezaa watoto wawili pamoja. Nimegundua kuwa amekuwa akinisaliti kimapenzi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Usaliti wa kimapenzi ni tabia isiyokubalika kati ya wapenzi na pia katika ndoa. Iwapo una hakika kuwa mwenzako si mwaminifu, basi huna sababu ya kuendelea na uhusiano huo.

 

Amenipa masharti niokoke kabla nimuoe

Shikamoo shangazi! Kuna msichana tunayependana na tumekubaliana kuwa akimaliza masomo nitamuoa. Hata hivyo, yeye ameokoka na ameniwekea sharti kwamba ni lazima mimi pia niokoke ndipo nimuoe. Nishauri.

Kupitia SMS

Ndoa ni ushirika wa maisha na kuna masharti ambayo wahusika wanafaa kuyaweka katika juhudi za kuidumisha. Mwenzako anaamini kuwa wokovu ni muhimu kwenu wawili iwapo mtaishi pamoja kama mume na mke. Sasa itabidi utimize sharti lake hilo ndipo umuoe la sivyo ukishindwa uachane naye.

 

Ameniandama miaka 3 akitaka niwe mke wa pili lakini sitaki

Kuna mwanamume ambaye ameniandama kwa miaka mitatu sasa akitaka tuwe wapenzi. Nimemwambia wazi kuwa haiwezekani kwa sababu ana mke lakini haachi kunifuata. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa wanaume kuwatongoza wanawake popote pale wakati wowote ule. Je, unashangaa ni kwa nini anakuandama tu licha ya kumwambia wazi kuwa hawezi kupata anachotaka kwako? Ukweli ni kuwa anajaribu bahati yake tu kwa matumaini kuwa siku moja utalegeza msimamo wako. Kama umeamua haiwezekani, shikilia msimamo wako huo, hatimaye atachoka na kuachana nawe.

 

Nasikia fununu kuwa mpenzi ameniacha ila yeye hajaniambia

Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye nampenda sana. Hata hivyo, siku za hivi majuzi amekuwa akinionyesha dharau. Nimesikia fununu kuwa anasema ameniacha ingawa nimemuuliza akakana. Je, nimwamini ama nimuache?

Kupitia SMS

Una sababu ya kuwa na hofu hasa kama umepata fununu hizo na pia umeona mabadiliko ya mienendo yake kwako. Hata hivyo, huna ushahidi kwamba ameamua kukuacha kwa sababu yeye mwenyewe amekanusha habari hizo. Ninaamini kuwa akiamua kukuacha atakwambia ama atoweke tu kimya kimya.

 

Anataka kunioa shida ni kuwa haachani na wake za zamani

Nina mpenzi tunayependana sana hata amenipeleka kwao kwa sababu anapanga kunioa. Tatizo pekee ni kuwa imekuwa vigumu kwake kumuacha mpenzi wake wa awali. Nishauri.

Kupitia SMS

Sielewi ulivyokubali kuanzisha uhusiano na mwanamume huyo ukijua moyo wake haujatoka kwa huyo wa zamani. Ni muhimu ujue msimamo wake mapema asije akakuoa kisha aendelee na wa pembeni.

 

Nahisi niko tayari kumuonjesha asali

Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili na ameanza kudai asali. Nafikiria kumgawia kwa sababu nampenda na ninamwamini. Isitoshe, amekuwa na subira kwa miaka hiyo miwili. Waonaje?

Kupitia SMS

Hiyo asali ni yako na pia huyo ni mpenzi wako. Iwapo unahisi wakati umewadia kwako kumfungulia mzinga kwa hiari, hiyo ni sawa. Hata hivyo ni muhimu mtumie kinga kuepuka mimba isiyohitajika kwa sababu bado hamjaoana.