Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ataka kuonja asali kabla ya kunipa hela za biashara

November 15th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 24 na kuna mwanamume anayedai kuwa ananipenda na anataka kunioa. Ameahidi kunifungulia biashara lakini kwanza anataka kulamba asali. Ninashuku nia yake kwangu na pia uwezo wake wa kuniwekea biashara kwa sababu ameniomba pesa mara kadhaa. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Jihadhari sana na mwanamume huyo kwani kuna dalili za kutosha kwamba nia yake ni kukutumia tu kisha atokomee. Ahadi zake za ndoa na biashara ni chambo ambacho ameamua kutumia ndipo akunase kwa haraka ili kukidhi tamaa yake. Imekuwaje kwamba anakuomba pesa na huku anaahidi kukuwekea biashara? Isitoshe, amekuwekea sharti kwamba ni lazima aonje asali ndipo atimize ahadi zake hizo!

 

Nataka kuoa lakini mchumba asema nisubiri kwanza

Hujambo shangazi? Nimekuwa na msichana mpenzi wangu kwa miaka miwili sasa na nimetosheka kuwa anaweza kuwa mke wangu. Wakati wangu wa kuoa umewadia lakini hataki kunisikia ananiambia nimpe muda zaidi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ninaamini msichana huyo pia anakupenda kwa dhati na yuko tayari kuwa mke wako. Kama ndivyo, ni lazima ana sababu nzuri ya kutaka umpe muda zaidi ndipo muweze kuoana. Wawili wanapopendana, hakuna lisilowezekana. Hilo ni jambo mnaloweza kushauriana na kukubaliana. Keti chini na mpenzi wako mzungumze.

 

Mke hapendi ‘nitie jembe’ zaidi ya mara moja nikiwa shamba

Kwako shangazi. Nimeoa na tumejaliwa mtoto mmoja. Kuna jambo fulani ambalo sielewi kuhusu mke wangu na naomba unisaidie. Ninapoingia shambani mara moja tu huwa ni basi hataki tena nirudi hapo wakati huo hadi siku nyingine. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mambo ya chumbani ni siri ya mtu na mkewe na kunapokuwa na tatizo ni wawili hao ambao wanafaa kulitafutia suluhisho. Mshauri mke wako akuelezee sababu yake ya kukukataza kuingia shambani jinsi unavyotaka. Ninaamini ana sababu ya kutosha ambayo itakufanya umuelewe.

 

Tumependana kwa mtandao, linaweza kuwa penzi la dhati?

Vipi shangazi? Kuna mwanamume ambaye tumependana sana ingawa hatujawahi kuonana, tumejuana tu kupitia kwa mtandao. Ni miezi mitano sasa tangu tujuane. Je, huo unaweza kuwa upendo wa kweli?

Kupitia SMS

Nimewahi kusikia visa vya watu ambao wamejuana na kupendana kupitia kwa mtandao na hatimaye wakaoana. Hata hivyo, mtaweza tu kujua hali ya uhusiano wenu baada ya kukutana na kuwa pamoja kwa muda ili kila mmoja wenu aweze kumjua vyema mwenzake.

 

Nimesalia mpweke

Shikamoo shangazi! Nina kijana mpenzi wangu ambaye tumekuwa pamoja kwa mwaka mmoja sasa. Alijiunga na chuo kikuu mwaka jana na nimekuwa nikimuwaza sana hadi ninakosa usingizi kwa sababu nilikuwa nimezoea kuwa naye karibu kila wakati. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hali unayopitia inatokana na upweke kwa sababu unasema kuwa kabla mpenzi wako hajaenda chuoni mlitumia wakati mwingi pamoja. Isitoshe, uhusiano wenu ni mchanga sana na jambo hilo pia linazidisha hali yako. Hata hivyo, usitie hofu kwa sababu hiyo ni hali ya muda tu, hatimaye utaizoea.

 

Naogopa kutatizwa na baba watoto, nimepata mwingine anayetaka kunioa

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 28 na nina watoto wawili ingawa niliachana na baba yao hivi majuzi baada ya kuishi pamoja kwa miaka mitatu. Sasa nimepata mwingine aliye tayari kunioa lakini nahofia kuwa mume wangu wa kwanza ataleta shida. Nishauri.

Kupitia SMS

Hali kwamba umeamua kuolewa na mwanamume mwingine ni thibitisho kuwa huna nia ya kumrudia baba ya watoto wako. Ndoa ni hiari ya mtu kwa hivyo mume mliyeachana hawezi kukuzuia kuolewa na mwanamume mwingine. Hiyo ni haki yako kwa hivyo huna chochote cha kuogopa.