Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ataka nigharimie mahitaji yote na tumejuana majuzi

June 6th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI nakusalimu. Nimeanza uhusiano majuzi tu na mwanamke ambaye nampenda kwa moyo wangu wote. Tatizo ni kuwa hatujajuana vizuri na tayari anataka nigharimie mahitaji yake yote kama kwamba yeye ni mke wangu ilhali ni mpenzi tu. Nahisi nia yake ni kunitumia. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Huo umekuwa udhaifu wa wanawake wengi hasa wakati huu ambao maisha yamekuwa magumu. Msimamo wangu ni kwamba mwanamke hafai kumwekelea mizigo mpenzi wake hadi wanapoona. Hata wakioana, maisha ya sasa ni kusaidiana. Ni nani alikuwa akilipa gharama hizo kabla hamjakutana? Kama unahisi huna uwezo wa kubeba mizigo yake hiyo, mwambie ukweli. Kama hilo litamfanya akuache, ni sawa.

 

Atishia nikifanya kazi ya mjengo ataniacha

Kwako shangazi. Nilimaliza masomo miaka sita iliyopita na bado sijapata kazi. Sasa nimeamua kufanya kazi za kibarua katika mijengo lakini mwanamke mpenzi wangu hataki anasema hiyo ni kazi duni. Anatishia kuwa nikianza kufanya kazi hiyo ataniacha. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Tunaishi enzi ambazo imekuwa vigumu kupata kazi hata kwa watu waliosoma. Ni vyema kwamba umeamua kufanya kazi iliyopo kwa sasa na ninashangaa kwa msimamo wa mpenzi wako. Kazi ni muhimu kwani ndiyo itakupa mapato ya kujikimu maishani. Akisisitiza kuwa hataki hutakuwa na budi kuchagua kati yake na kazi hiyo.

 

Mpenzi anapigiwa simu na wanaume wengi tukiwa pamoja

Hujambo shangazi? Kuna msichana tunayependana na tulipokutana aliniambia hana mwingine. Lakini kila tunapokuwa pamoja anapigiwa simu na wanaume wengi na inabidi awadanganye kwamba yuko nyumbani. Hilo linanitia wasiwasi. Nishauri.

Kupitia SMS

Kumbuka kuwa huyo ni mpenzi wako tu wala si mke wako na wanaume wengine wana haki ya kumtongoza. Pili, hali kwamba anawadanganya wanaume wanaompigia simu mkiwa pamoja ni ishara kuwa hana haja nao. Ondoa wasiwasi na uwe na imani wewe tu ndiye wake.

 

Mchumba hanisaidii, nahofia atakaponioa atakuwa mkono gamu

Shangazi pokea salamu zangu. Nina mchumba na ameniahidi kunioa. Tatizo lake ni kuwa kila nikimwendea nikiwa na haja ya pesa anapenda kulalamika. Nahofia kuwa akinioa atakuwa mgumu wa kutoa pesa na singependa kuwa na mume wa aina hiyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Hujaelezea iwapo una hakika mwenzako ana uwezo wa kukusaidia kifedha au la. Kama ana uwezo na anaona vigumu kukusaidia, basi hizo si dalili nzuri na itabidi umuache kama hutaki kuwa na mtu kama yeye maishani.

 

Natafuta mwanamke aliye tayari kuolewa, sijali ikiwa ana mtoto

Shangazi ni matumaini yangu kuwa wewe ndiye utanisaidia niweze kumpata mke mzuri. Nina umri wa miaka 35 na bado sijaoa. Namtafuta mwanamke yeyote yule aliye tayari kuolewa hata kama ana mtoto hiyo kwangu si hoja. Tafadhali nisaidie.

Kupitia SMS

Ningependa kukusaidia sana ndugu lakini siwezi. Sababu ni kuwa uhusiano wa kimapenzi na ndoa ni mambo ya kibinafsi na mtu binafsi ndiye anayefaa kuchagua mpenzi wa moyo wako. Endelea kutafuta tu na uwe na subira. Kuna wanawake ambao mara kwa mara hutuma jumbe zao hapa wakitafuta wanaume wa kuwaoa kwa hivyo endelea kusoma ukumbi huu, huenda ukabahatika kumpata hapa.

 

Shangazi nifafanulie ni wakati gani mmoja anaweza kuwa na uhusiano wa mapenzi

Shangazi nina jambo ambalo naomba unielezee. Je, ni wakati gani mzuri maishani ambao ninafaa kuwa na mpenzi? Ni wakati nikiwa chuo kikuu ama nikianza kazi?

Kupitia SMS

Mtu yeyote mzima, yaani aliyehitimu umri wa miaka 18, anaweza kushiriki uhusiano wa kimapenzi. Hata hivyo, mara nyingi ninapendekeza kwa watu kuanza uhusiano baada ya kumaliza masomo. Sababu ni kuwa uhusiano unaweza kumteka akili mtu kiasi cha kumfanya asahau masomo.