Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Baada ya mume wa mtu kunitia mimba ametoweka

August 23rd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Kuna jambo linalonitatiza moyoni na ninaamini utanisaidia. Nina umri wa miaka 24 na nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wa mtu kwa karibu mwaka mmoja. Miezi miwili iliyopita niligundua nina mimba na nilipomuelezea akaniambia nisiwe na hofu. Sasa huu ni mwezi wa tatu sijamuona, hakuna mawasiliano wala hanitumii pesa za matumizi kama awali. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Naona wewe bado ni msichana mchanga na sielewi ni kwa nini uliamua kushikana na mume wa mwenyewe badala ya kutafuta wako. Isitoshe, umepuuza umuhimu wa kutumia kinga na kwa sababu hiyo umepata mimba. Hali kwamba mwanaume huyo ametoweka baada ya kujua una mimba yake ni thibitisho kuwa hayuko tayari kuwajibika. Bahati mbaya ni kwamba huwezi kumlazimisha kufanya hivyo hata kisheria kwa sababu uhusiano wenu umekuwa haramu. Itabidi ujitayarishe kulea mtoto huyo.

 

Tumejuana mwezi 1 na anaomba tunda

Habari zako shangazi? Mimi nimechanganyikiwa na tafadhali nakuomba unisaidie. Mwanamume ambaye tumejuana kwa mwezi mmoja sasa anataka tushiriki mahaba. Nampenda sana lakini nahisi ni mapema sana kwa jambo hilo na pia sitaki kumpoteza. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Mimi kamwe siamini kuwa tendo la ndoa ndilo thibitisho pekee kuwa mtu anampenda mwenzake. Mwezi mmoja ni muda mfupi sana na nashuku mwanaume huyo hakupendi kwa dhati na shabaha yake ni hiyo tu. Unaweza kumtimizia ombi lake kisha akuteme uachwe ukijuta. Mwambie wazi kuwa unahitaji muda zaidi kumjua. Kama kweli anakupenda atangojea.

 

Ninatafuta mume

Habari yako shangazi. Nina umri wa miaka 25. Nilipata mtoto nikiwa ndo kwanza nabaleghe baada ya kudanganywa na mwanamume fulani kisha akaniacha. Sasa natafuta mwanamume ambaye atanioa pamoja na mtoto wangu na amkubali kama wake. Tafadhali nisaidie.

Kupitia SMS

Ninaamini umejifunza kutokana na uhusiano wako wa kwanza ambao ulitibuka na kukuacha na mzigo. Wewe bado ni msichana mdogo kiumri na unaweza kupata mume bora tu uwe na subira. Ni matumaini yangu kwamba ujumbe wako huu utawafikia wanaume wanaotafuta wake na labda kuna atakayevutiwa akutafute.

 

Nitamtoaje kwa mrembo mwingine?

Shikamoo shangazi! Kuna kijana fulani ambaye nampenda kwa moyo wangu wote ingawa sisi ni marafiki tu. Sasa nimegundua kuna msichana mwingine ambaye pia anampenda. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hilo sasa litategemea uamuzi wake mwenyewe. Kama mnampenda nyote wawili kuwa tayari kwa lolote kwani anaweza kukuchagua wewe ama huyo msichana mwingine.

 

Nimeshindwa kabisa kumpata mchumba

Vipi shangazi? Tafadhali nakuomba unisaidie. Nina umri wa miaka 24 na nimeshindwa kabisa kupata mchumba ilhali sina kasoro yoyote ya kimwili. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kutafuta mchumba si jambo rahisi na mtu anahitaji kuwa na subira. Endelea kutafuta kwani ninaamini kuna yule ambaye Mungu amekutengea na wakati ukifika utampata utulie.

 

Jumbe za wanaume kwake zinanihofisha

Hujambo shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu ninayempenda sana lakini ninashuku kuwa si mwaminifu kwangu. Sababu ni kwamba kuna wanaume ambao wamekuwa wakimtumia jumbe za kimapenzi na nikimuuliza anasema wao ndio wanamfuata yeye hawataki. Nimwamini?

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa wanaume kuwatongoza wanawake. Huenda ni kweli kuwa wanaume hao wanajaribu tu bahati yao kwa mpenzi wako naye hana shughuli nao. Badala ya kumshuku mwenzako bila ushahidi wowote, nakushauri uchunguze kwanza ujue ukweli ili uondoe wasiwasi moyoni. Unaweza hata kumwambia awatumie SMS ukiona au awapigie simu awaambie ana mpenzi kwa hivyo wamkome.