Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Baba ataka tushiriki mapenzi nikiwa na umri wa miaka 16, nifanyeje?

May 23rd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 16 na nina tatizo ambalo nataka unisaidie kutatua. Mimi ndiye mtoto wa pekee wa wazazi wangu. Mama yangu anafanya kazi mbali na ninaishi na baba yangu. Baba amekuwa akinisumbua akitaka tushiriki mahaba. Nimeshindwa nitafanya nini. Tafadhali naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Maajabu ya ulimwengu hayo! Siamini kuwa baba mzazi anaweza hata kufikiria kushiriki tendo hilo na binti yake mwenyewe. Usikubali kamwe kwani kitendo hicho ni mwiko katika jamii nzima ya binadamu. Pili, mfahamishe mara moja mama yako kuhusu jambo hilo. Kama mama yako hayupo, mwambie jamaa yako mwingine uliye karibu naye ili akupe mwelekeo zaidi.

 

Nitampataje mtoto baada ya kutengana na mke wangu?

Naomba ushauri wako. Nilikuwa na mke na tukajaliwa mtoto mmoja ambaye ninampenda sana naye pia ananipenda. Hata hivyo, mke wangu alianza kutembea sana nje na nikalazimika kumuacha. Alirudi kwao na mtoto na sijui nitafanya nini ili nimpate mtoto wangu. Nisaidie tafadhali.

Kupitia SMS

Wazazi wanapotengana na kukosa kupatana kuhusu ni nani kati yao anayefaa kuishi na mtoto au watoto, mzozo huo hutatuliwa mahakamani. Kama mke wako amekataa na mtoto na unahisi wewe ndiye unayefaa kuishi naye, itabidi utafute suluhisho kortini.

 

Nimegundua amepata mwingine mtandaoni

Vipi shangazi? Nina kijana mpenzi wangu ninayempenda sana. Hata hivyo, juzi niliona kwenye mitandao msichana mwengine aliye na jina sawa na langu ambaye wanaitana wapenzi. Je, nimuache?

Kupitia SMS

Kama unayosema ni ya kweli, basi ina maana kuwa huyo unayemuita mpenzi wako si mwaminifu bali ni ndumakuwili. Sasa umejua kuwa ana mpenzi mwingine kwa hivyo utaamua mwenyewe iwapo utamuacha ama utaendelea kumvumilia na tabia yake hiyo.

 

Nina umri wa miaka 26 na bado sijampata mpenzi, nisaidie

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 26 na natamani sana kuwa na mpenzi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kazi yangu katika safu hii ni kutoa ushauri wala si kusaidia watu kutafuta wapenzi. Kama wewe ni mwanamume, itabidi ujitahidi kutafuta mpenzi la sivyo utaishi kwa upweke. Kama wewe ni mwanamke, kuwa na subira na ujaribu kutangamana na wanaume wala si kuketi kitako nyumbani ukitarajia mpenzi aanguke kutoka angani.

 

Wasichana wanifuata wakitaka tuwe wapenzi, nishauri

Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 22. Ninashangaa kwamba warembo wanapenda sana kunifuata wakinitaka, si kwa simu, si kwa mitandao. Sijui nina jini la kupendwa ama vipi. Nishauri.

Kupitia SMS

Je, ina maana kwamba unalalamika kwa kupendwa ama nini? Mimi ninaamini kuwa mtu hupendwa kutokana na maumbile au tabia yake. Hayo yako eti una jini la kupendwa mimi siyajui. Pili, unafaa kushukuru badala ya kulalamika kwa sababu kuna wenzako ambao wamekuwa wakisaka wapenzi kwa muda mrefu bila kufaulu.

 

Niliachana na mpenzi zamani ila nashindwa kumsahau, nifanyeje?

Kwako shangazi. Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 22. Sijaolewa ila nilizaa mtoto na mwanamume tuliyekuwa wapenzi. Punde tu nilipojifungua, tulianza kukosana na hatimaye tukaachana aliponitambulisha kwa mpenzi wake mwingine. Muda si mrefu waliachana na tangu hapo tumekuwa tukikutana na kufurahia mahaba kama awali. Hata hivyo nataka kumsahau ili niendelee na maisha yangu lakini nimeshindwa kwa sababu nampenda sana. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, nahisi kuwa unajaribu kubishana na moyo wako. Ukweli ni kwamba hutaki kumuacha mwanamume huyo kama unavyodai kwa sababu unamalizia kwa kukiri kuwa unampenda sana. Na hiyo ndiyo sababu yako kumkaribisha tena katika maisha yako baada yake kuachana na mpenzi aliyemfanya akuache. Kama yuko tayari mrudiane, acha maringo. Isitoshe, ndiye baba ya mtoto wako.