Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Bosi ananitaka nami sitaki ila nahofia kufutwa

October 21st, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HABARI zako shangazi? Nina umri wa miaka 22 na niliajiriwa mapema mwaka huu. Bosi wangu anataka tuwe wapenzi na yuko tayari kunipatia chochote ninachotaka. Ninajua kwamba ana mke na watoto na pia ana uhusiano na wanawake wengine kadhaa tunaofanya kazi pamoja. Mimi siwezi kuanzisha uhusiano na mtu nikijua wazi kuwa nia yake ni kunitumia. Hofu yangu ni kwamba nikikataa ombi lake atanifuta kazi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kama unavyosema, nia ya huyo mwajiri wako ni kukutumia kwa sababu ameoa tena unasema ana uhusiano na wanawake wengine hapo kazini. Ni muhimu kuheshimu nafsi yako wakati wowote na mahali popote pale. Huwezi kuwa na uhusiano wa kimapenzi na bosi wako kila mahali unapofanya kazi. Mwambie ukweli kwamba nafsi yako haikuruhusu kuwa na uhusiano na mtu mwenye familia kama yeye. Ni heri akufute kazi lakini udumishe heshima yako.

 

Simu yake yaonyesha kuna mume asiyekosa kumpigia kila siku

Shangazi nimekuja kwako kwa ushauri. Huu ni mwaka wa tatu tangu nilipooa na mke wangu amenizalia watoto wawili. Juzi nilipata kukagua simu yake na nikapata nambari yenye jina la mwanamume ambaye amekuwa akimpigia karibu kila siku. Bado sujamuuliza na jambo hilo linanisumbua sana moyoni. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Unasema umeona tu nambari ya simu yenye jina la mwanamume ambaye humjui na hujamuuliza mke wako. Kama amekuwa akimpigia mara kwa mara, ninaamini kuwa huyo ni mtu ambaye wanafahamiana vizuri na kuna jambo au mambo yanayowahusu ambayo wamekuwa wakizungumzia. Ni mke wako tu anayeweza kukwambia huyo ni nani na wamekuwa wakizungumzia nini. Itakuwa bora umuulize badala ya kukaa kimya huku ukiendelea kuumia moyoni.

 

Aliacha mtoto wetu kwa wazazi wake akaolewa kwingineko

Hujambo shangazi. Nilizaa mtoto na mwanamke aliyekuwa mpenzi wangu lakini mwishowe tukaachana. Aliolewa na mwanamume mwingine lakini mtoto wetu anaishi na wazazi wake. Je, ni haki ya kudai mtoto huyo.

Kupitia SMS

Hatua ya mwanamke huyo ya kumuacha mtoto wenu kwa wazazi wake ni ishara kwamba hakutaka mume wake ajue kuwa ana mtoto ama mwanamume huyo alimkataa mtoto asiyekuwa wake. Kama hali ni hiyo, una haki ya kumchukua mtoto huyo kwa sababu wewe ni mzazi wake halali na mama yake hataki kuishi naye.

 

Kwa miaka miwili ya kumtamani yeye huniambia tu nisijali, sijui nia yake ni ipi

Vipi shangazi? Kuna mrembo ambaye ninatamani sana awe mpenzi wangu. Nimemwambia lakini hajaniambia iwapo inawezekana ama haiwezekani. Kwa miaka miwili ambayo nimemfuata, kila nikimuuliza huniambia tu kwamba nisijali. Sijui jibu lake hilo lina maana gani. Nisaidie kuelewa.

Kupitia SMS

Miaka miwili ambayo umemfuata msichana huyo ni muda mrefu na hajakupa jibu kamili. Hilo la kukwambia kwamba usijali si jibu la ombi lako. Ninahisi kuwa hataki uhusiano nawe na labda anashindwa kukwambia. Hakuna haja ya kupoteza wakati wako zaidi kwake. Tafuta mwingine.

 

Alinisaliti nilipokuwa na mimba yake lakini nikamsamehe, kumbe hakuacha ukware

Hujambo shangazi? Nilikosana na mwanamume mpenzi wangu nilipomfumania akiwa na mwanamke mwingine. Wakati huo nilikuwa na mimba yake na nilipojifungua akaniomba msamaha tukarudiana. Sasa nimegundua ameanza kukutana tena na yule mwanamke. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mpenzi wako aliposaliti penzi lenu kwa mara ya kwanza ulimsamehe ukiamini kwamba alijuta na hangerudia. Hali kwamba amerudi kwa mwanamke huyo ni thibitisho kwamba huwezi kumwamini tena. Hufai kupoteza wakati zaidi kwake wala kuhangaisha moyo wako tena kumhusu. Achana naye.