Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Dada ya mpenzi wangu ananipa umbea dhidi yake

March 16th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina umri mwenye umri wa miaka 23 na ninasoma katika chuo kikuu. Nimekuwa na uhusiano na mrembo fulani kwa mwaka mmoja sasa na tunapendana sana. Ajabu ni kuwa mmoja wa dada zake amekuwa akinielezea mambo mabaya kumhusu. Sielewi nia yake na sijui nitafanya nini kwa sababu nampenda sana dada yake na siwezi kumuacha. Naomba unishauri.

Kupitia SMS

Ni jambo la kushangaza kwamba dada ya mpenzi wako amejitolea kumharibia sifa mwenzake. Inawezekana kwamba anawaonea wivu kwa hivyo anatafuta namna ya kuwatenganisha. Ushauri wangu ni kwamba umpuuze tu. Akigundua hutilii maanani udaku wake huo atakoma.

 

Amenipa masharti kabla ya kukubali kuwa mpenzi wangu

Hujambo shangazi? Kuna mwanamke jirani yangu katika mtaa ninamoishi ambaye nimempenda ingawa ana mtoto kutokana na uhusiano wa awali. Nimemwelezea nia yangu na akakubali lakini kwa masharti mawili – niwe nikimlipia kodi ya nyumba na karo ya shule ya mtoto wake. Nifanyeje?

Mwanamke huyo amekupatia masharti ambayo anataka utimize ndipo akubali kuwa mpenzi wako na hiyo ni haki yake. Ni haki yako pia kukataa masharti yake na hiyo itakuwa na maana kwamba usahau penzi lake. Uamuzi ni wako.

 

Ninahisi wazazi wake mchumba waweza kuwa wasumbufu

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na mchumba kwa miaka miwili sasa na ameamua kunioa. Katika muda ambao tumekuwa pamoja, nimekutana mara kadhaa na wazazi wake na ninahisi kuwa wanaweza kuwa wasumbufu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hujaelezea ni kwa nini unafikiri wazazi wa mpenzi wako ni watu wasumbufu. Hata hivyo, unaweza kushauriana jambo hilo na mpenzi wako ili mjue namna ya kulishughulikia. Kumbuka ndiye anayekuoa wala si wazazi wake.

Aliyenioa simpendi kama niliyekuwa naye awali

Hujambo shangazi? Nilikuwa na wapenzi wawili na mmoja wao akanipa mimba kisha akanioa. Lakini ninampenda zaidi huyo mwingine na bado huwa tunawasiliana ingawa yuko mbali. Nifanyeje?

Hayo ndiyo matokeo ya ulaghai wa kimapenzi. Kama ungeamua mapema na kuchagua unayempenda hungekuwa unajuta sasa. Mambo ni mawili; uvumilie kuishi na baba ya mtoto wako ama umwambie ukweli ili muachane umfuate huyo unayempenda.

 

Amekataa nipeleke mahari kwao

Habari zako shangazi? Huu ni mwaka wa tatu tangu nilipoanzisha uhusiano na mwanamke ninayempenda kwa dhati. Sasa niko tayari kupeleka mahari kwa wazazi wake lakini amekataa. Nifanye nini?

Hatua ya mwanamke huyo ya kukukataza kupeleka mahari kwao ni thibitisho kamili kuwa hayuko tayari kuwa mke wako. Anajua vyema kuwa kupeleka mahari ni kuhalalisha ndoa na ndiyo maana amekataa. Kama unamtaka awe mke inaonekana haitawezekana.

 

Nimechelewa?

Habari yako shangazi? Nina umri wa miaka 32 na sijaolewa wala sijawahi kuwa na mpenzi maishani mwangu. Je, nimechelewa?

Kupitia SMS

Hujachelewa hata kidogo. Kila jambo lina wakati wake maishani. Hasa, shughuli ya kutafuta mchumba si kazi rahisi na inahitaji subira kubwa. Huna sababu ya kuwa na hofu.

 

Ataka kunioa wa pili

Kwako shangazi. Kuna mwanamume tuliyekuwa wapenzi lakini tukatofautiana na kuachana. Hatimaye alioa mwanamke mwingine lakini amekuwa akiniambia eti ni mimi tu amewahi kupenda kwa dhati na yuko tayari kunioa mke wa pili. Mimi pia bado nampenda. Nishauri.

Kupitia SMS

Mara nyingi tunapokabiliwa na hali kama yako huwa tunajiliwaza kwamba bado tunapendwa kwa sababu tunaambiwa hivyo. Sidhani mwanamume huyo anakupenda kwa dhati kama anavyodai, la sivyo hangekuacha na kuoa mwanamke mwingine. Ningekuwa wewe singekubali.