Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Demu wangu ghafla ameanza kuwa baridi sana

December 6th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nimekuwa na msichana mpenzi wangu kwa miaka miwili sasa na nampenda kwa dhati. Hata hivyo, katika miezi mitatu iliyopita mwenzangu ameanza kuwa baridi kwangu na uhusiano wetu si mzuri kama hapo awali. Hali hiyo inanitia wasiwasi. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaamini kwamba kuna sababu ya mabadiliko ya tabia ya mpenzi wako kuhusu uhusiano wenu. Hali kama hiyo inaweza tu kutatuliwa kupitia mazungumzo kati ya wahusika. Keti chini naye umhoji kuhusu hali hiyo ili ujue kinachoendelea katika mawazo yake na kuona kama mnaweza kuirekebisha.

 

Nimelikataa dume ila halisikii, laniandama tu

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 21. Kuna kijana fulani ambaye ananiambia ananipenda lakini mimi simpendi. Nimemwambia hivyo mara kadhaa lakini hasikii, anaendelea kuniandama tu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Iwapo umeamua hutaki uhusiano na kijana huyo hawezi kukulazimisha hata kama anakupenda namna gani. Mapenzi ya dhati yanafaa kutoka pande zote mbili. Shikilia msimamo wako, hatimaye atachoka aachane nawe.

 

Ninamuacha mpenzi asiyefumba jicho

Vipi shangazi? Nina mpenzi ambaye nampenda sana lakini nimeamua kumuacha. Sababu ni kwamba nimegundua ana wanawake wengine wengi na pia anapenda sana masuala ya chumbani. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Uamuzi wako huo unatosha, sidhani unahitaji ushauri wowote. Uhusiano wa kimapenzi haudumishwi kwa mapenzi pekee bali pia uaminifu kati ya wahusika. Kama umethibitisha kuwa mpenzi wako ana wapenzi wengine, huna sababu ya kuendelea kupoteza wakati wako kwake. Achana naye utafute mwingine.

 

Hataki nidokoe tunda katu, subira yaniisha

Hujambo shangazi? Nimeanza kushuku iwapo mwanamke mpenzi wangu ananipenda kweli. Sababu ni kwamba kila nikimuomba haki yangu huniambia nisubiri. Je, ananichezea?

Kupitia SMS

Ninaamini kwamba haki unayozungumzia ni tendo la ndoa. Nitakwamba ukweli ingawa najua utakuuma. Huna haki yoyote kwa mwanamke huyo. Sababu ni kwamba yeye ni mpenzi wako tu wala si mke wako. Haki ya tendo la ndoa ni kwa mtu ambaye ameoa ama kuolewa. Mpenzi wako anajua hilo na ndiyo maana anakwambia usubiri.

 

Ninashuku kuwa mpenzi anitaka tu kwa sababu ya ubikira

Shikamoo shangazi! Ni matumaini yangu kwamba wewe ni mzima. Nina umri wa miaka 18 na ninasoma katika shule ya upili. Kuna kijana ambaye anadai kuwa ananipenda lakini nahisi kuwa ananitaka kwa sababu mimi ni bikira. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni jambo la maana kwamba umetunza mwili wako hadi kufikia umri wako huo. Hujasema umejuaje kwamba kijana huyo anakutaka kwa sababu wewe ni bikira. Hata hivyo, iwapo una hakika kuwa nia yake ni kuharibu ubikira wako, ni muhimu ujiepushe naye. Wewe bado ni mdogo na hujafikia kiwango cha kuelewa maana ya mapenzi. Isitoshe, unasoma na unafaa kuzingatia maomo yako.

 

Laazizi wa kwangu asema mapenzi bila kutimiza masuala ya ulilini hayana ladha

Shikamoo shangazi! Kuna kijana ambaye tumekuwa wapenzi kwa mwaka mmoja sasa. Kwa muda wote huo hatujawahi kushiriki mapenzi na sasa analalamika akidai eti mapenzi bila tendo lenyewe si mapenzi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Madai ya mpenzi wako si ya kweli. Tendo la ndoa ni halali tu kwa watu walio katika ndoa. Watu wanaweza kudumisha uhusiano wa kimapenzi kwa miaka mingi bila tendo hilo huku wakisubiri ndoa. Hata hivyo, wapo wengine wanaokubaliana kushiriki mapenzi kabla ya ndoa. Hatari ya uamuzi kama huo ni kwamba nia ya wanaume wengi huwa hiyo tu na wakitimiza wanatoweka. Haya ni mambo muhimu ya kuzingatia katika uamuzi wako.