Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Ex wake anamtia presha warudiane, nifanyeje?

July 31st, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI pokea salamu zangu. Nina mpenzi tunayependana kwa dhati. Hata hivyo mpenzi wake wa awali amekuwa akimpigia simu karibu kila siku akimuomba warudiane ingawa mpenzi wangu ameniambia hamtaki. Nahofia akisisitiza, mpenzi wangu anaweza kushawishika. Nishauri.

Kupitia SMS

Usitie wasiwasi sana kuhusu mwanamke huyo kama mpenzi wako amekwambia hamtaki. Hata hivyo, kama unavyosema, mpenzi wako akiendelea kumsikiza hatimaye anaweza kumuonea huruma na labda kumrudia. Mwambie akatize mara moja mawasiliano kati yao hata ikibidi abadilishe nambari yake ya simu.

 

Nimepata mwanamume kwake lakini anadai ni mpenzi wa zamani

Vipi shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka miwili sasa, lakini nilishangaa juzi nilipomtembelea kwake nikampata na mwanamume mwingine. Baadaye aliniambia huyo ni mpenzi wake wa awali waliyeachana na ameanza kumfuata. Sina hakika iwapo hiyo ni kweli au ananihadaa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Inawezekana anavyokuambia ni kweli. Hata hivyo, ni muhimu akuonyeshe kwa hakika kuwa hawana mpango wa kurudiana. Kwa mfano, hafai kukutana naye au kumruhusu amtembelee nyumbani kwake kama kweli waliachana. Ukiwapata pamoja tena ujue wamerudiana.

 

Moyo umempenda ila anajitia hamnazo

Kwako shangazi. Kuna mwanamke anayeishi mtaa jirani ambaye ameteka hisia zangu kimapenzi. Nimekutana naye mara kadhaa na kumuelezea lakini hataki kuelewa. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Unakosea kwa kusema kuwa mwanamke huyo hataki kukuelewa. Ukweli ni wewe ndiye hutaki kuelewa kwamba hakutaki na huwezi kumlazimisha akupende. Acha kupoteza wakati wako kwake na badala yake utafute mwingine.

 

Wazazi wake wakataa kunipa mtoto wangu

Kwako shangazi. Nilikuwa nimeoa lakini nikamuacha mke wangu nilipogundua kwamba alikuwa na uhusiano wa pembeni na mwanamume mwingine. Hatimaye aliolewa na mwanamume huyo na sasa wazazi wake wamekataa na mtoto tuliyezaa pamoja. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kama wewe ndiye baba mzazi wa mtoto huyo, basi una haki kwake na hakuna anayefaa kukataa naye. Pili, sielewi ni kwa nini mtoto huyo anaishi na wazazi wa mama yake ilhali amepata mume mwingine. Iwapo unaona hamtaweza kusuluhisha wenyewe mvutano huo, unaweza kutumia sheria kudai mtoto wako.

 

Nina wasiwasi mafisi watamnyakua mpenzi

Hujambo shangazi? Kuna msichana ambaye tumekuwa na uhusiano kwa mwaka mmoja sasa. Nampenda sana lakini pia kuna vijana wengine ambao wamekuwa wakimnyemelea hasa ninapokuwa mbali. Hivi sasa niko mbali na nina hofu kwamba wanaweza kumnasa. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mapenzi ya dhati huwa yamejengwa katika msingi wa uaminifu. Vijana unaosema wanamnyemelea mpenzi wako ukiwa mbali hawawezi kufua dafu kwake kama anakupenda kwa dhati. Zungumza naye umwambie awe akijaribu kuwaepuka wakati unapokuwa mbali.

 

Anipigiapigia simu na simjui na wala simtaki

Kwako shangazi. Tafadhali nahitaji msaada wako. Kuna mwanamume ambaye amekuwa akinisumbua kwa simu kuhusu jinsi anavyonipenda ilhali sijawahi kumuona wala sijui alivyopata nambari yangu ya simu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Wanawake wengi wamejipata katika hali hiyo siku hizi kwani watu wana njia nyingi za kupata nambari za simu za wenzao. Hujasema mmefikia wapi katika suala hilo. Kama unahisi ni mtu unayeweza kumpa nafasi, panga mkutane ili ujue kama anakufaa. La sivyo, kama hutaki mambo yake na unahisi amekuwa chukizo, kuna jinsi ya kumzuia kukupigia. Kama hujui jinsi ya kufanya hivyo, tafuta msaada kutoka kwa wataalamu wa simu.