Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Hajanitenda ila kuna wakati nashuku penzi lake

May 29th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina mwanamume mpenzi wangu ambaye tunapendana sana. Hasa amenizuzua kwa maumbile na tabia zake. Lakini wakati mwingine nimekuwa nikishuku ana wanawake wengine ingawa pia sina uhakika kwa sababu ninaamini mapenzi yake kwangu ni ya dhati. Ni kwa nini?

Kupitia SMS

Inaonekana kwamba mapenzi kati yenu yamepenya moyo na akili yako hivi kwamba huwezi kudhania kwamba mpenzi wako anaweza kumpenda mwanamke mwingine. Kwa kuwa una hakika wewe pekee ndiye wake, unafaa kuamini kuwa unastahili penzi lake na ndiyo maana alikuchagua wewe miongoni mwa wengine wengi.

 

Mpenzi afanya kazi mbali, tutamudu?

Shikamoo shangazi! Mpenzi wangu anafanya kazi mbali na imekuwa vigumu kwetu kuonana. Nahisi kuwa hali hiyo inaathiri vibaya uhusiano wetu na hali itakuwa mbaya hata zaidi tukioana. Nishauri.

Kupitia SMS

Kwa sasa sioni kama kuna shida sana bora tu kila mmoja anamwamini mwenzake na mnaonana nafasi inapopatikana. Tatizo litakuwepo mkioana kwani mtahitaji kuishi pamoja. Itabidi muanze kushughulikia jambo hilo sasa. Ikiwezekana mtafutie kazi karibu na ulipo.

 

Kumbe alinipa ahadi hewa tu, nifanyeje?

Vipi shangazi. Kuna msichana tuliyejuana akiwa shuleni na nikamsaidia kwa sana kwa sababu aliniahidi kuwa akimaliza masomo atakuwa mke wangu. Amenishangaza sana kwa kuniacha ghafla bila sababu kwa ajili ya mwanaume mwingine. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ninaelewa unavyohisi. Hata hivyo, katika dunia hii sio kila mtu anayelipa wema kwa wema. Kunao wenye tabia sawa na punda, ambaye asante yake ni mateke. Usijute kwa kumsaidia, Mungu atakulipa tena maradufu. Badala yake, jaribu uwezavyo kumsahau.

 

Nimemzimikia kichizi lakini nasikia ana mwingine

Vipi shangazi? Kuna mwanamume ambaye ninampenda sana lakini nimeulizia nikaambiwa ana mwingine. Nifanye nini na nampenda?

Kupitia SMS

Ni lazima ujifunze kuelewa na kukubali ukweli wa mambo. Kama umeambiwa kuwa mwanaume huyo ana mwingine, ina maana kuwa huwezi kumpata hata kama unampenda. Huwezi kumlazimisha amuache aliye naye kwa hivyo msahau na utafute wako.

 

Matusi yamenifanya kushuku penzi lake

Kwako shangazi. Mwanamume niliyeamini ananipenda juzi alinishambulia kwa matusi mazito nikashangaa. Ingawa nilikuwa nimemkosea, matamshi aliyotoa yamenifanya niamini kuwa hanipendi bali anajifanya tu. Siku mbili baadaye alinipigia simu kuniomba msamaha akidai yote aliyosema yalitokana na hasira. Nishauri.

Kupitia SMS

Nijuavyo ni kuwa kuna watu wengine ambao wakikasirika wanaweza kusema au kufanya chochote. Kuna usemi kuwa hasira ni hasara na ni hatari kuishi na watu wa aina hiyo. Hata hivyo, kama amekuomba msamaha itakuwa vizuri umpe nafasi nyingine. Lakini ukiona hali hiyo inajirudia mara kwa mara, nitakushauri ujiondoe katika uhusiano huo.

 

Amekana anisaliti ila nimeamua kujiondoa

Shangazi nimekuwa nikipata habari kuwa mwanamume mpenzi wangu ana mwanamke mwingine. Amekana habari hizo lakini mimi nimeamua kumuacha. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Si jambo la busara kutegemea habari za watu kufanya uamuzi kama huo kwa sababu wanaweza kukuhadaa. Sijui ni kwa nini unaonekana kuwa na hakika kuwa mpenzi wako ana mwingine ilhali umeambiwa tu. Nakushauri uchunguze mwenyewe ujue ukweli ndipo uchukue hatua hiyo.

 

Sina haja na mpenzi wake, nimwelezeje?

Kwako shangazi. Kuna mwanamke rafiki yangu wa miaka mingi anayeshuku kuwa ninamtaka mpenzi wake. Sijui amepata wapi habari hizo kwani ameanza kusepa. Juzi alinitumia SMS kuniambia niachane na mpenzi wake. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Iwapo hujafanya jambo lolote lenye dalili kuwa unamtaka mpenzi wake huyo, inawezekana kuna mtu anayetaka kuchochea uhasama kati yenu. Ni muhimu umtafute ujue sababu anakushuku kisha umweleze wazi huna haja na mwenzake.