Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Hata tukosane vipi huwa sibanduki, ni mapenzi?

June 13th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Mimi nina mpenzi lakini kuna jambo fulani ambalo ninashindwa kuelewa kuhusu uhusiano wetu. Tumekosana vibaya mara kadhaa na hata kumaliza miezi bila kuonana wala kuwasiliana. Lakini hatimaye hujipata pamoja. Kila tunapokosana huwa najaribu sana kumsahau lakini ninashindwa. Hiyo ni kawaida kweli?

Kupitia SMS

Naam, hiyo ni kawaida kwa watu wanaopendana kwa dhati. Hata wakikosana namna gani, inakuwa rahisi kwao kusahau tofauti zao kwa sababu nguzo ya uhusiano wao ni mapenzi ya dhati. Hiyo ndiyo sababu mnakosana kwa miezi kadhaa na hatimaye mnarudiana.

 

Amekubali ana mke lakini kanikwamilia

Kwako shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja na nimegundua kupitia kwa rafiki yake kwamba ana familia ingawa hajaniambia. Nimemuuliza akakiri lakini anasisitiza kuwa hawezi kuniacha. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni bahati kubwa kwamba umepata habari hizo mapema kabla hujapoteza muda wako mwingi kwa mwanamume huyo. Sasa ni juu yako kuamua iwapo utaachana naye ama utakuwa mpango wake wa kando. Madai eti amesema hatakuacha hayana msingi kwani hawezi kukulazimisha kumpenda.

 

Amekatalia halua na hata huwa mkali

Hujambo shangazi? Kuna jambo moja ambalo nimeshindwa kuelewa kumhusu mpenzi wangu. Tumependana sana na mwanamke huyo kwa miaka mitatu lakini amekataa kabisa nionje asali angalaU niamini kuwa ananipenda. Kila nikimgusia kuhusu suala hilo hugeuka kuwa mkali na kutishia kuniacha. Ni kwa nini?

Kupitia SMS

Kuna mambo yasiyoweza kulazimishwa katika uhusiano na hilo ni mojawapo. Iwapo una hakika kuwa mwanamke huyo anakupenda, hiyo inatosha si lazima uonje asali. Msimamo wake ni ishara kuwa hayuko tayari kwa jambo hilo sasa na ukisisitiza atadhani kuwa hiyo ndiyo nia yako kwake na anaweza kukuacha. Nenda taratibu.

 

Anuka shombo hata kulala naye balaa tu!

Shikamoo shangazi! Nina mwanamume mchumba wangu tunayependana sana. Hata hivyo kuna jambo fulani kumhusu ambalo hunichafua sana roho kila tunapokuwa pamoja. Mwenzangu ni mnene na mara nyingi hutokwa na jasho ambalo hunuka vibaya sana. Ukweli ni kuwa akinioa leo sitaweza kulala naye kitanda kimoja. Sijui iwapo anafahamu hali yake hiyo na naona aibu kumwambia. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Hiyo ni hali inayopatikana kwa watu wengi wakubwa kimaumbile na mara nyingi mtu mwenyewe huwa hajui. Kuna jinsi za kukabiliana na harufu mbaya inayotokana na jasho mwilini. Mtu kama huyo anatakiwa kuoga ipasavyo, kuvaa nguo safi kila mara na kutumia manukato. Huyo ni mpenzi wako na hufai kuona aibu kumwambia kwani usipofanya hivyo ni wewe utaendelea kuumia. Tafuta wakati mzuri umweleze kwa upole na bila shaka ataelewa.

 

Huyu ndiye barafu ya moyo wangu?

Kwako shangazi. Kuna mwanamume tunayefanya kazi pamoja ambaye ananitaka. Ameniambia wazi kuwa amekuwa na mpenzi lakini wakaachana hivi majuzi baada ya kugundua mapenzi yake hayakuwa ya dhati. Ameniambia anatafuta mwanamke ambaye atamuonyesha mapenzi hadi ahisi kuwa kweli anapendwa. Ni mwanamume mchangamfu na mkarimu sana na ameteka hisia zangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Kupendwa na kupenda kuna raha. Lakini kumbuka kwamba mapenzi pia yana hadaa. Huenda aliyokwambia mwanamume huyo kuhusu sababu ya kuachana na mpenzi wake ni kweli ama uongo. Labda ni miongoni mwa wanaume wasiokuwa na msimamo, wanaopenda kuonja huku na kule. Hata huenda ndiye aliyeachwa kutokana na tabia kama hiyo. Ninakwambia yote haya kwa sababu nimejua unampenda mwanamume huyo kwa hivyo nataka uwe na subira usije ukatumbukia mikononi mwa laghai wa kimapenzi.