Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Jamaa wa mke wametufilisisha, sijui nifanye nini

December 30th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nahitaji ushauri wako tafadhali. Nimeoa kutoka kwa familia maskini. Mimi na mke wangu tunafanya kazi lakini mapato yetu yanatosha tu kujikimu kimaisha. Tatizo ni kwamba umekuwa mtindo wa wazazi na jamaa zake wengine wa karibu kudai pesa kutoka kwetu mara kwa mara na tabia yao hiyo imetufanya tushindwe hata kuweka akiba kwa ajili ya siku zijazo. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni jambo la maana kusaidia wazazi na jamaa wa familia ya mke wako. Hata hivyo, huo kamwe si wajibu wako. Kama umetimiza malipo ya mahari kulingana na utaratibu uliopewa, hawafai kudai kingine zaidi kutoka kwako. Wanafaa kuelewa kwamba mna familia iliyo na mahitaji ya kifedha na pia mnataka kutafuta namna ya kujitegemea kifedha kwa sababu hamtafanya kazi ya kuajiriwa maisha yenu yote. Zungumza na mke wake ili atafute jinsi ya kushauriana na wazazi wako kuhusu jambo hilo.

 

Nimetimu miaka 28 na sina mpenzi ila tuliyefahamiana juzi naarifiwa ana mpenzi

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 28 na sina mpenzi. Kuna mwanamume tuliyekutana katika sherehe fulani majuzi na akateka hisia zangu. Tulifahamiana na akanipa nambari yake ya simu. Nilikuwa na matumaini makubwa kwamba nitampata lakini nimeulizia wanaomjua wakaniambia ana mpenzi. Nashindwa kuamini kwa sababu angekuwa na mpenzi hangenipa nambari yake ya simu. Nampenda sana. Nishauri.

Kupitia SMS

Mapenzi yako kwa mwanamume huyo yamekuteka akili hivi kwamba hutaki kukubali wala kuelewa ukweli wa mambo. Uliwauliza watu wanaomjua ukitaka ukweli kuhusu jambo hilo. Mbona sasa hutaki kuwaamini? Kama huamini, mtafute yeye mwenyewe umuulize. Na iwapo ni kweli, hiyo ina maana kuwa huwezi kumpata hataka kama unampenda.

 

Aliyenioa hajui kwetu ila haonyeshi dalili

Mambo shangazi? Niliolewa na mpenzi wangu mwaka uliopita baada ya kuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa miaka minne. Kwa muda wote ambao tulikuwa wapenzi, hatujawahi kwenda nyumbani kwetu lakini alinipeleka kwao na wazazi wake wananijua. Ninahisi kuwa ni makosa kuendelea kuishi na mwanaume ambaye wazazi wangu hawamjui. Nimekuwa nikitaka twende kwetu lakini mwenzangu haonekani kuwa na haraka. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hatua mliochukua ni ya mkato, haikufuata utaratibu. Punde tu baada ya mpenzi wako kukutambulisha kwa wazazi wake, mlifaa kwenda kwenu ili nao wazazi wako wamuone na kufahamiana naye. Kama hilo halikuwezekana, basi mlifaa kwenda kabla ya kuoana. Ni muhimu mfanye hivyo haraka iwezekanavyo. Ni juu yako umwelezee mume wako unavyohisi kuhusu jambo hilo ili aweze kulizingatia. Mmekawia, lakini si neno, bora tu mfike.

 

Mwanamume niliyempa moyo wangu wote amenitupa, sasa sioni kama nitaishi bila yeye

Shikamoo shangazi! Mwanamume niliyempa moyo wangu wote ameniacha ghafla bila kuniambia sababu ya hatua yake hiyo. Alikuwa kila kitu kwangu na sijui kama niaweza kuishi bila kuwa naye. Tafadhali nisaidie.

Kupitia SMS

Hujaelezea unataka nikusaidie kwa njia gani. Ukweli ni kuwa sina uwezo wa kumtafuta mpenzi wako huyo na kumrudisha kwako. Hatua yake ya kukuacha ni ishara kwamba hakutaki tena katika maisha yake. Kauli yako eti huwezi kuishi bila yeye si ya kweli. Kila mtu ana maisha yake na hakuna aliyeumbwa ama anayeishi kwa ajili ya mwingine. Jinsi tu ulivyokutakana naye ukampenda, unaweza kukutana na mwingine umpende. Unachohitaji kufanya ni kukubali kwamba amekuacha na ujaribu uwezavyo kumsahau. Ni kwa njia hiyo tu ambapo utaweza kufungua moyo wako kwa mpenzi mwingine.