Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Je, huenda mke wangu ana uhusiano wa pembeni?

February 21st, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nina mke ambaye tumeishi pamoja kwa mwaka mmoja sasa. Hata hivyo kuna jambo fulani ambalo nimegundua kumhusu na ninahofia linaweza kutatiza ndoa yetu. Nimepata katika simu yake mawasiliano ya SMS kati yake na wanaume wengine. Ninamwamini sana na nitashangaa nikijua kuwa ana uhusiano nje ya ndoa. Nishauri.

Kupitia SMS

Hujaelezea iwapo jumbe ambazo umeona katika simu ya mke wako ni za kimapenzi ama ni mazungumzo ya kawaida. Kama ni mazungumzo ya kawaida, huna sababu nzuri ya kumshuku kwani huenda hao ni marafiki tu ama labda wanafanya kazi pamoja. Kama ni jumbe za kimapenzi, basi kuna tatizo. Ni muhimu umuulize ili ujue ukweli na kuchukua hatua inayofaa.

 

Ana mimba yangu lakini ameniambia hana mpango wa kuolewa, nifanyeje?

Mambo shangazi? Nina mpenzi na nilikuwa nimepanga kumuoa katika muda wa miaka miwili ingawa hatujazungumzia jambo hilo. Kwa bahati mbaya, amepata mimba na nimeamua kumuoa mara moja ili kumuondolea aibu ya kupata mtoto akiwa kwa wazazi wake. Lakini ameniambia hana mpango wa kuolewa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kwa kawaida, mapenzi ya dhati yanafaa kupeleka wahusika hadi katika ndoa. Ni jambo la kushangaza kwa mpenzi wako kukuelezea uamuzi wake huo baada ya kubeba mimba yako. Ni lazima ana sababu kubwa na ambayo hangetaka ujue. Huenda hata ana mpenzi mwingine na labda mimba hiyo ni yake wala si yako. Ukweli ni kwamba huwezi kubadili uamuzi wake huo na itabidi uachane naye.

 

Kipusa wangu akiguswa kidogo tu na wanaume huwa analegea

Shangazi pokea salamu zangu. Nina tatizo fulani ambalo linahitaji ushauri wako. Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye nampenda sana. Tatizo lake ni kuwa ni mdhaifu sana kwa wanaume, akiguswa kidogo tu, anasalimu amri. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Tabia ya mpenzi huyo inatia hofu na si ya kawaida hasa kwa mwanamke. Wewe mwenyewe unajua kwamba mwanamke mwenye tabia kama hiyo hafai kwa uhusiano wala ndoa na sielewi unahitaji ushauri gani mwingine kutoka kwangu. Itabidi umuache ama umvumilie na tabia yake hiyo.

 

Nimehamishwa kazi mbali sasa upweke unanipa mawazo ya kuwa na kimada

Shikamoo shangazi! Nimeoa na tumejaliwa watoto wawili. Huu ni mwezi wa pili tangu nilipohamishwa kikazi na kupelekwa mbali na nyumbani. Kutokana na mazoea ya kuishi na familia yangu nimeingiwa na upweke na pia mawazo ya kutafuta mpango wa kando. Lakini nampenda mke wangu na sitaki kumkosea. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Bila shaka hali yako hiyo imetokana na kuwa mbali na familia yako. Hata hivyo, itakuwa ya muda tu kwani nayo pia utaweza kuizoea. Kumbuka kuwa uaminifu ni muhimu katika ndoa. Kama unampenda mke wako, usikubali kujiingiza katika hali inayoweza kukushawishi usaliti ndoa yako. Kwa sasa, mawasiliano ya mara kwa mara kwa simu yanaweza kukusaidia kuondoa upweke na mawazo mengine yasiyofaa.

 

Mbona hanitamani tena baada ya kukubali nionje asali?

Hujambo shangazi? Kuna mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miezi kadhaa. Mwezi uliopita alikubali kunifungulia mzinga kwa mara ya kwanza. Ajabu ni kuwa tangu hapo naona mapenzi yake kwangu yamepungua. Awali haingepita hata siku moja kabla hatujawasiliana. Sasa wakati mwingine nampigia simu anapuuza. Unafikiri ni kwa nini?

Kupitia SMS

Kama umeona mabadiliko hayo baada ya nyinyi kushiriki mahaba, ina maana kuwa hicho hasa ndicho kiini. Inawezekana kuwa hukutimiza matarajio yake na ameamua kuwa huo ndio utakuwa mwisho wa uhusiano wenu. Hata hivyo, ni muhimu umtafute uzungumze naye kuhusu jambo hilo ili ujue ukweli wake.