Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Jike lilinialika kwake nikalikagua, sasa limeniganda

May 7th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 26. Juzi mwanamke jirani yangu katika mtaa ninamoishi alinialika kwake kwa chakula cha mchana na baadaye akanishawishi nimhudumie chumbani. Nilikubali ombi lake nikidhani hayo yangeishia hapo, lakini tangu siku hiyo amekuwa akiniandama akitaka tuwe wapenzi. Nilimsaidia tu, sina hisia kwake. Isitoshe, ni mama wa watoto watatu na siko tayari kuwa baba wa watoto wasio wangu. Nitamwepuka vipi?

Kupitia SMS

Inawezekana kwamba mwanamke huyo amekuwa akitafuta mume na alipanga kutumia mbinu hiyo kukunasa. Usikubali kabisa kuingia katika mtego wake huo kama unaamini hafai kuwa mke wako. Jinsi pekee ya kumuepuka ni kuhama mtaa huo na kukatiza mawasiliano naye hata kama ni kubadilisha namba yako ya simu.

 

Alinipa mimba ila hakunioa, sasa ataka niwe mkewe wa pili

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 22 na nilipata mtoto nikiwa katika shule ya upili. Niliolewa na mwanamume mwingine na tukapata mtoto wa pili pamoja lakini tukaachana. Baba wa mtoto wa kwanza ameoa kwa miaka mitatu sasa lakini hawajapata mtoto. Anashuku kuwa mkewe ndiye mwenye kasoro na sasa anataka kunioa mke wa pili. Ukweli ni kuwa bado nampenda. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Uamuzi wako utategemea iwapo uko tayari kuolewa mke wa pili. Itabidi pia mwanaume huyo ashauriane na mke wake kuhusu mpango wake huo wa kuoa mke wa pili kwani ukiolewa bila idhini yake ndoa yako haitakuwa na amani. Kama haya yanawezekana, itakuwa heri kwako.

 

Asema alitafuta dume eti kwa sababu mimi simridhishi kimahaba

Kwako shangazi. Nimekuwa na uhusiano na mwanamke ninayempenda sana kwa miaka miwili sasa. Sijawahi kumshuku hata siku moja na nimeshangaa sana kugundua kwamba ana mpango wa kando. Ameungama kitendo chake hicho akidai eti aliamua kutafuta mwanamume wa pembeni kwa sababu huwa simtoshelezi. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mpenzi wako anatumia hicho kama kisingizio tu kwa sababu umegundua mchezo wake. Yeye ni mpenzi tu, si mke wako na kama alihisi kuwa hapati huduma nzuri kutoka kwako alikuwa na uhuru wa kukwambia ukweli kisha kujiondoa katika uhusiano huo. Inawezekana ni sampuli ya wanawake wasiotoshe na mwanaume mmoja ama amekuwa akifaidi kwa mambo mengine kutoka kwa mwanamume huyo mwingine.

 

Tafadhali nitafutieni dawa ya tatizo la kumalizia haraka

Kwako shangazi. Nimekuwa na mpenzi kwa miezi kadhaa sasa lakini anatishia kuniacha. Sababu ni kuwa ninashindwa kumshughulikia ipasavyo na anasema hawezi kuvumilia hali yangu hiyo katika ndoa. Shida yangu hasa ni kumaliza shughuli haraka. Nitapata wapi dawa ya tatizo hilo?

Kupitia SMS

Uhusiano na ndoa hudumishwa kutokana na kila mhusika kuvumilia udhaifu wa mwenzake. Mpenzi wako hafai kutishia kukuacha kwa sababu ya hali yako hiyo iwapo anakupenda kwa dhati. Badala yake anafaa kukusaidia kutafuta suluhisho. Muone mtaalamu wa afya ya uzazi uone kama atakufaa.

 

Ninashuku mume wangu ana jambo la siri na mjakazi wetu

Hujambo shangazi? Ninashuku kwamba mfanyakazi wangu wa nyumbani ana uhusiano na mume wangu. Nimekagua simu yake na kugundua kuwa wamekuwa wakipigiana simu mara kwa mara. Sitaki kumuuliza mume wangu kwani hiyo ni aibu kubwa kwake. Nishauri.

Kupitia SMS

Si jambo la kawaida kwa mwanamume mwenye nyumba kuwa na mazoea na mfanyakazi kiasi cha wao kupigiana simu. Ninaamini kuwa wewe ndiwe unayeajiri wafanyakazi wa nyumbani kwenu kwa hivyo una uwezo wa kumwachisha kazi mfanyakazi huyo kama unahisi amekuwa tishio kwa ndoa yako.