SHANGAZI AKUJIBU: Kidosho wangu ataka kuzaa kabla tuoane rasmi!

SHANGAZI AKUJIBU: Kidosho wangu ataka kuzaa kabla tuoane rasmi!

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nina uhusiano na mwanamke fulani mrembo sana na nimeamua kuwa ndiye atakuwa mke wangu. Mipango ya ndoa bado lakini anasema anatamani mtoto. Nimemwambia asubiri hadi nimuoe lakini anashikilia kuwa mtoto hawezi kuzuia ndoa. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Si jambo la kawaida kwa mwanamke kudai mtoto kutoka kwa mpenzi wake kabla ya ndoa. Bila shaka mwenzako ana sababu anayoijua mwenyewe. Huenda anahofia kuwa unaweza kunaswa na mwanamke mwingine na anaamini kuwa mkizaa pamoja atakuwa amekufunga. Shikilia msimamo wako kisha utafute namna ya kumuondolea hofu hiyo.

 

Nimempachika mimba lakini hayupo moyoni, itakuwaje?

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na uhusiano na msichana ambaye ametoka jamii tofauti na yangu. Kwa bahati mbaya nimempa mimba na ukweli ni kwamba simpendi. Wazazi wangu pia hawamtaki. Lakini naye anasisitiza kuwa wazazi wake wamesema ni lazima nimuoe. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kamwe, siamini eti umekuwa na uhusiano na msichana ambaye humpendi, awe anatoka jamii yako au la. Je, ina maana kwamba ulikuwa unamtumia tu, hukuwa na nia nyingine kwake? Uongo mtupu! Ukweli ni kwamba unataka kumtoroka kwa sababu umempa mimba na hutaki kuwajibika katika kumlea mtoto. Lakini fahamu kuwa maji ukiyavulia nguo ni lazima uyaoge. Huo ni mzigo wako na ukijaribu kuuhepa ndio utawajua vizuri wazazi wake.

 

Tuliyewachana ataka tufufue penzi la kale

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 27 na nimeoa. Hapo awali kabla sijaoa nilikuwa na uhusiano na mwanamke fulani na tulikuwa tumepanga ndoa. Lakini aliniacha akaolewa na mwanamume mwingine ingawa waliachana baada ya muda mfupi tu. Nilipata mwanamke mwingine nikamuoa. Sasa mpenzi wangu huyo wa awali amekuwa akinipigia simu na kunitumia SMS kila mara akiniambia eti bado ananipenda ilhali anajua kuwa nina mke. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Unasema kuwa mwanamke huyo alikuacha akaolewa na mwanamume mwingine naye pia akamuacha. Kwa nini unamruhusu kutatiza amani ya moyo wako ilhali ulimsahau na ukaamua kuendelea na maisha yako? Aliharibu ndoa yake na nia yake hasa ni kukuharibia wewe pia. Usimpe nafasi hiyo. Mwambie wazi kuwa tayari una familia na hakuna nafasi yake katika maisha yako.

 

Namtamani sana mpenzi aliyeniwacha

Kwako shangazi. Mwanamume mpenzi wangu tuliyependana sana aliniacha baada ya kunipata na mwanamume mwingine. Ninaumia sana moyoni kwa kukosa mapenzi yake na sijui nitafanya nini. Tafadhali nipe ushauri.

Kupitia SMS

Ingawa hujaelezea mpenzi wako aliwapata mkifanya nini na huyo mwanamume mwingine, jinsi pekee ya kujua iwapo kuna uwezekano wa kufufua uhusiano wenu ni kumtafuta umwelezee hisia zako. Akikubali itakuwa heri kwako, akikataa itabidi utosheke na uamuzi wake.

 

Nampenda ila ni mjeuri na ana dharau

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 22 na mscichana mpenzi wangu ana miaka 19. Tumekuwa pamoja kwa mwaka mmoja sasa na nina mapenzi ya dhati kwake tena nimejitolea kwake kwa moyo wangu wote. Lakini ninashuku iwapo ananipenda kwani mara nyingi huwa mjeuri kwangu na pia kunidharau. Nishauri.

Kupitia SMS

Mpenzi ni chaguo la mtu binafsi na mapenzi hudumu kutokana na kila mmoja kumpenda mwenzake. Kulingana na maelezo yako, ninahisi kuwa mapenzi katika uhusiano wenu yanatoka upande wako tu, ni kama mwenzako anajilazimisha tu. Mtu anayekupenda hafai kuwa mjeuri kwako ama kukudharau. Hizo ni dalili za uhusiano ambao unaelekea pabaya. Ningekuwa wewe ningejiondoa mapema.

You can share this post!

Saba wauawa raia wa Sudan wakianza upya maandamano

Kwaheri Bob

adminleo