Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Kipusa anayetosha mboga haamini ninachomwambia

September 14th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na wanawake kadhaa maishani. Lakini hakuna kati yao aliyetosha kuwa mke wangu. Kuna mwanamke fulani ambaye tumekuwa marafiki kwa miaka mingi na ninaamini ananifaa. Nimemwambia lakini anafikiri ninamchezea kwa sababu anawajua wapenzi wote niliowahi kuwa nao na nikawaacha. Nifanye nini ili aniamini?

Kupitia SMS

Bila shaka itakuwa vigumu sana kwake kuamini kuwa unamaanisha unayomwambia iwapo amekuona ukishikana na wengine na kuwatema. Itabidi utumie mbinu mbalimbali za kumhakikishia kuwa yeye ndiye chaguo lako. Kwa mfano, unaweza kumpeleka kwenu kumjulisha kwa jamaa zako na pia uende kwao uwalezee jamaa zake nia yako. Kwa njia hiyo anaweza kuamini kuwa umeamua.

 

Ngoma yamshinda, asema hajielewi pia

Salamu kwako shangazi. Nina umri wa miaka 24 na huu ndio mwaka wangu wa kwanza tangu niolewe. Kwa hakika ninampenda mume wangu kwa dhati. Lakini sielewi ni kitu gani kimetendeka kwake kwa sababu ameanza kulemewa na kazi chumbani na mara nyingi huniweka na njaa. Nimemuuliza akasema yeye pia haelewi. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kuna mabadiliko ya kila aina yanayotokea ndani ya mili yetu na kutuathiri kwa njia mbalimbali. Inawezekana kuwa hali ya mume wako imetokana na mabadiliko fulani mwilini na ndiyo sababu hata yeye mwenyewe haelewi kinachoendelea. Shauriana naye amtembelee mtaalamu wa afya ya uzazi akaguliwe ili ijulikane kama anaweza kusaidiwa.

 

Aliniacha sababu ya mimba, bahati mbaya ikaharibika sasa ananitafuta

Vipi shangazi? Mwanamume aliyekuwa mpenzi wangu alinipa mimba na nilipomwambia akaikana na kuniacha. Kwa bahati mbaya, mimba hiyo iliharibika. Sasa amekuwa akinipigia simu karibu kila siku akiomba turudiane. Nishauri.

Kupitia SMS

Kitendo cha mwanamume huyo cha kukuacha baada ya kujua kwamba una mimba yake ni thibitisho kamili kuwa hakupendi kwa dhati. Kama ungepata mtoto sasa ungekuwa na mzigo wa kumlea peke yako na kamwe hungemuona baba yake huyo. Ningekuwa wewe ningetafuta maisha kwingine wala singemsikiliza hata dakika moja.

 

Sipati mume kwa madai eti nina tabia za watu wa mjini

Vipi shangazi? Mimi nimezaliwa mjini na nimekuwa nikiishi na mzazi wangu kwa zaidi ya miaka 20. Nimehitimu umri wa kuolewa lakini wanaume wamekuwa wakiniepuka kwa madai eti nimeathiriwa vibaya na maisha ya mjini. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Kama kweli kuna wanaume ambao wanaamini mwanamke aliyezaliwa na kuishi mjini hawezi kuolewa, basi hao wametawaliwa na mawazo ya ushamba na itikadi zilizopitwa na wakati. Maisha ya mtu yeyote yule hutegemea malezi na tabia yake binafsi. Kuna wengi waliozaliwa na kulelewa mashambani ambao hawajaolewa kutokana na tabia zao mbaya. Usiwe na shaka, siku moja utakutana na mwanaume atakayekupenda na kukuheshimu bila kujali mahali ulikozaliwa na kulelewa.

 

Nimelemewa na kazi za chumbani, tafadhali nisaidie

Kwako shangazi. Nimeoa na tumejaaliwa mtoto mmoja. Nimeamua kuja kwako unisaidie kwa sababu nimelemewa na wajibu wangu kama mwanamume. Ghafla nimeanza kulemewa na shughuli za chumbani na sielewi ni kwa nini. Mke wangu ni mchanga na ninahofia kuwa ataanza kwenda nje. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kuna mambo kadhaa unayofaa kuzingatia kuhusu suala hilo ukiwemo umri, majukumu mengine ya kimaisha uliyo nayo na hali yako ya afya. Mawazo mengi kuhusu maisha na magonjwa pia yanachangia hali hiyo. Iwapo unaamini hali yako haitokani na mambo haya, basi ni muhimu umuone mtaalamu wa afya ya uzazi ili ujue kiini cha hali yako hiyo.