Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Kipusa mpenzi ameanza ghafla kubugia pombe

September 13th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye nampenda sana. Lakini kuna jambo moja ambalo limenishangaza kumhusu. Ameanza ghafla kunywa pombe ilhali katika miaka miwili ambayo tumejuana sijawahi kumpata akinywa pombe ama akiwa mlevi. Ninachukia sana pombe hata harufu yake siwezi kuvumilia. Nimejaribu kuzungumza naye ili aache lakini naona anaendelea kuzama kwa uraibu huo. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Inawezekana kwamba mwenzako alikuwa na uraibu huo kabla mjuane na akalazimika kuacha kwa sababu yako lakini ameshindwa kuvumilia. Uhusiano wowote ule, uwe urafiki, mapenzi au ndoa unafaa kuwa na masharti ndipo uweze kudumu. Unasema kuwa huwezi kuvumilia harufu ya pombe na hiyo ina maana kuwa huwezi kuishi na mpenzi au mke mlevi. Kama hawezi kuacha uraibu wake huo basi itabidi umuache.

 

Huongea sana na kijana mwingine

Kwako shangazi. Nina mpenzi ninayempenda sana ingawa ninashuku kuhusu hisia zake kwangu. Sababu ni kuwa kuna kijana mwingine ambaye amekuwa akimpigia simu karibu kila siku. Nikimuuliza husema ni urafiki tu. Juzi niliwapata katika maskani fulani ya burudani wakibugia pombe. Je, huo kweli ni urafiki? Nashuku kuwa ninachezewa. Nishauri.

Kupitia SMS

Maelezo yako yanaonyesha kuna zaidi ya urafiki kati ya wawili hao. Ninaamini mpenzi wako ana marafiki wengi na ni ajabu kwamba anatumia wakati wake mwingi na kijana huyo hata labda kuliko wewe ambaye ni mpenzi wake. Ningekuwa wewe ningemkabili nimwambie sitaki kuwaona pamoja tena la sivyo achague kati yangu na huyo mwingine.

 

Nina hofu huenda alipize kisasi kwa kuonja wa pembeni

Hujambo shangazi? Nilikuwa na mpenzi tuliyependana sana ingawa alikuwa anaishi mbali. Wakati fulani nilimkosea kwa kuwa na uhusiano wa kisiri na mwanamume mwingine na alipojua tukakosana. Baadaye nilimuomba msamaha na tukarudiana. Sasa nimekuwa nikiishi na wasiwasi kwamba huenda akalipiza kisasi. Nishauri.

Kupitia SMS

Usaliti wa kimapenzi unauma sana ukigunduliwa. Kama unavyoeleza, mwenzako aliumwa na akakuacha kwa kumsaliti. Lakini yeye mwenyewe aliamua kukusamehe ndipo mkarudiana. Kwa sababu hiyo, hufai kuwa na wasiwasi. Amini kwamba alikusamehe roho safi na akasahau.

 

Natamani watoto na mume hataki tupimwe

Shangazi nimekuja kwako unipe ushauri kuhusu jambo linalonisumbua. Nimeolewa kwa miaka mitano na kufikia sasa bado hatujapata mtoto. Nimekuwa nikimuomba mume wangu twende hospitali tuone kama tutasaidiwa lakini amekataa. Natamani sana kuwa na watoto. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hali kwamba mume wako anapinga wito wako wa kwenda hospitalini ni ishara kuwa labda anashuku ndiye aliye na kasoro na anahofia mkipimwa ukweli utajulikana. Ushauri wangu ni kuwa umuone mtaalamu wa afya ya uzazi peke yako. Akiweza kuthibitisha kuwa unaweza kupata mtoto, itabidi umwambie mume wako ili mshauriane kuhusu mwelekeo wa ndoa yenu.

 

Nashangaa ameoa ilhali aliniambia mie mpenziwe wa kwanza

Hujambo shangazi? Mimi ni mwanafunzi wa chuo kikuu na nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa miaka miwili. Mpenzi wangu amenishangaza sana kuniambia kuwa ameoa. Nimeshangaa kwa sababu tulipokutana aliniambia kuwa mimi ndiye mpenzi wake wa kwanza. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni wazi kwamba mwanaume huyo amekutapeli. Inawezekana mlipokutana alikuwa tayari ameoa ama ameoa bado mkiwa wapenzi huku akikuhadaa kuwa ni wewe tu. Inawezekana pia hajaoa na ameamua kutumia hicho kuwa kisingizio cha kukuacha. Sasa ni juu yako kuamua iwapo utavunja uhusiano huo ama utaendelea naye. Ningekuwa wewe ningejiondoa tu kwani uhusiano huo tayari umeingia doa.