Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Kisa cha kumfumania kimenitia kichaa jamani eeh!

April 25th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI naomba unisaidie. Nina umri wa miaka 25 na nimekuwa kwenye uhusiano na mwanamume ambaye nimemkubali kwa moyo wangu wote awe mwenzangu maishani. Ananipa chochote ninachotaka na penzi lake linanipumbaza nikajihisi kama kwamba ninaishi ahera. Lakini sifa zake zote hizo ziliyeyuka kama barafu juzi nilipomtembelea nikamfumania uchi wa mnyama chumbani mwake akiwa na mwanamke mwingine. Kisa hicho kimenitia kichaa sijui nitafanya nini mimi.

Kupitia SMS

Kupitia kwa kisa hicho, sasa umejua kuwa mpenzi wako si mwaminifu kwako. Ingawa unasema anakupa chochote unachotaka na juu yake penzi la kukata na shoka, sidhani utachagua kuendelea kunufaika kwa njia hiyo ukijua kuwa anakucheza na wanawake wengine. Ningekuwa wewe ningejiondoa katika uhusiano huo.

Nimethibitisha simu ilikuwa ya rafiki tu, nifanyeje turudiane?

Kwako shangazi. Nilimuacha mpenzi wangu majuzi alipopigiwa simu na mwanamume ambaye nilishuku wana uhusiano ingawa aliniambia ni rafiki yake tu. Nimethibitisha ni kweli na ninajuta kwani nampenda kwa moyo wangu wote. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ulikosea kumshuku mwenzako bila ushahidi wowote. Bila shaka kitendo chako hicho kilimkasirisha kwani kilionyesha kuwa humwamini. Si haramu kwa mpenzi wako kupigiwa simu na wanaume bora tu awe mwaminifu kwako. Jaribu kumuomba msamaha uone kama atakubali.

 

Natamani joto la ndoa, mimi na mke ni kama wageni kwetu

Vipi shangazi? Nimeoa kwa miaka minne sasa. Hata hivyo, katika miaka miwili iliyopita, mimi na mke wangu tumeishi kama watu wageni na chumba chetu kimekuwa baridi . Tatizo hili limetokea baada ya kupata watoto wetu watatu. Sijui nitafanya nini ili kuokoa ndoa yangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninavyoelewa maelezo yako ni kuwa hakuna mmoja kati yenu aliye na hisia kwa mwenzake. Hali ikiwa hiyo, inabidi mmoja wa wahusika, hasa mume, atafute namna ya kuchochea na kuamsha hisia za mwenzake ili kurudisha uhai katika ndoa.

 

Nataka kumuambia nampenda lakini yeye hujifungia kwake

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 25 na bado sijapata mpenzi. Moyo wangu umenaswa na mwanamke aliyehamia katika mtaa ninamoishi majuzi. Hata hivyo, nimekosa namna ya kumwelezea kwa sababu anapenda sana kujifungia nyumbani. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kuna usemi kuwa mwenye kiu ndiye huingia kisimani kuchota maji. Kama unampenda kwa dhati mwanamke huyo na huna nia yoyote mbaya kwake, jipeleke huko nyumbani umwelezee haja yako.

 

Anadai kunipenda lakini nimeshindwa kuelewa hisia zake

Shikamoo shangazi! Nina mpenzi ambaye tumejuana kwa miezi mitatu sasa. Tatizo ni kuwa nisipompigia simu mimi anaweza hata kumaliza wiki nzima bila kuwasiliana nami. Nikimtembelea kwake humaliza muda mwingi na marafiki zake nje na nikimuuliza anakasirika. Anadai ananipenda lakini simuelewi. Nishauri.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, mimi nahisi unajilazimisha tu kwa huyo unayemuita mpenzi wako. Kama kweli anakupenda hawezi kumaliza hata siku bila kuwasiliana nawe wala kukuacha peke yako nyumbani akae nje na marafiki. Labda amegundua hakupendi na anashindwa kukwambia, anakuonyesha kwa vitendo. Usiendelee kujisukuma kwake.

 

Shangazi, wanaume kazini wananikera

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 26 na niliajiriwa majuzi tu baada ya kukamilisha elimu ya chuo kikuu. Kuna wanaume wengi mahali ninakofanya kazi ambao wananiandama wakitaka tuwe na uhusiano lakini mimi siko tayari kwa sasa. Nifanye nini ili niwaepuke?

Kupitia SMS

Jinsi pekee ya kuepuka wanaume wasumbufu ni kukatiza kabisa mawasiliano nao na kuepuka sehemu ambako mnaweza kukutana baada ya kazi. Kama wanatumia simu yako, badilisha namba na uhakikishe kwamba hawataipata.