Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Kisomo cha mpenzi wangu kinanitia kiwewe

December 7th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye anasoma chuo kikuu. Mimi sijasoma kama yeye, nilifika darasa la nane tu. Ingawa amekuwa akiniambia kuwa ananipenda, nina hofu kuwa anaweza kutafuta mwingine ambaye amesoma kama yeye. Je, nimuoe sasa ama nisubiri akamilishe elimu?

Kupitia SMS

Hofu yako hiyo imetokana na wewe kutojiamini na kujihisi duni mbele ya mpenzi wako kwa sababu ya kiwango chake cha juu cha masomo. Lakini ningependa ujue kuwa mapenzi hayajui masomo, rangi wala tabaka. Mwanamke huyo amekubali kuwa mpenzi wako akijua kiwango chako cha elimu na kuwaacha wanaume wengine wengi ambao wamesoma. Isitoshe, hata akiamua kukuacha kwa sababu yoyote ile huwezi kufanya chochote kwa sababu ni uhusiano wa hiari si lazima. Ndoa pia si suluhisho kwa sababu akiamua anaweza kujiondoa. Tosheka na uhusiano wenu kwa sasa na uwe na imani kwamba utadumu hadi ndoa.

 

Bado tunalishana mapenzi japo tumetengana

Nilikuwa nimeolewa lakini tukatengana na mume wangu tukiwa na mtoto mmoja. Licha ya kutengana, tumeendelea kuwa wapenzi na pia ananisaidia kulea mtoto ingawa hatuishi pamoja. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, wewe na mume wako mlitengana tu, hamjaachana rasmi. Unasema kuwa mambo mengine yote kati yenu yanaendelea kama kawaida, tatizo pekee ni kwamba kila mmoja wenu anaishi peke yake. Ingawa hujaelezea kilichowafanya mtengane, kuna matumaini makubwa kwenu kuishi tena pamoja kwa sababu bado mnapendana. Unaweza kutumia nafasi hiyo na ujuzi wako wa kimapenzi kumshawishi muungane tena ili muishi kama familia.

 

Tulikuwa wapenzi, akaniacha kwenda kuolewa, sasa anataka kurudi

Kwako shangazi. Nimezaa watoto wawili na mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka minne. Mwezi uliopita aliniacha akaniambia amepata mwanamume mwingine aliye tayari kumuoa. Wiki mbili baadaye ameanza kunipigia simu akitaka turudiane. Waonaje?

Kupitia SMS

Miaka minne ambayo mmekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke huyo ni muda mrefu sana na unafaa kuwa umemuoa. Pili, ni makosa kuzaa naye watoto bila mpango thabiti kuhusu maisha yenu pamoja. Kuna uwezekano mkubwa kwamba aliamua kuchukua hatua hiyo kwa kuhisi kuwa unampotezea wakati. Iwapo bado unampenda, kubali mrudiane na uhalalishe uhusiano wenu kwa kumuoa. Kama huna nia ya kumuoa, mwambie ukweli ili muachane atafute mume.

 

Hawa wapenzi ninavyowaona, kuna mengine ya ziada

Niko na mpenzi ambaye nampenda naye pia anasema ananipenda. Kwa muda wa miaka miwili ambayo tumekuwa pamoja, amekuwa akiwasiliana kwa simu na wanawake wengi ambao anasema ni marafiki tu. Lakini mimi ninashuku kuwa ananidanganya. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa mtu kuwa na marafiki wa jinsia zote, wanaume kwa wanawake. Hali kwamba mpenzi wako amekuwa akiongea na wanawake hao kwa simu hata ukiwepo ni ishara kwamba huenda ni marafiki tu. Kama hujasikia chochote kuhusu mapenzi katika mazungumzo yao ama kuona ujumbe wowote wa kimapenzi kutoka kwa mwanamke mwingine katika simu yake, huna sababu ya kumshuku.

 

Ni miaka mitatu tu lakini mahanjamu yameisha kabisa

Shangazi mimi nimeolewa kwa miaka mitatu na nina mtoto mmoja. Tatizo ni kuwa nimepoteza hisia kabisa kwa mume wangu ingawa ananipenda sana. Hali hiyo inanitia wasiwasi kwa sababu ndoa yetu bado ni changa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hiyo ni hali yenye utata sana hasa kwa sababu unasema mume wako anakupenda. Hata hivyo, iwapo unaamini hali hiyo haitabadilika, ni muhimu ufungue moyo wako kwake umwambie ukweli ili ajue la kufanya.