Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Kumbe nina mke mwenza mashambani na sina habari!

June 15th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO Shangazi! Nimeolewa kwa miaka miwili sasa na ninaishi mjini na mume wangu. Mwanamke rafiki ambaye ni jirani ya mume wangu mashambani alinidokezea kwamba mume wangu ana mke mwingine na watoto watatu huko mashambani. Nimechunguza na kugundua kuwa habari hizo ni za kweli. Mume wangu hajaniambia kuwa ana mke na nafikiria kumkabili kuhusu jambo hilo kwa sababu mimi sikutaka kuolewa mke wa pili. Nshauri.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, inaonekana kuwa katika miaka miwili ambayo umeishi na mume wako, hajakupeleka kwao mashambani na ndiyo maana hata hukuwa na habari kwamba ana mke mwingine. Iwapo umethibitisha habari hizo, una haki ya kumuuliza ili ujue ni kwa nini hajakwambia. Kisha utaamua iwapo utakuwa mke wake wa pili ama utamuacha.

 

Kwa kweli simpendi

Kwako Shangazi. Nilimuacha mwanamume aliyekuwa mpenzi wangu nilipogundua kuwa alikuwa akimtongoza rafiki yangu. Muda si mrefu, nilipata mwingine ambaye tumekuwa pamoja kwa miaka miwili sasa. Ukweli ni kuwa, simpendi na nilimkubali ili kulipiza kisasi. Sasa nataka kumuacha na sijui nitamwambia nini. Nishauri.

Kupitia SMS

Ulifanya makosa makubwa kumdanganya mwanamume huyo kuwa unampenda ukijua vyema kuwa ulitaka kumtumia kulipiza kisasi. Bila shaka unahisi vigumu kumwambia ukweli huo hasa kama anakupenda kwa dhati. Lakini ni heri umwambie badala ya kuendelea kumpotezea wakati.

 

Nahisi anichezea shere

Kwako Shangazi. Nahitaji msaada wako. Niko katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamke fulani lakini ninahisi kuwa mwenzangu ananichezea. Kisa ni kuwa, huwa hataki kabisa tukutane sisi wawili mahali pasipokuwa na watu wengine karibu. Nashindwa kumuelewa.

Kupitia SMS

Hali kwamba mwanamke huyo hataki mkutane faraghani haina maana kuwa hakupendi. Inawezekana kuwa hajakufahamu kiasi cha kukuamini katika hali kama hiyo. Nimesikia visa kadhaa ambapo wanawake wametendewa mambo mabaya na watu wanaodai kuwa wapenzi wao na huenda hiyo ndiyo hofu yake. Pili, yeye ni mpenzi wako kwa hivyo uko huru kushauriana naye kuhusu jambo hilo ili ujue shida yake.

 

Ajiandaa kunitema

Shikamoo Shangazi! Kuna msichana aliyekubali kuwa mpenzi wangu baada ya kunipuuza kwa muda mrefu. Tumekuwa pamoja kwa miezi kadhaa sasa na nimeanza kuona dalili zake kuniacha. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Jinsi tu msichana huyo alivyokubali kuwa mpenzi wako kwa hiari yake, vivyo hivyo ana haki ya kujiondoa katika uhusiano huo. Kama ameamua kukuacha huwezi kumzuia kwa sababu yeye si mke wako. Hata mke wako ana haki ya kukuacha akiamua kuwa hataki kuendelea kuishi katika ndoa.

 

Sina ujasiri kabisa

Shikamoo Shangazi! Mimi ni kijana mwenye umri wa miaka 30 na sina mpenzi ingawa natamani sana kuwa naye. Tatizo langu ni kwamba nina uwoga wa kutongoza wasichana. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Nimesema mara nyingi katika ukumbi huu kwamba hakuna dawa ya woga. Ni juu yako kujieleza mwenyewe kwa mwanamke unayempenda la sivyo utaishi maisha yako yote bila mke.

 

Namjua ni mlaghai

Hujambo Shangazi? Nimeshindwa nitamfanya nini mwanamume ambaye ananitaka akisema ananipenda ilhali ninajua vizuri kuwa ana uhusiano na wanawake wengine wawili. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Sidhani unahitaji ushauri wowote kutoka kwangu kwa sababu unasema unajua mwanamume huyo ana wapenzi wengine. Kama humtaki kwa sababu hiyo, basi mwambie hivyo kwani hawezi kukulazimisha umpende. Na iwapo unataka kuwa mpenzi wake wa tatu uko huru na ni haki yako.

 

Siamini ananipenda

Mimi ni kijana wa umri wa miaka 23. Nina mpenzi ambaye nampenda sana. Pia huniambia ananipenda. Yuko kidato cha nne. Kila kitu anachohitaji namnunulia, lakini naogopa kumwambia anipe burudani na siamini kama ananipenda. Tumekaa naye muda wa miaka miwili. Nisaidie.

Kupitia SMS

Miaka miwili bila shaka umemuelewa mwenzako vizuri. Na kila safari huanza na hatua. Bila kufungua mdomo na kueleza yaliyo moyoni mwako kuhusiana na suala hilo, mwenzako hawezi kujua. Pia utafanya busara iwapo utampatia muda amalize masomo yake kwanza.