Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Kuna jamaa mjini ananitaka ila nahisi ana mke

February 28th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Kuna mwanamume jirani yangu mjini ambaye amekuwa akitaka tuwe wapenzi. Yeye pia ameteka hisia zangu na ninaendelea kuwazia ombi lake kwani bado sijapata mpenzi. Hata hivyo, kuna dalili ambazo nimeona kwake zinazonifanya nishuku kuwa ana mke na singependa kumharibia ndoa mwanamke mwenzangu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kauli yako ya mwisho inaonyesha wazi kwamba unaheshimu nafsi yako na pia unawajali wenzako. Inawezekana kuwa dalili unazoona ni za kweli ama zimechochewa na hali yako ya tahadhari. Kabla hujakubali ombi lake, itakuwa muhimu ujipe muda wa kutosha umchunguze ili uthibitishe ukweli kuhusu dalili unazoona. Ikiwezekana, wajue marafiki zake ili uweze kupata habari zake kutoka kwao.

Mke ananinyima haki yangu ya unyumba

Shangazi nimeoa kwa miaka minne sasa lakini mke wangu amebadilika simuelewi kabisa. Kisa ni kuwa amekuwa akininyima haki yangu na nikimuuliza anadai eti ni mgonjwa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni kweli kwamba mume ana haki yake kwa mkewe naye mke kwa mumewe. Hata hivyo, haki hiyo inafaa kupatikana kwa maelewano si kwa lazima. Kama mwenzako anasema ni mgonjwa, shauriana naye ujue anaumwa wapi ili mshughulikie hali hiyo kwanza. Mapenzi huonyeshwa kwa namna nyingi na mojawapo ni kujali uzima na usalama wa mwenzako.

Nimpendaye hataki nimuoe na mtoto aliyezaa nje ya ndoa

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 28 na kuna mwanamke ambaye nimepanga kumuoa. Alipata mtoto kutokana na uhusiano wa awali na ananiambia siwezi kumuoa akiwa naye anataka kumpelekea baba yake. Nishauri.

Kupitia SMS

Sioni tatizo lolote kama hivyo ndivyo anavyotaka na itawezekana. Kubali kuwa huyo ni mtoto wa mwanaume mwingine na kama yuko tayari kumchukua hiyo ni haki yake. Ninaamini una uwezo wa kupata watoto wako mwenyewe.

Kuna mwanafunzi analilia asali yangu

Vipi shangazi? Mimi ni mwanafunzi wa shule ya msingi na nina uhusiano na mwanafunzi mwenzangu. Amekuwa akinishawishi tuonje asali na anatishia kuniacha nikikataa ombi lake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mapenzi kati ya wanafunzi ni haramu na hatari. Sababu ni kuwa nyinyi ni watoto hamjui wala hamuelewi maana ya mapenzi. Huyo anayetaka asali atakupa mimba na hawezi kukupeleka popote. Pili, mnapoteza wakati badala ya kuzingatia masomo. Ushauri wangu ni kuwa uvunje uhusiano huo mara moja kama hutaki kujuta baadaye maishani.

Ana mwingine ila anadai kunipenda, inawezekana kweli?

Shangazi pokea salamu zangu za dhati. Nimekuwa na uhusiano na mrembo fulani kwa mwaka mmoja sasa. Tulipokutana aliniambia hakuwa na mpenzi. Baadaye niligundua kuna mwingine lakini anasisitiza ananipenda zaidi. Tafadhali nishauri kwani nijuavyo ni kuwa mwanamke hawezi kupenda wanaume wawili.

Kupitia SMS

Ni kweli haiwezekani kwa mtu kuwa na wapenzi wawili kwa wakati mmoja. Lakini fahamu kuwa kuna matapeli wa kimapenzi ambao kwao ni kawaida kuwa na zaidi ya mmoja. Mwambie achague mapema kati yako na huyo mwingine, akishindwa umuondokee.

Mtoto anatunyima raha, habanduki katika chumba chetu

Hujambo shangazi? Nimeoa na mtoto wetu wa kwanza ni msichana ambaye sasa ana umri wa miaka mitano. Tatizo ni kuwa amekataa kabisa kutoka katika chumba chetu cha kulala ingawa ana chumba chake. Tabia yake hiyo inatunyima raha zetu chumbani ingawa mama yake haonekani kujali. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ingawa bado ni mtoto, binti yenu, katika umri wake huo, hafai kuwa akilala katika chumba chenu. Wewe na mke wako mna wajibu wa kumfunza kulala katika chumba chake. Kulingana na maelezo yako, ni kama kwamba mke wako hajaathiriwa na jambo hilo. Ni vyema uketi chini naye mlizungumzie na kupata suluhisho.