Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Kusaka asali nje kumeniletea balaa na mke wangu

March 26th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nilioa miaka mitano iliyopita na tuna watoto wawili. Ilifika wakati mama watoto akashindwa kunishibisha na nikalazimika kutafuta nje. Juzi alitufumania na sasa anatishia kuniacha. Nishauri.

Kupitia SMS

Ulipoamua kumuoa mke wako ulikuwa umetosheka kuwa ndiye anayekufaa. Lakini kutokana na tamaa, ukaona utafute kimada. Hayo ni masaibu ya kujitakia na ningekuwa yeye pia ningekuacha.

 

Mume sasa ameanza kulala nje, nifanyeje?

Habari yako shangazi. Nimeolewa na tuna mtoto mmoja. Nampenda sana mume wangu na sijawahi kumshuku hata siku moja. Lakini siku za hivi majuzi amenishangaza sana kwa sababu ameanza kulala nje. Tabia yake hiyo inanitia hofu. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Kama hujamuuliza sababu yake kulala nje au mwenyewe kujieleza, sijui nitakusaidia vipi. Muulize usikie atasema nini, ukiridhika ni sawa, usiporidhika, uchukulie hizo kuwa dalili za mienendo isiyofaa na umwambie wazi kuwa huwezi kuivumilia.

 

Huumwa na tumbo kila ninaposhiriki unyumbe na mume

Kwako shangazi. Nimeolewa na tumejaliwa mtoto mmoja. Kuna jambo fulani kuhusu mwili wangu ambalo limeanza kunitia wasiwasi katika siku za hivi majuzi. Kila nikishiriki shughuli za chumbani na mume wangu huwa ninaumwa na tumbo kwa karibu wiki mbili mfululizo. Je, ni kwa nini?

Kupitia SMS

Mimi sina uwezo wa kukusaidia katika jambo kama hilo kwa sababu ni suala la kimatitabu ambalo linafaa kushughulikiwa na mtaalamu. Ushauri wangu ni kwamba umuone daktari mtaalamu wa masuala ya uzazi ili akusaidie.

 

Naogopa wanawake!

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 37 na bado sijaoa wala sina mpenzi. Sababu ni kwamba ninaogopa wanawake. Nifanyeje ili nipate mke?

Kupitia SMS

Sielewi ukimpata huyo mke utaishi naye namna gani kama unaogopa wanawake. Sina namna ya kukusaidia lakini nakufahamisha tu kwamba ukiendelea kuogopa wanawake hutawahi kuwa na mke maishani.

 

Ananitesea mtoto na sasa anatishia kuniacha, nishauri

Habari zako shangazi? Nilikuwa nimeoa lakini mke wangu akaaga dunia miaka miwili iliyopita na kuniachia mtoto wetu wa pekee ambaye sasa ana miaka minane. Nilioa mke mwingine mwaka uliopita lakini ameanza kumtesa mtoto wangu. Nimemkanya na sasa anatishia kuniacha. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Ninaamini kwamba ulipomuoa mwanamke huyo ulimwambia ukweli kuwa una mtoto wa marehemu mke wako. Kwa sababu hiyo, kama kweli anakupenda antarajiwa pia kumpenda mwanao. Mtoto wako ni damu yako na kwake kumtesa ni sawa tu na kukutesa wewe. Ni heri muachane kuliko kuendelea kuona mtoto wako akiteswa na mtu anayedai kuwa mke wako.

 

Mpenzi amenizidi kwa miaka 16 nahofu hilo litakuwa tatizo

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 26 na mwanamume mpenzi wangu ana umri wa miaka 42. Nampenda sana ingawa nahisi tofauti ya umri kati yetu ni kubwa sana. Nishauri

Kupitia SMS

Mapenzi ya dhati hukiuka mipaka ya aina nyingi ukiwemo umri. Mahaba na mambo mengine yote yakiwa sawa, umri haufai kuwa hoja. Isitoshe, tofauti iliyopo si kubwa sana, ondoa wasiwasi.

 

Nahisi mume ana tatizo la uzazi, naomba ushauri

Kwako shangazi. Nimekuwa katika ndoa kwa miaka miwili sasa. Mume wangu aliponioa nilikuwa na mtoto kutokana na uhusiano wa awali. Katika miaka hiyo miwili tumejaribu kupata mtoto mwingine lakini hatujafaulu. Ninaamini kuwa mwenzangu ndiye mwenye kasoro. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Huwezi kuwa na hakika kuwa mume wako ndiye mwenye kasoro eti kwa kuwa wewe una mtoto uliyezaa na mwanamume mwingine. Sababu ni kuwa kasoro za kimwili zinaweza kumpata mtu wakati wowote. Ushauri wangu ni kuwa muende hospitalini mkapimwe ili mjue tatizo liko wapi na iwapo linaweza kutatuliwa.