Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mama mkwe na binti zake wananihangaisha

March 30th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nimeolewa lakini kuna jambo linalotatiza ndoa yangu. Mama mkwe na wasichana wake hawanipendi na tunaishi kama maadui. Hali ni mbaya hivi kwamba nikiondoka nyumbani inabidi nimpeleke mtoto wangu kwetu nilikozaliwa ili kuhakikisha usalama wake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Una sababu ya kutokuwa na raha na pia kuwa na wasiwasi kutokana na uhusiano mbaya kati yako na jamaa za mume wako. Kama huoni dalili za hali kubadilika, jambo la kufanya ni kuzungumza na mume wako ili mtafute makao yenu mbali na nyumbani kwao ndipo muweze kupata amani na furaha katika ndoa yenu.

 

Aliyetuma wakora kuniua sasa anataka kurudi kwangu

Shangazi nahitaji ushauri wako. Nilikuwa nimeoa mke lakini nikamuacha alipoanza kutembea nje na kuwa mjeuri kwangu. Wakati fulani alituma wanaume marafiki zake kuniua. Watoto wetu pia walimkataa kutokana na tabia yake hiyo wakarudi kwangu na nimekuwa nikiwalea peke yangu. Hatimaye nilioa mke mwingine na tumeishi kwa amani na upendo. Sasa huyo mke wa kwanza anataka kurudi kwangu na sisi hatumtaki tena katika maisha yetu. Nishauri.

Kupitia SMS

Ingawa hujasema ni miaka mingapi tangu uachane na mke wako huyo, ni wazi kuwa hamuwezi kuishi tena pamoja hasa kutokana na tabia yake na jaribio la kukuua hapo awali. Kama watu wa familia zenu wanajua kuwa ndoa yenu ilivunjika, tumia sheria kumzuia kuingilia maisha yenu kwani watakuwa mashahidi wako. Kama humtaki hawezi kurudi kwako kwa lazima.

 

Amepata mimba ya jamaa mwingine

Vipi shangazi? Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa miaka miwili sasa. Ajabu ni kuwa nimegundua kuwa ana mimba ambayo si yangu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kama kweli hiyo mimba si yako, ni lazima ni ya mwanamume mwingine. Hiyo ina maana kuwa huyo unayemuita mpenzi wako ni ndumakuwili, si mwaminifu kwako. Huo ni ukweli ambao hawezi kukana kwani mimba aliyo nayo ni ushahidi wa kutosha. Ningekuwa wewe ningemuachia huyo aliyempa mimba nitafute mpenzi mwaminifu anayethamini na kuheshimu uhusiano wetu.

 

Aliyenipa nambari ya simu anichezea

Kwako shangazi. Juzi nilikutana na mwanamke fulani katika sherehe fulani na nikampenda. Nimuomba namba yake ya simu na tukakubaliana tuwasiliane baadaye ili tupange siku ya kukutana. Sasa nimekuwa nikimpigia simu anampa dada yake naye anaanza kunitania kwa mambo ambayo hayana maana. Je, ananichezea akili?

Kupitia SMS

Ni wazi kuwa mwanamke huyo hayuko tayari kukutana nawe kwa sasa na ameamua kushirikiana na dada yake kukuchezea akili. Ushauri wangu ni kwamba uwache kumpigia simu. Kama anakutaka atakutafuta mwenyewe kwa sababu ana nambari yako ya simu.

 

Baba ya mpenzi wangu anataka tuwe na uhusiano

Kwako shangazi. Nimekosana na kijana mpenzi wangu kwa sababu ya jambo dogo tu na hatujaonana kwa muda ingawa tunawasiliana kwa simu. Hivi majuzi baba yake alinifuata akaniomba tuwe wapenzi. Nilipomwambia kuwa mimi ni mpenzi wa mwanawe alijifanya kushangaa na kusema hakujua ingawa ninaamini anajua. Ajabu ni kuwa bado anaendelea kunipigia simu akitaka tuwe na uhusiano wa pembeni na mimi hilo siwezi. Nifanye nini ili nimuepuke?

Kupitia SMS

Huyo ni mmoja wa wanaume wa enzi tunanazoishi wasiokuwa na adabu. Ni jambo la kushangaza kwamba anajua wewe ni mpenzi wa mtoto wake na bado anataka muwe na uhusiano wa pembeni. Kwanza, mtishie kuwa akiendelea kukufuata utamwambia mwanawe. Asipoacha, itabidi ubadilishe namba yako ya simu kisha uepuke sehemu zote anakopitia ili msikutane. Asipokuona wala kukusikia kwa muda atakusahau.