Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mapenzi yake ni ya mdomo tu, hakuna vitendo

March 6th, 2018 2 min read

Shikamoo shangazi. Kuna msichana ambaye nampenda kwa dhati lakini nina shaka iwapo yeye pia ananipenda. Sababu ni kuwa ananipenda kwa maneno tu si kwa vitendo. Nifanyeje?
Kupitia SMS

Uhusiano wa kimapenzi huanzia kwa ahadi za maneno wala si vitendo. Kama mwenzako anakuhakikishia kwa maneno kuwa anakupenda, kuwa na subira hadi atakapokuwa tayari kugeuza maneno yake kuwa vitendo.

Mumewe amerudi, nifanye nini?
Shangazi hujambo? Nimekuwa na uhusiano wa miaka mitatu na mwanamke aliyeachana na mumewe na ana watoto watatu. Sasa baba ya watoto wake amerudi. Nishauri.
Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, mwanamke huyo na mume wake wameamua kurudiana. Kama ndivyo, huna budi kujiondoa kwani wenu umekuwa uhusiano tu wala hujamuoa. Sasa amekuwa tena mke wa mwenyewe na itakuwa haramu kuendelea na uhusiano huo.

 

Natafuta mume
Vipi shangazi? Nilimaliza shule 2014 na natafuta mume mwenye sifa zifuatazo: mwokovu, msomi, mwenye maono, mwenye bidi, mkarimu na mwaminifu. Mchezo kando. Tafadhali nisaidie.
Kupitia SMS

Ninaamini wapo wanaume walio na sifa zote hizo. Hata hivyo, siwezi kukusaidia kwani wajibu wangu hapa kutoa ushauri tu wala si kutafutia watu wachumba. Kuwa na subira na uendelee kutafuta, hatimaye uapata. Nakutakia kila la heri.

 

Mchumba amesema siwezi kumuoa
Mwanamke ambaye nilidhani nitamuoa amegeuka akaniambia haiwezekani kwa sababu binamu yake ameolewa na ndugu yangu. Nahofia akiniacha sitaweza kupata mwingine kama yeye. Nifanyeje?
Kupitia SMS

Ingawa hakuna ubaya wowote kwake kuolewa katika familia moja na binamu yake hilo si jambo la kawaida katika jamii na labda limepingwa na jamaa zake. Kwa sababu hiyo, itabidi ukubali tu na uweke matumaini kwamba utapata mwingine anayekufaa.

 

Nilimsaidia sasa anataka nimuoe, tayari nina wake 3
Kuna msichana niliyemsaidia baada ya kupata ajali barabarani nikamsaidia kutibiwa hospitalini na pia kulipwa fidia. Sasa anataka nimuoe na tayari nina bibi watatu. Mimi nilitenda wema tu, sikutaka malipo. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Ulifanya vizuri kumsaidia msichana huyo lakini usikubali atumie ukarimu wako kwa njia isiyofaa. Mwambie wazi kuwa hutaki mke mwingine na kama unahisi amekuwa mzigo kwako ukatize kabisa mawasiliano kati yenu.

Napenda mzee lakini naogopa kusemwa
Nina umri wa miaka 30 na niliachana na mume wangu miaka kadhaa iliyopita. Kuna mzee wa rika ya baba yangu tunayependana sana na yuko tayari kunioa. Nataka sana lakini naogopa kwamba walimwengu watanisema. Nishauri.
Kupitia SMS

Wewe ni mtu mzima na una haki ya kujiamulia mambo yote kuhusu maisha yako. Ukikosa kufanya maamuzi kulingana na moyo wako kwa kuogopa kusemwa utakosa mengi mazuri. Isitoshe, hata ufanye nini, binadamu watakusema tu. Fuata moyo wako na uishi maisha yako.

 

Aliyenibaka anataka kuoa dada yangu
Kwako shangazi. Kuna mwanamume fulani ambaye alinibaka na sasa anataka kumuoa dada yangu. Je, niwatenganishe ama niachane nao? Tafadhali nishauri.
Kupitia SMS

Kama kweli mwanamume huyo alikubaka na ukaweka jambo hilo kuwa siri, huenda dada yako akose kukuamini na badala yake kudhani kuwa unamsingizia mchumba wake kusudi tu kuvunja uhusiano wao. Ni heri uachane nao.

 

Ameninyamazia
Nina mpenzi ambaye tumekuwa pamoja kwa miezi miwili sasa. Siku za hivi majuzi amenishangaza kwani nikimpigia simu ama kumtumia SMS ananyamaza tu. Nishauri.
Kupitia SMS

Si lazima mtu akwambie ndipo ujue hakutaki. Hizo ni ishara kamili za mtu ambaye anataka kumuacha mwenzake bila kumwambia hivyo. Mbona uendelee kupoteza wakati wako?