Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mbona ananihadaa kuwa ana mke na watoto?

March 4th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

HABARI zako shangazi? Nina umri wa miaka 36 na nina mtoto ingawa sijaolewa. Nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani kwa miaka miwili. Tulipokutana, aliniambia ana mke na watoto wawili. Nilishangaa kwa sababu bado ni mdogo, hata nimemzidi umri kwa miaka kadhaa. Hata hivyo, nilimwamini kwa sababu si wanaume wengi wanaofichua haraka kuwa wana familia wanapokuwa wakitafuta mapenzi pembeni. Nimekuwa nikichunguza na nimejua kupitia kwa marafiki zake kuwa hana mke wala watoto. Unafikiri ni kwa nini alinihadaa?

Kupitia SMS

Ni kweli kuwa wanaume wengi wenye familia huogopa kusema ukweli huo wanapotafuta wapenzi nje ya ndoa. Kama umethibitisha kuwa mpenzi wako alikuhadaa, sababu yake ya kukuhadaa inaweza kuwa moja tu. Hana mapenzi ya dhati kwako kwa hivyo alitaka ujue mapema kuwa huna nafasi katika maisha yake ya ndoa. Hiyo ina maana kwamba nia yake hasa ni kukutumia tu. Sasa umejua ukweli, chukua hatua inayofaa.

 

Mpenzi anagawa asali ovyo sasa nimeshindwa kabisa kuvumilia, nifanyeje?

Hujambo shangazi? Nina mwanamke mpenzi wangu ambaye nampenda sana na ningependa awe mwenzangu maishani. Hata hivyo, nimegundua ana udhaifu ambao siwezi kuvumilia. Anagawa ovyo asali yake kwa wanaume. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Utafanya makosa makubwa kuoa mwanamke kama huyo kwa sababu si rahisi kwake kubadilisha tabia yake hiyo. Usije ukafungwa macho na mapenzi uliyo nayo kwake ukajiingiza katika ndoa yenye balaa. Hakuna kitu kibaya katika ndoa kama mume au mke kutokuwa mwaminifu kwa mwenzake.

 

Mwalimu ametisha kufichulia wazazi kuwa nina uhusiano wa kimapenzi

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na nina uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani. Mwalimu wangu amejua na anatishia kuwaambia wazazi wangu. Nina wasiwasi sana hata ninashindwa kulala kwa sababu wazazi wakijua wanaweza hata kuniua. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hali kwamba tishio la mwalimu wako limekuingiza tumbojoto ni thibitisho kwamba unajua kuwa umekosea. Ndiyo; ni makosa sana kwako kuwa na uhusiano wa kimapenzi ilhali bado unasoma na wazazi wako wakijua utakuwa mashakani. Zungumza na mwalimu wako umuombe asiwaambie wazazi wako kisha umhakikishie kuwa utavunja mara moja uhusiano huo.

 

Anataka nihamie kwake kwa kuwa tumepanga ndoa ila hatujaeleza wazazi

Kwako shangazi. Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 28. Huu ni mwaka wa tatu nikiwa katika uhusiano wa kimapenzi. Mpenzi wangu yuko tayari kunioa na anapendekeza nihamie kwake tukiendelea kupanga ndoa. Lakini nina shida na ombi lake hilo kwa sababu bado hatujafahamisha wazazi wetu kuhusu uhusiano wetu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Jambo analopendekeza mpenzi wako haliambatani na utaratibu unaofaa. Kulingana na maadili, mwanamume na mwanamke hawafai kuishi pamoja kabla ya ndoa. Isitoshe, unasema kuwa watu wa familia zenu hawajui kuhusu uhusiano wenu. Jambo muhimu sasa ni kutangaza uhusiano na mpango wenu wa ndoa kwa wazazi wenu. Kama anatamani sana kuishi nawe, mwambie aharakishe mipango ya ndoa.

 

Nampenda ila sasa sijui kama ni sawa kuoa mwanamke aliyekuzidi umri

Shikamoo shangazi! Nina mpenzi ambaye nimepanga kumuoa lakini kuna jambo fulani linalonitia wasiwasi. Amenizidi umri kwa miaka mitano na ninashangaa iwapo ninaweza kuoa mwanamke mwenye umri mkubwa kunishinda. Nishauri.

Kupitia SMS

Unaweza kuoa mwanamke mwenye umri wowote ule bora tu mnapendana. Kamwe, umri hauwezi kuwa kizingiti palipo na mapenzi ya dhati. Hasa tofauti iliyopo kati yenu ni ndogo sana na hilo si jambo linalofaa kukutia wasiwasi.