Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mbona mpenzi alinikana baada ya kuhamia mji tofauti?

January 27th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

HABARI zako shangazi? Mwanamke aliyekuwa mpenzi wangu alihamishwa kikazi hadi mji tofauti. Nafikiri alibadilisha ghafla namba yake ya simu kwa sababu nilijaribu kumpigia mara nyingi bila kumpata. Niliamua kumtembelea mwenyewe kazini kwake. Ajabu ni kwamba aliponiona alinikana mbele ya wafanyakazi wenzake akaniambia hanijui wala hajawahi kuniona. Niliona aibu sana na kufikia sasa sijaelewa maana hasa ya kitendo chake hicho. Bado nampenda. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mwenye macho haambiwi tazama. Kulingana na maelezo yako, kuna ushahidi wa kutosha kwamba mwanamke huyo alikatiza uhusiano wenu siku aliyohamia mji mwingine. Ndiyo maana hakushughulika kukupigia simu tena akabadilisha namba yake. Hatimaye ulijipeleka kwake akakukana peupe hadharani. Je, unahitaji ushahidi gani zaidi kujua kuwa hakutaki tena maishani mwake? Na unasema bado unampenda? Msahau uendelee na maisha yako.

 

Kuna mwanamke ninamtamani lakini nimegundua kuna wengi wanamtaka

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 36. Kuna mwanamke ambaye ameteka moyo wangu na niko tayari kumpata kwa vyovyote vile awe mpenzi wangu. Hata hivyo, nimechunguza nikagundua kwamba kuna wanaume wengine wengi ambao pia wanamtaka. Hali hiyo imenifanya nianze kukata tamaa mapema. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Msimamo wako huo ni ishara ya uoga na kutojiamini. Ni muhimu ufahamu kwamba hakuna kitu kizuri kinachopatikana kwa urahisi. Sababu ni kwamba kitu cho chote kizuri huwavutia watu wengi na huleta ushindani mkubwa. Anayestahimili ushindani huo hadi mwisho ndiye anayekipata. Umesema kuwa uko tayari kumpata kwa vyovyote vile, kwa hivyo ni lazima uwe tayari kumpigania. Fahamu pia kwamba palipo na mashindano pana mshindi na mshindwa. Kuwa tayari kwa matokeo yoyote yale.

 

Mke alihama bila kuniaga, asema amegundua nilimuoa kimakosa, hanipendi

Shangazi pokea salamu zangu za mwaka mpya. Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 39. Nilikuwa na mke na mtoto mmoja. Siku moja nilirudi nyumbani nikapata ameondoka. Hakuwa ameniambia wala hatukuwa tumekosana. Nilipompigia simu aliniambia aligundua hanipendi, eti nilimuoa kimakosa. Ninampenda sana na itakuwa vigumu kwangu kuanza kutafuta mwingine. Nishauri.

Kupitia SMS

Mtu akiamua kujiondoa katika uhusiano ama ndoa anaweza kutumia mbinu yoyote ile tu, si lazima akwambie ukweli. Madai ya mwanamke huyo eti ulimuoa kimakosa hayana msingi. Ni lazima kuna sababu nyingine iliyomfanya akuache na hataki kukwambia. Ukweli ni kwamba amekata kauli kuwa hataki ndoa kati yenu na huwezi kumlazimisha hata kama unampenda. Itabidi tu ujitose uwanjani utafute mwingine.

 

Alinipachika mimba wazazi wakamkataa sasa anataka niwe mke wa pili, nikubali?

Shikamoo shangazi! Kuna mwanamume tuliyekuwa wapenzi lakini tukatenganishwa na wazazi wangu aliponipatia mimba nikiwa shuleni. Nilimaliza masomo mwaka uliopita na amekuwa akinipigia simu akisema kuwa bado ananipenda na nikitaka anaweza kunioa mke wa pili. Bado ninampenda akini sitaki kuolewa mke wa pili. Ninajua ananipenda kwa dhati na labda nikimshawishi anaweza kumuacha aliye naye kisha anioe. Je, nitakuwa nimekosea.

Kupitia SMS

Hatua ya mwanamume huyo kurudi kwako akitaka muwe pamoja tena ni ishara kuwa anakupenda kwa dhati. Labda kama wazazi wako hawangewatenganisha angekuoa wewe. Mbali na mapenzi uliyonayo kwake, kumbuka kuwa huyo sasa ni mume wa mtu. Ombi lake kwamba uwe mke wa pili ni ishara kuwa anamthamini na kumjali mke wake na hataki kumuacha. Tafadhali usimharibie mwenzako. Ninaamini wewe piz hungependa kufanyiwa jambo kama hilo. Kama huko tayari kuwa mke wa pili mwambie hivyo na utafute mwingine.