Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Meidi, baba watoto wanatupiana macho kivingine

March 14th, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Huu ni mwaka wa pili tangu niolewe na tumejaliwa mtoto mmoja. Ninashuku kuna kitu kinachoendelea kati ya mume wangu na mjakazi wa nyumbani kwetu. Nimeona dalili kupitia jinsi wanavyotupiana macho na pia mume wangu amekuwa akisifia sana kazi yake hasa mapishi na usafi nyumbani. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ingawa umeona dalili hizo, hazitoshi kuthibitisha kuwa wawili hao wanapendana. Sijui jinsi unavyoweza kujua iwapo watu wanapendana kwa jinsi wanavyotupiana macho. Si hatia pia kwa mume mwenye nyumba kusifia kazi nzuri ya mjakazi wake. Jipe muda ufanye uchunguzi wa kina ili upate ukweli.

 

Nimpendae ni kama ameingia woga wa kuoa; amegura mipango ya harusi

Shangazi pokea salamu zangu. Nina umri wa miaka 28 na kuna mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitatu. Tulikuwa tumeanza mipango ya ndoa lakini amesimama ghafla kwa kushuku kuwa nina mwingine. Ukweli ni kuwa mimi sina mwingine na sielewi ni kwa nini ameanza kunishuku. Nishauri.

Kupitia SMS

Mpenzi wako hana sababu ya kukushuku kwa sababu hana ushahidi wowote. Ninaamini hatua hiyo imetokana na mapenzi yake kwako, hasa wakati huu ambapo ameamua kukuchukua uwe mke wake. Mpe muda afanye uchunguzi wake. Hatimaye atajua ukweli na kurudisha imani kwako.

 

Je, nilikosea kuolewa naye wiki chache tu baada ya kukutana?

Kwako shangazi. Nimeolewa na nilipata mtoto wangu wa kwanza hivi majuzi. Mume wangu alinioa muda mfupi tu baada ya kujuana na sikuwa na wakati mzuri wa kumfahamu vyema. Sasa nimegundua kuwa hapendelei kutangamana na watu. Tangu nijifungue, tumekuwa tukitembelewa na wageni na nimeona akiwa na shida ya kujumuika nao. Kwa upande mwingine, mimi ni mtu wa watu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Watu wameumbwa kwa namna tofauti na kuna baadhi ya maumbile ambayo si rahisi kubadilisha. Kuna mambo fulani ambayo mume ama mke anakubali kuyavumilia ili kudumisha ndoa. Ni bahati nzuri kwamba wewe unapenda kujumuika na watu. Unaweza kutumia hali yako kumbadilisha mumeo kupitia mazoea ya kujumuika na watu wengine mara kwa mara.

 

Nimemzimikia sana demu jirani ila yeye anataka kuniweka ‘kwa friends zone’ nami nataka penzi si urafiki

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 28 na kuna mwanamke ninayempenda. Amekuwa jirani yangu mtaani kwa mwaka mmoja na tumekuwa tukionana kwa karibu kila siku. Juzi nilimuuliza iwapo ananipenda akaniambia tunaweza kuwa marafiki. Kwa muda ambao tumejuana, nimeona dalili kuwa yeye pia ana hisia kwangu na sikutarajia kwamba atakataa ombi langu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Subira kubwa inahitajika katika kujenga uhusiano wa kimapenzi. Hali kwamba mwanamke huyo amekubali muwe marafiki ni dalili nzuri na hatua kubwa kwa mpango wako, kwa sababu mapenzi huanza kwa urafiki. Hata kama ana hisia kwako, hawezi kukubali mara moja kwani hajakufahamu vyema. Kubali urafiki kwa sasa kisha utautumia kufikia lengo lako.

 

Nimekuwa nikitupia akina dada ndoana bila mafanikio, wote wamenikataa na sijui kasoro yangu ni gani

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 39 na bado sijaoa wala sina mpenzi. Natamani sana kuwa na mwenzangu maishani lakini wanawake wote ambao nimewapenda wamenikataa. Sijui nina kasoro gani; nahofia nitaishi bila mke. Naomba ushauri wako tafadhali.

Kupitia SMS

Mawazo uliyo nayo kuhusu wanawake si ya kweli na unafaa kuyaondoa akilini mwako kama unataka kupata mke. Kuna wanawake wa kutosha duniani na kila mwanamume ana nafasi ya kupata wake. Hali kwamba umewapenda wanawake kadhaa wakakukataa haimaanishi hakuna mwanamke anayeweza kukupenda. Usikate tamaa, endelea kutafuta na hatimaye utampata.