Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mke ananidharau kwani ana pesa nyingi kunishinda

April 4th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nimeoa mke ambaye ameajiriwa na analipwa mshahara mkubwa. Ninahisi kwamba hali yake hiyo ndiyo inamfanya anidharau kwani haniheshimu hata kidogo na amekuwa akifanya mambo mengi bila kuniambia. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Hali ya mke kuingiwa na kiburi na kumkosea heshima mumewe kwa sababu ana pesa kumshinda ni dalili mbaya katika ndoa. Ni muhimu uchukulie jambo hilo kwa uzito na mlizungumze ili ujue mapema hatua ya kuchukua. Ndoa isiyo na heshima haiwezi kudumu.

 

Nimemchukia bila sababu maalumu 

Shangazi natumai wewe ni mzima. Nina umri wa miaka 20 na nimekuwa kwa uhusiano na kijana fulani kwa miaka miwili, lakini moyo wangu umeanza kumchukia tu bila sababu. Kuna mwingine anayenipenda lakini bado sijaamua kumpa moyo wangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Haina haja kuendelea na uhusiano huo kama humpendi mwenzako. Hata hivyo, ni muhimu pia uwe na msimamo katika uamuzi utakaotoa ili usiwe mtindo wako ni kuruka huku na kule. Hakikisha kuwa ukipenda unapenda kwa dhati la sivyo hutawahi kutulia.

 

Nilimuacha lakini ataka nimrudie

Kwako shangazi. Ni miezi miwili tangu nilipomuacha mwanamume mpenzi wangu kwa sababu ya mienendo yake ambayo haikunifurahisha. Sasa ameanza kunitafuta akisema amejirekebisha. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Uamuzi wako utategemea uzito wa mambo yaliyokufanya umuache na jinsi unavyompenda. Kama amekwambia mwenyewe kuwa amebadilika, mpe nafasi uone kama anavyosema ni kweli.

 

Ana vidosho wengi

Shikamoo shangazi! Kuna kijana anayetaka tuwe na uhusiano lakini huwa namuona na wasichana wengi na ninaamini ni lazima ana uhusiano na mmoja au baadhi yao. Naomba ushauri wako.

Sijui kama umechunguza ukajua kuwa ana uhusiano na wasichana hao kwa sababu huenda si wapenzi bali ni marafiki tu. Kama wewe pia unampenda, ni muhimu ujue ukweli usije ukamkataa ilhali hana mwingine.

 

Nampenda lakini shida ana mtoto

Kwako shangazi. Nimependana na mrembo fulani na niko tayari kumuoa. Shida pekee ni kuwa ana mtoto.

Kupitia SMS

Kama hutaki kuoa mwanamke aliye na mtoto basi unapoteza wakati wako kwake kwa sababu huwezi kumtenganisha na mtoto wake. Mambo ni mawili: Umkubali na mwanawe ama umsahau utafute asiye na mtoto.

 

Naweza kumuoa na mtoto si wangu?

Shikamoo shangazi! Nina uhusiano na msichana aliye na mtoto na nampenda sana. Je, ninaweza kumuoa ilhali mtoto si wangu?

Kupitia SMS

Mtoto si hoja bora tu uwe tayari kumkubali na kumlea kama mtoto wako. Ukweli ni kuwa huwezi kumtenganisha mpenzi wako na mtoto wake. Kama kweli unampenda na unataka awe mke wako, itabidi pia umkubali mwanawe.

 

Ana mke nami pia nina mume

Kwako shangazi. Kuna mwanamume anayenipenda nami pia nampenda ingawa bado hatujaanza uhusiano. Tatizo ni kuwa ana mke na mimi pia nimeolewa. Naomba ushauri wako.

Hata kama mnapendana, mnajua kuwa mkianza uhusiano utakuwa haramu. Na kama hujui, mpango wa kando kwa watu walio katika ndoa huwa ndio mwanzo wa mwisho wa ndoa zao. Umeolewa, kwa hivyo acha tamaa na utulie katika ndoa yako.

 

Adai kunipenda kuliko mume wake

Kwako shangazi. Nilioa mwaka uliopita na tumejaliwa mtoto mmoja. Kuna mke wa rafiki yangu ambaye pia ni jirani mtaani ambaye amekuwa akiniandama akitaka uhusiano. Ananimbia eti ananipenda kuliko mumewe. Nifanye nini?

Huyo ni mwanamke aliyepotoka kimaadili na usikubali akupotoshe. Kinachomfanya atake kwenda nje ya ndoa ndiye anakijua. Kwa hivyo, jiepushe naye asije akavuruga ndoa yako changa.