Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mke hanipi tena joto, asema ndoa imemchosha!

July 30th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nimeoa kwa miaka mitatu na tumejaliwa watoto wawili. Kwa miezi kadhaa sasa mke wangu amekuwa akilala katika chumba cha wageni. Nimemuuliza sababu akaniambia ametosheka na ndoa. Matamshi yake hayo yamenishangaza kwani nilimuoa awe mwenzangu wa maisha wala si wa muda tu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Bila shaka ulikuwa unatafuta ndoa ya maisha kwa hivyo mwanamke huyo hana manufaa kwako tena kama amesema hataki ndoa. Huwezi kuendelea kuishi naye ukijua kuwa si mke wako. Shauriana naye ili muachane utafute mwingine.

 

Mume amezidi kupekua sketi nje

Kwako shangazi. Nimeolewa lakini maisha yangu ya ndoa yamegeuka balaa. Sababu ni kwamba mume ana wanawake wengi wa pembeni hata katika mtaa tunamoishi. Nahofia kwamba asiporekebisha tabia yake hiyo ataniletea virusi. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Naelewa masaibu unayopitia iwapo kweli hiyo ndiyo tabia halisi ya mume wako. Ushauri wangu ni kuwa uketi chini naye umwambie wazi kuwa hutaendelea kuvumilia tabia yake hiyo. Asipojirekebisha ni heri muachane aendelee na maisha anayopenda nawe uache kuishi kwa hofu.

 

Sijui anipenda kweli

Kwako shangazi. Kuna msichana ambaye tumejuana majuzi tu na ninampenda kwa dhati. Yeye pia anasema ananipenda lakini nikimwangalia naona ni kama hana hisia kwangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Huwezi kupima hisia za mtu kwako kwa kutumia macho wala hakuna kifaa cha kupimia hisia. Kama amekwambia mwenyewe kuwa anakupenda huna sababu ya kumshuku. Utaweza tu kujua ukweli kupitia vitendo vyake jinsi uhusiano wenu unavyoendelea kukomaa.

 

Alinikimbia na sasa ataka turudiane

Hujambo shangazi? Nilikuwa na mpenzi lakini akaniacha na kushikana na rafiki yangu. Muda si mrefu ameanza kunipigia simu akiniomba turudiane. Sijapata mwingine na nilikuwa nampenda sana. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Unasema kuwa mpenzi wako huyo alikuacha tu bila sababu na kushikana na rafiki yako. Kwangu mimi huo ni usaliti mkubwa wa kimapenzi na sielewi ni kwa nini unataka kumpokea tena kwa mikono miwili hata kama unampenda. Kuna hatari ya mwanamke huyo kukutumia vibaya akijua kuwa amekupumbaza kwa penzi lake.

 

Hanionyeshi mahaba nitajuwaje penzi lake ni la dhati?

Shangazi, nimependana na mwanamke jirani yangu mtaani. Nampenda sana naye pia ameungama kwa moyo wake wote. Ajabu ni kwamba amekataa kabisa kunionyesha kwa vitendo mahaba aliyonayo kwangu. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Masuala ya mahaba ni kuelewana wala hayalazimishwi. Mwenzako ameungama mwenyewe kuwa anakupenda na huna shaka kuhusu hilo. Kwa sababu hiyo itakuwa vyema kwako umuelewe akikwambia hayuko tayari kwa jambo hili au lile iwapo unathamini uhusiano wenu na unataka kuudumisha. Kuwa na imani kwamba siku atakayokuwa tayari atakutimizia ombi lako.

 

Aliniona na haja ni kukagua chungu tu!

Shikamoo shangazi! Kuna mwanamume tuliyejuana kupitia kwa simu na amekuwa akinipigia mara kwa mara kuniambia kuwa ananipenda na kuomba tukutane. Hatimaye nilikubali ombi lake na juzi tukakutana. Ajabu ni kuwa siku hiyo hiyo alitaka kuonja asali. Nina hisia kwake lakini siwezi kumtimizia ombi hilo kwani sijamfahamu vyema. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hata kama mwanamume huyo anakupenda, nahisi kwamba ameweka mbele tamaa badala ya uhusiano wa dhati. Shikilia msimamo wako huo hadi utakapojua kwa hakika nia yake kwako.

 

Asema hayuko tayari tuoane, nifanyeje?

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 35 na nahisi kuwa wakati wangu wa kuoa umewadia na pia niko tayari. Tatizo ni kwamba mwanamke tunaependana anasema hataki kuolewa sasa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kama mwenzako amekwambia hayuko tayari kuolewa haitakuwa vyema kumsukuma afanye jambo ambalo hataki. Utaamua iwapo utasubiri hadi atakapokuwa tayari ama utatafuta anayetaka kuolewa sasa.