Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mke niliyeoa majuzi hataki nijue kwao, ametoweka

August 16th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI pokea salamu zangu. Ni mwaka mmoja sasa tangu nilipooa. Ajabu ni kuwa mke wangu huwa hataki jamaa zake wajue kuwa ameolewa. Amekuwa akiwadanganya yuko kazini na pesa anazowatumia huwa zinatoka kwangu. Juzi alisafiri kwao na amekataa kurudi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ukweli ni kuwa huyo unayemuita mke wako hakupendi bali alikuchezea akili tu ili kwanza avune pesa kutoka kwako. Ndiyo maana hakutaka ujulikane kwao wala jamaa zake wajue kuwa ameolewa kwa sababu hiyo haijawa nia yake kwako. Kama ameenda kwao na amekatalia huko, usimngojee kwani hatarudi. Ameshapata alichokuwa akitaka kutoka kwako.

 

Sijawahi kufurahia mchezo hata mara moja

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 28 na nimekutana na wanaume kadhaa tangu nijue masuala ya mahaba. Ajabu ni kuwa sijawahi kufurahia utamu wa burudani hata siku moja. Je, nina kasoro?

Kupitia SMS

Kusema kweli sijawahi kukutana na mtu mwingine aliye katika hali kama hiyo yako. Wengi wao hasa hulalamika kwamba hawatosheki. Inawezekana kwamba unaokutana nao hawana ujuzi unaohitajika kusisimua hisia zinazoleta utamu wa shughuli hiyo. Kuwa na subira, siku moja utakutana na pwaguzi akushughulikie ipasavyo.

 

Mama yake hataki anioe eti kwa sababu ana miaka 22 pekee

Shikamoo shangazi! Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 20 na mpenzi wangu ana umri wa miaka 22. Yeye yuko tayari kunioa lakini mama yake anapinga akisema eti bado ni mdogo hajafikisha umri wa kuoa. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mimi pia nahisi ni mapema kwa mwanamume huyo kuoa kwani bado hajakomaa kiakili kiasi cha kuweza kushughulikia masuala ya ndoa. Labda pia hana uwezo wa kukimu familia na ndiyo maana mama yake anapinga. Mpe muda kwanza akomae.

 

Je, nimuoe hata japo amenizidi umri na mwaka mmoja

Shangazi nina mpenzi lakini kuna jambo linalonitia wasiwasi. Amenizidi umri kwa mwaka mmoja na ninashangaa iwapo ninaweza kuoa mwanamke mwenye umri mkubwa kunishinda. Nishauri.

Kupitia SMS

Nimesema mara nyingi katika safu hii kuwa umri si hoja sana wawili wanapopendana. Isitoshe, tofauti ya mwaka mmoja ni ndogo sana na hilo si jambo linalofaa kukutia wasiwasi. Ondoa hofu na ushughulikie uhusiano na ndoa yenu.

 

Niliyetamani halafu akaolewa ameachana na mume, nimtwae?

Vipi shangazi. Kuna msichana niliyempenda lakini akanyakuliwa na rafiki yangu kabla sijamdokezea hisia zangu kwake. Sasa wameachana na bado nampenda. Ninajua pia nikimwambia nampenda atanikubali. Nishauri.

Kupitia SMS

Sijui unahitaji ushauri gani ilhali kila jambo liko wazi kutokana na maelezo yako. Unasema kuwa wameachana sasa hana mpenzi, bado unampenda na una hakika ukimwambia atakubali. Unangoja nini. Ukizubaazubaa atanyakuliwa tena. Shauri yako.

 

Alinipenda nikiwa mbali, sasa amegeuka

Hujambo shangazi. Nilikuwa na mpenzi na nikaenda kazi mbali. Nikiwa huko alikuwa akinipigia simu kuniambia jinsi anavyonipenda na hata kuniahidi kuwa tutaoana. Nilirudi majuzi kwa likizo na nilipompigia simu akakata na kunitumia SMS akisema hana wakati wa kuongea nami. Baadaye nilimpigia simu akazima. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Tabia ya mpenzi wako ni ishara kwamba hataki tena uhusiano kati yenu. Kuna uwezekano mkubwa kwamba alishikana na mwanamume mwingine ulipokuwa mbali naye. Mapenzi hayalazimishwi kwa hivyo itabidi ukubali uamuzi wake.

 

Anapenda pesa tu hata asali hanipi

Shikamoo shangazi! Mimi nina mpenzi lakini nimegundua kuwa haja yake kwangu ni pesa tu hakuna mapenzi. Nikimuomba asali anaruka. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kama huna habari, si lazima mwanamke akulambishe asali ili kuthibitisha penzi lake kwako. Tendo hilo hasa linafaa kusubiri hadi watu wanapooana. Hata kama unampa pesa mpenzi wako, unafanya hivyo kwa hiari wala si kumhonga ili akulambishe asali. Ukihisi kwamba anakutumia vibaya acha kumpa pesa ama uachane naye.