Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mke wa zamani ameanza kumwandama tena

April 23rd, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nimekuwa katika uhusiano na mwanamume aliyekuwa na mke lakini wakaachana. Wakati ambapo penzi letu limefikia kileleni, aliyekuwa mkewe ameanza kumsumbua akitaka warudiane. Mpenzi wangu ameniuliza iwapo ningependa kuolewa mke wa pili. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Ninaelewa kuwa moyo wako tayari umezama kwa mwanamume huyo na unahisi vigumu kutafuta mwingine. Kama umetosheka moyoni kuwa ungependa kuolewa mke wa pili na unaamini utakuwa na furaha katika ndoa hiyo basi kubali mpango huo.

 

Nikiwa peke yangu hisia hunizidia lakini niwapo naye siwezi

Kwako shangazi. Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 26 na nina mpenzi ingawa uhusiano wetu umekuwa baridi kutokana na hali yangu. Nina shida ambayo inahitaji msaada wako. Ninapokuwa peke yangu huwa ninapandwa na hisia nzito za kushiriki mahaba, lakini ukifika wakati wa mwenzangu kuhitaji huduma hiyo ninashindwa kabisa. Je, shida yangu hiyo ina dawa?

Kupitia SMS

Ingawa mimi si mtaalamu wa masuala ya afya ya uzazi, ninahisi kuwa shida yako ni ya kimawazo wala si ya kimatibabu. Inawezekana kwamba huna mazoea ya kitendo hicho ama huamini kuwa una uwezo wa kukitekeleza kikamilifu. Hayo ni maoni yangu tu. Jaribu umuone mtaalamu wa masuala ya uzazi uone kama atakusaidia.

 

Ninamshuku kwani anaandamana sana na wanaume

Shangazi nina mpenzi lakini nina wasiwasi kuhusu uhusiano wetu. Sababu ni kuwa anajuana na wanaume wengi sana ambao anadai ni marafiki tu lakini mimi siamini na nafikiria kumuacha. Nishauri.

Kupitia SMS

Iwapo hujawahi kumpata na mwanamume mwingine katika hali ya kuonyesha kuwa wana uhusiano, huna sababu ya maana ya kumshuku. Isitoshe, yeye mwenyewe amekwambia kuwa hao ni marafiki tu na sijui ni kwa nini hutaki kumwamini.

 

Huwa ninajishibisha maana mara nyingi mpenzi huwa mbali

Vipi shangazi? Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 22. Nina mpenzi lakini mara nyingi amekuwa akienda kazi mbali kwa muda mrefu. Wakati kama huo huwa ninalazimika kujishughulikia angalau kupunguza joto. Je, kitendo hicho kina madhara?

Kupitia SMS

Ingawa hujalelezea unatumia mbinu gani, hakuna madhara yoyote yanayoweza kutokana na shughuli hiyo bora tu isiwe inayoweza kukujeruhi au isiyo safi, ambayo inaweza kukuletea maambukizi katika sehemu husika.

 

Hajawahi kuniambia kama ananipenda

Shangazi kuna mwanamke ambaye nimempenda kwa moyo wangu wote lakini hataki kuniambia iwapo yeye pia ananipenda au la. Kila nikimuuliza huniambia ningoje tu, hatimaye atanijibu. Huu sasa ni mwaka wa pili. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Miaka miwili ni muda mrefu wa kusubiri jibu kama hilo. Inawezekana kwamba mwanamke huyo hataki uhusiano kati yenu na anahisi vigumu kukwambia. Utaamua iwapo utaendelea kungoja ama utaachana naye utafute mwingine.

 

Mpenzi wa kakangu anataka nirambe asali ya kwake kisiri

Vipi shangazi? Kuna msichana mpenzi wa kaka yangu ambaye ameniambia anataka tuwe na uhusiano wa kimapenzi kisiri. Sijui nitafanya nini.

Kupitia SMS

Huyo msichana ni hatari na usipochunga atakufanya ukosane na kaka yako. Kataa kabisa mambo yake na akisisitiza umwambie utamshtaki kwa kaka yako.

 

Anataka mali ingawa tumemaliza mwezi tu

Shikamoo shangazi! Nimekuwa katika uhusiano kwa mwezi mmoja sasa na tayari mwenzangu anasema nimemuachia njaa sana. Shida ni kuwa mimi siko tayari kwa jambo analotaka. Nishauri.

Kupitia SMS

Uhusiano si kama ndoa kwa hivyo hakuna kati ya wawili aliye na haki ya kudai chochote kutoka kwa mwenzake. Mambo ambayo kila mmoja anamfanyia yanatokana na hisani tu. Kama huko tayari kumuondolea hiyo baridi mwambie hivyo.