Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mke wangu anipenda kweli ila ana wivu kupita kiasi

August 15th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HABARI zako shangazi? Nimeoa na tumejaliwa mtoto mmoja. Mke wangu ananipenda sana lakini mapenzi yake hayo pia yamekuwa balaa kwangu kwani yanaandamana na wivu. Nikichelewa kidogo kufika nyumbani hawezi kutulia, hunitumia SMS akitaka kujua niko wapi na nitafika nyumbani saa ngapi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Palipo na mapenzi ya dhati hapakosi wivu. Hata hivyo, wivu huo ukizidi unaweza kugeuka na kuwa sumu katika ndoa. Usimlaumu mke wako kwa sababu wivu wake huo unatokana na mapenzi yake kwako. Iwapo mambo hayo ndiyo anayohitaji kuondoa wasiwasi wake na kutuliza moyo wake, ni vyema umuelewe. Hasa, usiwe ukisubiri hadi akupigie simu. Badala yake, ukijua utachelewa ni heri uwe ukimpigia simu mapema na kumwelezea.

 

Mke alitoroka baada ya kumfumania na dume lingine

Nina umri wa miaka 35. Nilikuwa nimeoa lakini wakati fulani nikagundua kuwa mke wangu alikuwa akitembea na wanaume wengine. Alipojua nimegundua alitoroka nyumbani na kuniacha na watoto wetu wawili. Huu sasa ni mwaka wa pili sijui yuko wapi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Mke wako alitoroka nyumbani kwa sababu anajua ni makosa makubwa kuwa na mahusiano nje ya ndoa na labda alihofia ungemuadhibu na kumfukuza nyumbani. Miaka miwili ni muda mrefu sana na sidhani ana mpango wa kurudi iwapo bado unamtarajia. Ushauri wangu ni kwamba umuondoe katika mawazo na mipango ya maisha yako.

 

Mwalimu wangu ananinyemelea, masomoni pia sijiwezi

Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili. Mwalimu wangu amekuwa akinitaka kimapenzi kwa muda mrefu licha ya kukataa ombi lake hilo. Tabia yake hiyo inanichukiza na pia inanifanya nishindwe kumakinika katika masomo yangu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni makosa na haramu kubwa kwa mwalimu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanafunzi wake. Hasa, ni kinyume cha maadili ya taaluma ya elimu. Ushauri wangu ni kwamba uwapashe habari hizo wazazi wako, nao wazipeleke kwa mwalimu mkuu wa shule ili mwalimu huyo achukuliwe hatua za kinidhamu na kukomeshwa.

 

Ataka nitafute mume anioe sababu hawezi kukimu mahitaji ya mtoto wetu

Nina umri wa miaka 21 naye mpenzi wangu ana umri wa miaka 20. Tumezaa mtoto pamoja ingawa bado hatujaoana. Mpenzi wangu hana kazi na sasa ameniambia ataniacha kwa sababu hana uwezo wa kunisadia kulea mtoto. Ananiambia nitafute mwanamume mwingine.

Kupitia SMS

Umejiingiza mwenyewe katika hali hiyo wala hukulazimishwa. Nimeonya mara nyingi hapa kwamba si jambo la busara kwa mwanamke kupata mtoto katika uhusiano wa kimapenzi. Aliyeungama mapenzi yake kwako sasa anakwambia utafute mwingine akusaidie kubeba mzigo aliokupa. Kwa jinsi hiyo, umejifunza na umefunza wengine pia.

 

Ninampenda sana lakini hachukui simu

Kuna mwanamke ambaye ninampenda kwa dhati na nimemwambia hivyo. Lakini ananiudhi sana kwa kunipuuza kwani nikimpigia simu ama kumtumia SMS hajibu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Kwa kutojibu simu na SMS zako, mwanamke huyo tayari amekujibu. Amekuonyesha kwamba hana haja nawe kwa hivyo unapoteza wakati wako bure. Achana naye utafute mwingine kwani huwezi kumlazimisha akupende.

 

Nimesikia mpenzi ana wanawake wa kando, sili silali, nisaidie

Nina umri wa miaka 22 na nimependana na mwanamume wa miaka 29. Nimepata fununu kwamba ana mke na pia anapenda sana wanawake na habari hizo zimenipa tumbo joto. Nimemuuliza kuhusu mambo hayo na amekana. Nifanyaje?

Kupitia SMS

Habari hizo zinaweza kuwa za kweli ama za uongo. Huwezi kufanya uamuzi kutokana na habari ambazo hujathibitisha. Ningekushauri ufanye uchunguzi wako mwenyewe ili ujue ukweli wake ndipo upate mwelekeo kuhusu uhusiano wenu.