Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mke wangu mrembo ajabu lakini bado natamani nje

June 26th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Mimi nimeoa lakini nina tatizo kubwa. Mke wangu ni mrembo sana na ninajua kwa hakika kuwa wanaume wengi wanaomuona humtamani yeye ama kutamani kuwa na kama yeye. Ajabu ni kwamba nikiwaona wanawake wengine bado ninawatamani. Ni kwa nini?

Kupitia SMS

Tamaa ni hali ya kawaida, sio tu kwa binadamu bali pia kwa wanyama. Hata hivyo, binadamu ameumbwa tofauti na mnyama, akapewa uwezo wa kujizuia kuongozwa na tamaa. Umeungama mwenyewe kuwa tayari umempata anayekufaa kwa hivyo hisia zako kwa wengine ni tamaa tu. Ni juu yako kudhibiti hisia hizo na kuweka nia yako kwa mwanamke uliyechagua kuishi naye kama mke wako.

 

Sitaki mke arudi, amenitesa tosha

Shangazi nina tatizo kuhusu ndoa yangu na nahitaji ushauri wako wa kitaalamu. Nilikuwa nimeoa kwa miaka mitatu lakini mwaka uliopita mke wangu aliniacha akaenda na mtoto wetu mmoja. Kabla hajaondoka alikuwa ameanza kuninyima haki yangu ya ndoa. Sasa ameanza kunipigia simu akitaka kurudi lakini sitaki arudi kwangu kisha aendelee kunitesa. Nishauri.

Kupitia SMS

Inawezekana kuna mwanamume aliyeingilia ndoa yenu na kumhadaa mke wako akuache ili amuoe. Huenda hatua yake ya kukunyima haki ya ndoa ilikuwa mbinu ya kukuchokoza ili umfukuze na ulipokosa kumtimua akaamua kuondoka mwenyewe. Lakini inaonekana mambo hayakwenda alivyodhania na ndiyo maana ameamua mwenyewe kurudi. Iwapo bado unamtaka katika maisha yako, una nafasi nzuri ya kumpa masharti ya kurudi kwako na mojawapo ya masharti hayo linafaa kuwa awe tayari kukutimizia haki yako ya ndoa.

 

Baba mtoto hataki kugharimia malezi

Hujambo shangazi? Nilipendana na kijana fulani mwaka uliopita baada ya kumaliza shule ya upili. Muda si mrefu alinishawishi tukashiriki mahaba na papo hapo nikapata mimba. Sasa nimejifungua lakini amesusia wajibu wa kugharimia malezi ya mtoto. Hajanitembelea wala kunipigia simu kunijulia hali. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Siku hizi ni wanaume wachache sana wanaowajibika katika kulea watoto waliozaa nje ya ndoa. Ni kwa sababu hiyo ambapo wanawake wanafaa kuwa waangalifu kwa kuepuka mimba nje ya ndoa. Kama baba ya mtoto amesusia wajibu wa kulea, itabidi ubebe mwenyewe mzigo huo.

 

Mkewe wa zamani anitishia maisha

Salamu nyingi kwako shangazi. Nina uhusiano na mwanamume aliyekosana na mke wake na akaolewa na mtu mwingine. Ameamua kunioa na mke wake ameanza kunitumia jumbe za kiajabu baada ya kupata habari hizo. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini mwanamke huyo anaingilia uhusiano wenu kama tayari ameolewa na mwanamume mwingine. Nafikiri bado ana kisasi na huyo aliyekuwa mume wake na anataka kumharibia tu. Usihangaishe moyo wako kumhusu. Akijaribu kukutishia maisha mchukulie hatua za kisheria.

 

Wazazi wataka niharibu mimba

Hujambo shangazi? Nina umri wa miaka 19 na ninapendana na kijana mwenye umri wa miaka 21. Nimepata mimba na yuko tayari kunioa. Amewafahamisha wazazi wake lakini wamepinga vikali mpango huo wakisema hajatimiza umri wa kuoa. Badala yake wanataka niharibu mimba. Tunapendana sana na sitaki kuharibu mimba. Nishauri.

Kupitia SMS

Usikubali kuharibu mimba hiyo kwani ni hatari na pia ni kinyume na maadili. Kama kweli mpenzi wako anakupenda, ninaamini yeye pia hangependa mimba hiyo iharibiwe. Hata kama hayuko tayari kukuoa kwa sasa, ni vyema msubiri ujifungue na muendelee kulea mtoto hadi atakapokuwa tayari kukuoa.