Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi ana mimba ila hataki kuwa mke wangu

August 21st, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

MAMBO shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa mwaka mmoja sasa na sasa ana mimba yangu. Niko tayari kumuoa lakini ameniambia wazi kuwa hawezi kuwa mke wangu. Kuna mwanamume ambaye amekuwa akimpigia simu kila mara na ninashuku kuwa mawazo yake hasa yako kwake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa mapenzi ya dhati yanastahili kuzaa ndoa. Kama mpenzi wako amekwambia wazi kuwa hawezi kuwa mke wako licha ya kwamba ana miba yako, uhusiano wenu huo sasa hauna faida kwako wala kwake. Huenda kweli ameamua kuolewa na huyo mwanamume anayempigia simu. Ni heri muachane mapema kila mmoja wenu ajitafutie maisha kwingine.

 

Tunapendana kufa kuzikana lakini wazazi wasema ni wa kabila tofauti

Vipi shangazi. Mimi nina mpenzi tunayependana kufa kuzikana na ndiye chaguo langu maishani. Nimemjulisha kwa wazazi wangu lakini wamemkataa kwa sababu anatoka kabila tofauti na langu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Kuna mambo ya kijamii ambayo yamepitwa na wakati. Mahusiano ya enzi tunazoishi hayajui kabila wala rangi. Kama weusi na weupe wanaoana, watu wa makabila tofauti watakosa? Ndoa ni suala la mtu binafsi na wazazi au jamaa zako hawafai kukuamulia, Waambie wazi kuwa moyo wako umenata kwa huyo na hauwezi kubanduka. Ukishikilia msimamo huo hatimaye watakuelewa na kukubali uamuzi wako.

 

Anadai ni rafiki tu mimi nahisi ni zaidi ya urafiki, nifanyeje?

Vipi shangazi? Tafadhali naomba unisaidie kwani nimechanganyikiwa. Nimekuwa katika uhusiano kwa miaka miwili sasa. Wiki moja iliyopita nilimpata mpenzi wangu mahali akiwa na mwanamke mwingine na nilipomuuliza akaniambia ni marafiki tu. Nahisi kuwa mpenzi wangu ananichezea, kuna zaidi ya urafiki kati yake na mwanamke huyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Hujaelezea uliwapata wakifanya nini ingawa kulingana na maelezo yako ninaelewa kuwa walikuwa wakizungumza tu. Ni muhimu ufahamu kuwa ni haki ya mtu kuwa na marafiki wa kiume na wa kike pia hata kama ana mpenzi. Iwapo huna ushahidi wowote kwamba wawili hao ni wapenzi, amini anavyokwambia mpenzi wako kwa sasa. Tayari unamshuku kwa hivyo kama kuna zaidi ya urafiki, kuwa na subira na muda si mrefu utamfumania.

 

Mbona anidanganye kuwa ana mke?

Habari yako shangazi? Kuna mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa mwaka mmoja sasa. Amekuwa akiniambia kuwa ana mke lakini nimekuwa nikishuku kuwa ananihadaa. Juzi nilienda kwake ghafla na sikuona dalili zozote za mwanamke. Ni kwa nini aliamua kunidanganya?

Kupitia SMS

Iwapo umethibitisha kuwa mwanamume huyo hana mke ilhali amekuwa akikwambia ameoa, sababu yake ya kukuhadaa inaweza kuwa moja tu. Anakuhitaji katika maisha yake kwa sasa lakini ameamua moyoni kwamba huwezi kuwa mke wake. Ameridhika na uhusiano wenu lakini hakutaka kabisa uingiwe na mawazo kwamba mnaweza kuishi pamoja kama mume na mke. Sasa umegundua njama yake, chukua hatua inayofaa.

 

Tumepanga kuoana lakini anashuku ninagawa chungu kwa mwingine!

Shangazi pokea salamu zangu. Nina umri wa miaka 28 na kuna mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka mitatu. Tumepanga kuoana lakini anashuku kuwa nimeshiriki mahaba na mwanamume mwingine. Mimi sina mwingine ila yeye tu na sielewi ni kwa nini ananishuku. Nishauri.

Kupitia SMS

Iwapo kweli huna uhusiano wa pembeni mume wako hana sababu ya kukushuku kwa sababu hana ushahidi wowote. Labda ni wivu tu kutokana na mapenzi yake kwako. Endelea kumuonyesha mapenzi ya dhati pamoja na kumhakikishia kuwa huna mwingine. Hatimaye atajua ukweli na kurudisha imani yake kwako.