Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi anasema amezaa baada ya miezi 5 ya tendo

September 6th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHANGAZI ni matumaini yangu kwamba wewe ni mzima. Nina mpenzi na tulikutana mara ya mwisho mapema mwaka jana nilipomtembelea katika mji anakofanya kazi. Wakati huo aliniambia alikuwa na mimba yangu na baada ya miezi mitano akaniambia amepata mtoto. Sasa amekuwa akiniambia nimtumie pesa za kutunza mtoto lakini hataki kuniletea mtoto nimuone na pia hataki nimtembelee aliko. Ninashuku kama kweli alikuwa na mimba na iwapo kweli amejifungua. Nishauri.

Kupitia SMS

Ni ajabu sana kwamba mpenzi wako amejifungua mtoto wako na hataki umuone. Kuna uwezekano mkubwa kwamba hakuwa na mimba, alikuhadaa tu ili apate namna ya kupata pesa kutoka kwako na ndiyo maana hataki umtembelee kwa sababu utajua ukweli. Na kama kweli alikuwa na mimba, labda aliitoa ama iliharibika lakini ameamua kukuchezea akili. Kwa sababu unajua anakoishi, mtembelee bila kumwambia ili ujue ukweli wa jambo hilo.

 

Dume fulani lanifuata sana hadi sipati amani

Vipi shangazi? Nina mwanamume mpenzi wangu ninayempenda sana. Hata hivyo, kuna mwingine ambaye ananiandama akitaka nimuache mpenzi wangu nishikane naye. Mimi simtaki na kamwe siwezi kumpenda. Nishauri.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, ni wazi kuwa umefunga moyo wako kwa mpenzi uliye naye na huna nafasi ya mwingine. Unachofaa kufanya ni kumwambia wazi huyo anayekuandama kwamba huna haja naye na akome kukusumbua.

 

Nikimwangalia naona hana hisia kwangu

Kwako shangazi. Kuna mwanamke ambaye tumejuana majuzi tu na ninampenda kwa dhati. Yeye pia anasema ananipenda lakini nikimwangalia naona ni kama hana hisia kwangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hisia ni hali inayotoka katika moyo wa mtu binafsi na haiwezi kupimwa kwa macho. Kama mwanamke huyo amekwambia mwenyewe kuwa anakupenda, huna sababu ya kumshuku. Utaweza tu kujua ukweli kupitia vitendo vyake mkiendelea na uhusiano wenu.

 

Demu king’ang’anizi ananihatarishia ndoa

Hujambo shangazi? Kuna mwanamke tuliyekuwa wapenzi lakini tukaachana kisha nikaoa mwingine. Tatizo ni kwamba bado anaendelea kunifuata kwa kunipigia simu kila mara na nahofia ataniharibia ndoa yangu. Nimemkanya lakini hataki kusikia. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Ingawa mlikuwa wapenzi, mwanamke huyo anafaa kuelewa kwamba sasa una mke kwa hivyo hana nafasi yoyote katika maisha yako. Kama umemuonya na bado anaendelea kukusumbua, unaweza kumchukulia hatua kisheria.

 

Naambiwa nimezama katika familia maskini

Kwako shangazi. Nina umri wa miaka 22 na nimeolewa. Shida iliyopo ni kwamba wazazi wangu hawana furaha kuhusu ndoa yangu. Wamekuwa wakiniambia eti nimeolewa na mwanamume maskini huku wakinishauri nimuache. Mimi nampenda mume wangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Manufaa ya ndoa yako yanafaa kuwa yako wala si ya wazazi ama jamaa zako wengine. Madai ya wazazi wako eti umeolewa na mwanamume maskini hayana msingi bora tu wewe unampenda alivyo na umetosheka katika maisha yako ya ndoa. Wapo wanawake wengi ambao wameolewa na matajiri lakini wanaishi kwa majonzi. Kwa sababu hiyo, usihangaishe moyo wako kuhusu wanavyohisi ama wanayosema wazazi wako kwani hayakuathiri kwa njia yoyote ile.

 

Haamini ahadi yangu

Habari yako shangazi? Nina umri wa miaka 23 na nina mpenzi ambaye tayari nimemuahidi kuwa nitamuoa. Tunapendana sana lakini tatizo pekee ni kwamba haamini kwamba hatimaye nitamuoa. Nifanye nini ili aniamini?

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini mpenzi wako hakuamini licha ya kwamba umeahidi kuwa utamuoa. Unafaa kumuuliza yeye mwenyewe ni kitu gani kinachomtia shaka. Kama kuna jambo lolote analotaka ufamnyie ili aweze kukuamini, basi mwambie akwambie ili umtimizie, bora tu liwe linawezekana kwako.