Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi ataka kujua iwapo mie ni wake wa kwanza

June 11th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

ZA kwako shangazi? Mimi na mpenzi wangu tumekubaliana kwamba tutashiriki tendo la mapenzi baada ya ndoa. Tumedumisha msimamo huo kwa miaka miwili ambayo tumekuwa wapenzi. Sijui ni kwa nini ghafla ameanza kushuku kuwa nilikuwa na mpenzi au wapenzi wengine kabla yake kwani ameniuliza mara kadhaa iwapo mimi ndiye wake wa kwanza ilhali nilimwambia hivyo siku tuliyokutana. Nifanyeje ili aniamini?

Kupitia SMS

Labda kuna mambo ambayo umemwambia ama kuyaona katika mienendo yako yanayomfanya kuamini kwamba siye wa kwanza. Mpe nafasi akuelezee yake kuhisi anavyohisi ndipo nawe uweze kujieleza na kumuondolea wasiwasi.

 

Nifanye nini ili kumuondolea laazizi shaka kwangu?

NINA mpenzi ambaye ninampenda sana. Nimempa moyo wangu wote na ninaamini atakuwa mume wangu hivi karibuni. Hata hivyo, ninahisi kama haniamini ingawa sina mwingine wala sijawahi kufikiria kuwa naye katika miaka miwili ambayo tumekuwa pamoja. Nifanye nini ili kumuondolea shaka?

Kupitia SMS

Iwapo kweli wewe ni mwaminifu kwake, mpenzi wako hana sababu ya kukushuku. Nijuavyo ni kuwa palipo na mapenzi hapakosi wivu. Hiyo ni ishara kuwa mwanamume huyo anakupenda sana na hangependa mtu au kitu chochote kuvuruga uhusiano wenu. Itakuwa vyema ushauriane naye kuhusu suala hilo ujue hofu yake kisha umhakikishia kuwa ni yeye tu ndiye wako huna mwingine.

 

Hii ajabu! Ataka kunioa ila haniamini

Vipi shangazi? Nina mpenzi wa dhati ambaye tumekuwa na uhusiano kwa miaka mitatu sasa. Tumepanga ndoa yetu miezi miwili ijayo lakini nilishangaa juzi aliponiambia yuko tayari nimuoe ingawa bado haniamini. Nimekuwa mwaminifu kwake kwa muda wote ambao tumekuwa wachumba na sielewi ni kwa nini haniamini. Nampenda sana lakini pia sitaki kuwa na mke asiyeniamini. Nishauri.

Kupitia SMS

Ninaamini nia ya mpenzi wako ya kutoa matamshi hayo ni kupima uaminifu wako kwake kabla hatua hiyo muhimu ya maisha yenu pamoja. Hawezi kukubali mfunge ndoa kama kweli hakuamini. Utagundua kuwa huo ni mzaha tu ukimhakikishia kuwa huna mwingine ila yeye tu.

 

Kidudumtu fulani anavuruga penzi letu

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 24 na nimekuwa katika uhusiano wa kimapenzi kwa karibu mwaka mmoja sasa. Kuna mwanamume mwingine ambaye amekuwa akinitaka lakini mimi sina haja naye na nimemwambia hivyo. Mpenzi wangu amejua na sasa uhusiano wetu umeingia baridi. Kwa mwezi mmoja sasa hatujaonana wala kuzungumza. Sijui anafikiria nini. Nipe ushauri.

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa mwanamke kutongozwa hasa mtu kama wewe ambaye hujaolewa. Kwa sababu hiyo, mpenzi wako hana sababu nzuri ya kukukasirikia kama tayari umemwambia mwanamume huyo ndiye anayekutafuta na huna shughuli naye. Jaribu kumtafuta uzungumze naye ili ujue msimamo wake.

 

Anapokea pesa kutoka kwa mpenzi wa zamani, nashuku hapa ninachezewa!

Ninapendana na mwanamke aliye na mtoto kutokana na uhusiano wa awali. Nimekuwa nikigharimia mahitaji yake na mtoto wake lakini nimeshangaa kugundua kuwa amekuwa pia akipokea pesa kutoka kwa baba ya mtoto wake. Sijamuuliza ni kwa nini lakini ninashuku bado wako pamoja. Nishauri.

Kupitia SMS

Inawezekana mwanamume huyo aliamua kuendelea kugharimia malezi ya mtoto wake licha ya wao kuachana. Inawezekana pia hajui iwapo mama ya mtoto wake amepata mpenzi ambaye anashughulikia mahitaji yao. Kwa kuwa umechukua jukumu hilo sasa, mpango huo unafaa kusimama. Badala ya kunyamaza na kumshuku mpenzi wako, mueleze unavyohisi. Kama anakupenda atakusikia.