Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi hatulii mke wa kwanza kuhepa na watoto wake

August 8th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

KWAKO shangazi. Nimeolewa na mwanamume aliyekuwa ameoa mwanamke mwingine lakini wakaachana. Mke wake alienda na mtoto wao na jambo hilo linamtatiza sana mume wangu kwani anampenda sana mwanawe. Nahisi kwamba hali hiyo inaathiri maisha yetu pamoja. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ukweli ni kuwa damu ni nzito kuliko maji. Ingawa mume wako aliachana na mkewe wa kwanza, mtoto waliyezaa pamoja ni damu yake na hawezi kumsahau kwa haraka. Ushauri wangu ni kuwa umpe muda nawe pia umzalie na hatimaye akili yake itarudi kwako.

 

Ameanza kunishuku, ataka tutumie kinga

Nina uhusiano na mwanamke fulani na tumekuwa tukishiriki mahaba bila kinga kwa sababu tunaaminiana. Sasa ameanza kushuku eti nina uhusiano wa pembeni na anasisitiza tutumie kinga iwapo ninataka tuendelee na uhusiano. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Kinga haitumiwi kuepuka magonjwa tu bali pia mimba. Nyinyi ni wapenzi na sidhani mko tayari kupata watoto kwa hivyo ni muhimu kutumia kinga. Pili, itakuwa vyema uzungumze na mpenzi wako ili ujue ni kwa nini anakushuku kisha utafute namna na kumuondolea shaka.

 

Bosi wangu wa kike ni rafiki wa miaka 2, juzi amenikasirikia nilipomfichulia hisia

Kuna mwanamke bosi wangu katika kampuni ninakofanya kazi ambaye tumekuwa marafiki wakubwa kwa miaka miwili sasa. Sijaoa naye pia hajaolewa. Ni mrembo na nimeishia kumpenda. Juzi nilipiga moyo konde nikamdokezea hisia zangu kwake na akakasirika sana. Sasa nahofia nitamwaga unga.

Kupitia SMS

Mapenzi na urafiki ni mambo mawili tofauti. Urafiki ni uhusiano wa kawaida wa binadamu kutokana na utangamano wao wa kila siku. Lakini mapenzi ni suala la moyoni linaloamuliwa na mtu binafsi. Sasa umejua kuwa mwanamke huyo hataki uhusiano wa kimapenzi kati yenu kwa hivyo tosheka na urafiki. Sidhani atakufuta kazi kwani yeye ni mtu mzima na si hatia kwako kumwelezea hisia ulizo nazo.

 

Mwanamume aliyezaa na mke wangu sasa ananichafua roho

Nilioa mwanamke aliyekuwa ameolewa na mwanamume mwingine. Alikuwa na mtoto waliyezaa pamoja. Sasa mwanamume huyo amekuwa akimpigia simu mara kwa mara na jambo hilo linanichafua roho. Je, hiyo ni haki?

Kupitia SMS

Alipokubali umuoe, mwanamke huyo alionyesha kwamba aliachana na mume wake akakatiza kabisa uhusiano wao na ndiyo maana alirudi kwao na watoto wake. Ni makosa kwake kuendelea kuwasiliana na mume wake wa zamani akiwa kwako. Mwambie wazi kuwa jambo hilo linakuudhi na hutavumilia. Hata kama walizaa pamoja, mtoto huyo sasa ni wako kwani ni wewe unayegharamia malezi yake. Akishindwa kukubaliana na hilo, mwambie arudi kwa mwanamume huyo.

 

Mpenzi wa muda mrefu amenigeuka ghafla bila sababu, amepata mwingine?

Mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa muda mrefu amenigeuka ghafla anataka tuachane. Sielewi ni kwa nini ameamua hivyo kwa sababu sijamkosea. Yawezekana amepata mwingine?

Kupitia SMS

Hatua yake hiyo inaweza kutokana na mambo mawili. Labda hisia zake kwako zimepungua na anahisi kuwa hataki tena kuendelea na uhusiano huo, ama amepata mwingine. Ukweli ni kwamba kama ameamua kujiondoa katika uhusiano huo huwezi kumzuia.

 

Sijapata mwanamke mwenye sifa nitakazo

Mimi ni mwanamume mwenye umri wa miaka 28. Ninataka sana kuoa lakini nina shida moja. Imekuwa vigumu kwangu kuvutiwa na wanawake wengi ninaokutana nao kwani hawatimizi sifa zote za mwanamke ninayetafuta. Naona itanichukua muda kutafuta. Je, kuna njia ya mkato.

Kupitia SMS

Kwanza, kakuna kitu kizuri kinachopatikana kwa njia ya mkato kwa hivyo ni lazima ujitolee na uwe na subira unapotafuta mke mwenye sifa unazotaka. Pili, ukiendelea kutafuta ningependa kukuonya kuwa haitakuwa rahisi kumpata mwenye sifa zote unazotaka kwani hakuna duniani mtu mkamilifu. Kila la heri.