Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi wa dadangu ni jogoo, sijui nimfichulie?

April 19th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

MAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 22 na nina dada yangu mdogo ambaye tunapendana sana. Nimegundua kuwa dada yangu ameshikana na kijana ambaye ana mpenzi mwingine ingawa yeye hajui. Ninaamini kuwa nia ya kijana huyo ni kumtumia dada yangu tu. Sijui kama nikimwambia dada yangu atanisikia ama atahisi ninaingilia maisha yake binafsi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Sidhani ungependa kuacha dada yako aendelee kutumiwa vibaya na mtu ambaye unajua kwa hakika hana mienendo mizuri. Ni muhimu umwambie ili aweze kufanya uamuzi wake kuliko ukose kumwambia kisha uje kujuta baadaye akifikwa na mabaya.

 

Vichuna 2 wameteka moyo wangu, naomba wasiwahi kugundua

Kwako shangazi. Nina mpenzi ambaye nampenda sana. Hata hivyo, kuna mrembo tuliyekutana majuzi akanasa moyo wangu. Nilimdokezea hisia zangu na bila kusita akanikubalia ombi langu. Sasa changamoto iliyopo ni jinsi ambavyo nitaweza kuwa nao wawili bila wao kugundua. Nishauri.

Kupitia SMS

Ukikubali kuongozwa na tamaa utajipata pabaya. Kumbuka hao unaojaribu kuwachezea ni binadamu wenye akili zao. Muda si mrefu ukweli utafichuka utawakosa wote. Tunaambiwa kuwa mtaka yote hukosa yote.

 

Ninajua anapakua chungu kwa mwingine lakini amekana kabisa

Hujambo shangazi? Ninajua kwa hakika kuwa mwanamke ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili ana mwanamume mwingine, lakini amekana kabisa na kusisitiza kwamba hawana lolote. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Iwapo una hakika kwamba ana mwingine lakini amekanusha, kuna njia moja tu ya kumaliza mgogoro huo. Mtafute huyo mwanamume mwingine umuulize. Iwapo wanapendana atakuambia ukweli.

 

Mwanafunzi anadai kunipenda ila mimi naona ningali mdogo

Shikamoo shangazi! Mimi ni mwanafunzi wa shule ya upili na kuna kijana mwanafunzi mwenzangu anayenipenda. Hata hivyo, mimi sitaki uhusiano kwa sababu nataka kwanza nimalize masomo. Shida ni kuwa kila akiniuliza kuhusu uhusiano nikikataa huanza kulia. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Mapenzi ni haramu kwa wanafunzi kwa sababu yanaathiri vibaya masomo. Ushauri wangu ni kuwa ushikilie msimamo wako huo, umwambie bila kumbembeleza kwamba haiwezekani na haitawezekana. Mwambie pia akiendelea kukusumbua utamshtaki kwa mkuu wa shule ili akomeshwe.

 

Pesa nikitaka anipa lakini simuoni kwa macho, amenikimbia

Hujambo shangazi? Mimi nina mpenzi lakini ninashuku kuwa ananicheza pembeni. Sababu ni kuwa siku hizi nikimpigia simu au kumtumia SMS hajibu. Nikimuuliza anasema eti ana shughuli nyingi. Hata hivyo ananitimizia mahitaji yangu ya kifedha. Nishauri.

Kupitia SMS

Madai ya mpenzi wako ni kisingizio tu, ni lazima kuna sababu zinazomfanya asijibu simu zako, labda ana mwingine. Haiwezekani kwa wapenzi kuishi bila kuwasiliana. Chunguza ujue ukweli ili uchukue hatua inayofaa.

 

Nimemfumania mke na rafiki yangu wa dhati, nifanyeje mie?

Shangazi nahitaji ushauri wako. Nina umri wa miaka 36 na nina mke na watoto watatu. Nampenda sana mke wangu na sijawahi kumshuku hata siku moja. Lakini nilishtuka juzi nilipomfumania peupe na mwanamume rafiki yangu mkubwa. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Iwapo unavyosema ni kweli, huo ni usaliti wa hali ya juu, sio tu kutoka kwa mke wako, bali pia kwa rafiki yako. Kitendo hicho kinakupa haki ya kumuacha mara moja mke wako. Ukihisi una nafasi moyoni ya kumsamehe unaweza kufanya hivyo bora tu akuahidi kwa hakika kwamba hatarudia.