Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi wa mamangu ananimezea mate, nifanyeje?

November 1st, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina umri wa miaka 24 na mimi ndiye mtoto wa pekee wa mama yangu. Mama yangu hajaolewa lakini ana mwanamume mpenzi wake. Tatizo ni kwamba mwanamume huyo ananitaka kimapenzi. Amekuwa akija nyumbani kwetu akijua mama hayuko na kuniambia jinsi anavyonipenda eti yuko tayari kumuacha mama yangu kisha anioe. Mimi kamwe siwezi na kutokana na jaribio lake hilo nimejua kuwa si mwaminifu kwa mama yangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Huyo hastahili hata kuitwa mwanamume bali ni paka shume ambaye anaongozwa na tamaa. Hatua yake ya kukunyemelea kimapenzi inaonyesha wazi kuwa haheshimu nafsi yake wala hamheshimu mama yako. Ni muhimu umwambie ukweli mama yako ili ajue kwamba mwanamume anayejifanya kuwa mpenzi wake ni tapeli wa kimapenzi. Ninaamini kuwa huo utakuwa mwisho wa uhusiano wao lakini itakuwa heri kwa mama yako.

 

Mpenzi alia sichezi ngoma akatosheka, naogoga sasa huenda akaniacha

Shangazi pokea salamu zangu. Tafadhali nahitaji msaada wako. Nina hali ambayo inatishia kuharibu uhusiano wangu wa kimapenzi. Nimekuwa na mpenzi kwa karibu mwaka mmoja sasa. Kila mara tukikutana kufurahia mahaba huwa analalamika kwamba simtoshelezi. Naona aibu na kuhisi vibaya sana kutokana na upungufu wangu huo na nahofia kuwa muda si mrefu ataniacha. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ninaamini kuwa huna kasoro yoyote kimaumbile, kwa hivyo una uwezo wa kutekeleza wajibu huo ipasavyo. Mpenzi wako anakosea kwa kukulaumu na lawama zake hizo ndizo zinazokufanya ujihisi kuwa mpungufu. Hilo ni jambo ambalo mnaweza kusuluhisha pamoja kupitia mashauriano. Nyinyi ni wapenzi kwa hivyo mnafaa kujadiliana kwa uwazi mambo yanayowahusu. Mwenzako anaweza kukuelekeza wakati wa shughuli hiyo kuhusu jinsi ya kufanya ili kuhakikisha kuwa ametosheka. Shauriana naye.

 

Anataka kunioa ila mimi nahisi nipate kazi kwanza kabla ya ndoa, nipe ushauri

Habari zako shangazi? Mpenzi wangu ambaye tumekuwa pamoja kwa miaka mitatu alipata kazi hivi majuzi baada ya kutafuta kwa miaka kadhaa. Nilikamilisha elimu ya chuo kikuu mwaka uliopita na bado sijapata kazi. Sasa ameaniambia anataka kunioa lakini mimi naona kwanza ningoje hadi nipate kazi. Waonaje?

Kupitia SMS

Ni jambo la maana kwako kupata kazi ili uwe na uwezo kujitegemea hata ukiolewa. Hata hivyo, siku hizi si rahisi kupata kazi kwa hivyo hujui utasubiri kwa muda gani na labda mwenzako anahisi kuwa wakati wake wa kuoa umewadia. Kama umeamua kuwa ndiye atakuwa mume wako, unaweza kukubali ombi lake. Hali ni kwamba amepata kazi ina maana kuwa akikuoa ana uwezo wa kugharimia mahitaji yenu huku ukiendelea kutafuta kazi.

 

Nimepumbazwa kwa mapenzi, nikikosa kumuona jamani napata kichefuchefu

Shangazi naomba msaada wako. Nina umri wa miaka 21 na nimependana na mwanamume mwenye umri wa miaka 32. Tumejuana kwa miezi sita sasa na amenipumbuza sana kwa mapenzi yake ya hali ya juu. Tatizo ni kwamba siku ikipita kabla hajaniona ama kunijulia huwa ninachafuka roho na kuanza kufikiria kuwa ana mwingine. Je, hiyo ni kawaida?

Kupitia SMS

Hiyo ni hali ya kawaida hasa uhusiano unapokuwa mchanga kama huo wenu na pia kama mnapendana sana. Mapenzi ya dhati huwa na wivu pia na ndiyo maana usipomuona mpenzi wako unaanza kuwa na hofu kwamba amepata mwingine. Hata hivyo, hali hiyo ni ya muda tu. Jinsi uhusiano wenu unavyoendelea kukita mizizi, hali hiyo itaendelea kupungua na pengine kutoweka.

 

Mume wa jirani anadai kunipenda

Kuna mwanamume jirani yangu ambaye ana mke lakini yeye huniandama kila asubuhi ninapoelekea kibaruani akidai ananipenda. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Ni vyema kwamba unatambua huyo ni mume wa mtu na labda watoto wake unawafahamu vyema. Mueleze wazi msimamo wako ambao hujatueleza.