Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi wa mbali amejaa wasiwasi na maswali!

August 14th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

MAMBO shangazi? Nina mpenzi tunayependana sana. Ninaishi mbali naye na amekuwa na wasiwasi kuwa niliko nina mwingine. Kila tukiongea kwa simu ni lazima aniulize niko wapi, niko na nani na ninafanya nini? Sijui nitafanya nini ili aweze kuniamini. Nishauri.

Kupitia SMS

Mapenzi yana wivu na hata zaidi kwa wapenzi ambao kila mmoja anaishi mbali na mwenzake. Kama mwenzako hana sababu nzuri ya kukushuku, basi hali yake hiyo inatokana na wivu wa kimapenzi tu. Jinsi pekee ya kujaribu kumuondolea hofu ni kumpigia simu mara kwa mara kumhakikishia kuwa ni yeye tu, huna mwingine. Ni muhimu pia kila mmoja wenu kumtembelea mwenzake kila ikiwezekana ili kuchochea penzi lenu.

 

Mke hanijali tena hupigiwa simu na wanaume hata tukiwa pamoja

Habari yako shangazi? Nina umri wa miaka 29 na nina mke na mtoto mmoja. Katika siku za hivi karibuni, mke wangu amekuwa akipigiwa simu hata usiku na wanaume ambao wanamtongoza. Ninaumwa sana moyoni akipokea simu hizo na kuzungumza na wanaume hao mbele yangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni jambo la kawaida kwa wanaume kuwatongoza wanawake, walio katika uhusiano wa kimapenzi na pia walioolewa. Hata hivyo, nahisi kuwa mke wako anakukosea heshima kwa kupokea simu za wanaume kama hao na kuzungumza nao ukisikia.

 

Nampenda ila kazi ni kunizungusha bila kunipa jibu nitakalo

Shikamoo shangazi! Kuna mwanamke ambaye ameteka moyo wangu na nimempigia simu mara kadhaa kumwelezea. Nimekuwa nikitaka tukutane tuongee lakini ananizungusha tu, sijui ana mpango gani. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Subira ni muhimu sana katika shughuli ya kutafuta mpenzi. Kama umemdokezea mwanamke huyo hisia zako kwake, ni vyema umpe muda wa kutosha ili afikirie kuhusu jambo hilo. Inawezekana pia hana hisia kwako na ndiyo maana hataki mkutane. Hali kwamba unampenda haina maana kuwa naye pia anakupenda. Kwa sababu hiyo, usiweke matumaini yako yote kwake. Kuwa tayari kwa jibu lolote lile kutoka kwake.

 

Ameniambia nisubiri ndoa sasa ni mwaka wa pili, niendelee?

Kwako shangazi. Nina mpenzi na ninampenda sana. Hata hivyo, kuna jambo fulani kumhusu ambalo linanitatiza. Amekuwa akiniambia atanioa na sasa tumekuwa pamoja kwa miaka miwili. Kila nikimuuliza huniambia nisubiri tu. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ndoa inahitaji mpango na makubaliano kati ya wahusika. Mkikubaliana mnaweza kusubiri hata miaka mitano. Kama kweli mwanamume huyo yuko tayari kukuoa, anafaa kukwambia wakati ambao anahisi atakuwa tayari ili ujue badala ya kukwambia usubiri tu. Iwapo hujawahi kumuuliza, basi fanya hivyo.

 

Nimeonywa na wengi niachane naye huyu binti ila nampenda sana sasa shangazi nifanye nini?

Shikamoo shangazi! Ninahitaji ushauri wako. Nimekuwa na uhusiano na msichana fulani kwa miezi miwili sasa na ninampenda sana. Ajabu ni kuwa watu wengi wanaomjua wamenionya niachane naye. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hujaelezea iwapo watu wanaokuonya wamekupatia sababu za kukushauri uachane na msichana huyo. Ingawa kuna watu wengine wasiopenda kuona wawili wakipendana, haiwezekani kwamba watu wote wanaokuonya wananuia kuvunja uhusiano wenu bila sababu. Ni muhimu uchunguze wanayosema kuhusu mpenzi wako ili uweze kufanya uamuzi wa busara.