Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi wa pembeni ametimuliwa na mumewe, nifanyeje?

November 12th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 26, nimeoa na tumejaliwa watoto wawili. Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamke ambaye tulikuwa wapenzi hapo awali lakini akaolewa na mwanamume mwingine. Juzi mume wake aligundua kuhusu uhusiano wetu na akamfukuza nyumbani kwake pamoja na mtoto wao. Sasa ananitegemea mimi kugharamia kodi ya nyumba na mahitaji yake mengine ilhali mapato yangu ni duni. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ni jambo la kushangaza kwamba unatafuta ushauri kuhusu jinsi ya kutatua tatizo ambalo umelitafuta wewe mwenyewe. Ulitoka nje ya ndoa yako ukashikana na mke wa mwenyewe ukimwambia kwamba unampenda. Sasa umemharibia ndoa, huna haja naye tena kwa sababu unahisi atakuwa mzigo kwako. Beba mzigo wako.

 

Shangazi jamani mbona unapotosha wanawake katika ukumbi huu?

Kwako shangazi. Heko kwa kazi yako nzuri katika ukumbi huu. Hata hivyo, ninahisi kwamba unawapotosha wanawake kuhusu hali ya wanaume ya kuwa na wanawake zaidi ya mmoja. Je, wewe hujui kwamba mwanamume anaweza kuoa zaidi ya mwanamke mmoja?

Kupitia SMS

Mimi kamwe sijapinga uwezekano wa mwanamume kuoa zaidi ya mwanamke mmoja. Kile ninachopinga ni mwanamume aliye katika ndoa kuwa na wanawake wengine wa pembeni kwa sababu hiyo si haki kwa mke wake. Mwanamume ambaye ameoa akimpenda mwanamke mwingine anafaa kumuoa kwa kuzingatia utaratibu unaofaa ili kuweka rasmi uhusiano wao.

 

Nimekutana naye akiwa na wanawake kadha anaodai ni marafiki, anihadaa?

Vipi shangazi? Nina umri wa miaka 21 na mpenzi wangu ni mwanafunzi wa chuo kikuu. Ninajua ananipenda lakini kuna jambo fulani kumhusu ambalo linanitatiza moyoni. Nimekutana naye mara kadhaa akiwa na wanawake wengine na nikimuuliza ananiambia ni marafiki tu na kunihakikishia kuwa mimi ndiye wake. Marafiki zangu pia wanashuku kwamba ananicheza. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni vyema unajua kwa hakika kwamba mwanamume huyo anakupenda naye pia amekuhakikishia hivyo. Ingawa unasema umemuona na wanawake wengine, huna ushahidi wowote kwamba ana uhusiano wa kimapenzi nao na inawezekana kuwa ni marafiki tu kama anavyokwambia. Hata hivyo, ni muhimu umwelezee unavyohisi ukimuona na wanawake wengine ili atafute namna ya kurekebisha hali hiyo.

 

Tuliachana lakini hunipigia simu eti hataki kuniona na wanaume wengine

Kwako shangazi. Kuna mwanamume tuliyekuwa wapenzi na tukaachana baada ya kutofautiana. Sasa amepata mwingine lakini amekuwa akinipigia simu na kunitumia SMS kuniambia eti hataki kuniona na mwanamume mwingine. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mwanamume huyo kamwe hana haki wala mamlaka katika maisha yako kwa sababu uhusiano wenu ulikwisha tena akapata mwingine. Anafaa kukusahau kabisa na badala yake kuzingatia uhusiano wake mpya. Mpuuze na uendelee na maisha yako. Itakuwa vyema zaidi ubadilishe nambari yako ya simu ili akome kukusumbua.

 

Nampenda sana mchumba wangu tatizo ni kuwa tuko katika dini tofauti

Shikamoo shangazi! Nina mchumba tunayependana sana na niko tayari kumuoa. Lakini imani zetu tofauti za kidini zimekuwa kikwazo. Yeye ni Muislamu na baba yake anasisitiza nisilimu ndipo niweze kumuoa binti yake. Lakini nami nimezaliwa na kulelewa katika familia ya Kikristo na naona vigumu sana kubadili imani yangu. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Tofauti ya imani inaweza kuwa kizingiti kikubwa katika uhusiano wa kimapenzi na wakati mwingine hata inaweza kuuvunja. Hali inapokuwa hiyo, inabidi mmoja wa wahusika akubali kubadili imani yake ya kidini ili kudumisha uhusiano. Lakini hilo halitawezekana kati yenu, basi huo utakuwa mwisho wa maisha yenu pamoja ili kila mmoja wenu atafute mwingine kutoka kwa dini yake.