Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi wa rafiki yangu ananitia kwenye majaribu

April 9th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nina umri wa miaka 36 na bado sijapata mpenzi, naendelea kutafuta. Kuna mwanamke mpenzi wa rafiki yangu ambaye simuelewi. Ni mara mbili sasa akinitumia SMS kunishawishi tuwe na uhusiano wa kisiri ilhali anajua mpenzi wake ni rafiki yangu mkubwa. Ni mrembo sana na sijui nitafanya nini kumuepuka kwani sitaki kumkosea rafiki yangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Tabia ya mpenzi wa rafiki yako si ya mtu mwaminifu na anayempenda mwenzake kwa dhati. Ni ajabu kwamba haoni aibu kukutongoza na anajua vizuri kuwa wewe ni rafiki mkubwa wa mpenzi wake. Itakuwa makosa kwako kuingia katika mtego wake kwani rafiki yako akijua mtakosana. Mwambie wazi kuwa hutaki na kwamba akisisitiza utamwambia rafiki yako.

 

Nimejaribu kila aina ya mbinu na bado hanitaki

Shangazi pokea salamu zangu. Kuna mwanamke ambaye nimekuwa nikimtaka kwa miaka mitatu sasa lakini amenikataa kabisa. Nimemuahidi chochote anachotaka lakini hataki! Nimfanye nini?

Kupitia SMS

Kupenda ni moyo wala hakutegemei vitu unavyomuahidi mtu. Kama amekukataa kwa muda wote huo, sidhani atabadili msimamo wake na kuendelea kumfuata ni kupoteza wakati wako.

 

Umaskini wa kwetu unanitia woga

Kwako shangazi. Nimevutiwa sana na msichana tunayesoma pamoja chuo kikuu. Najua anaweza kunikubali lakini nahofia kuwa wazazi wake watapinga uhusiano wetu kwa sababu wana pesa ilhali ninatoka familia maskini. Nifanyeje?

Kupitia SMS

Hakuna sheria inayosema kuwa ni lazima maskini aolewe na maskini na tajiri kuolewa na tajiri. Mapenzi hayajui mipaka ya rangi wala pesa. Msichana mwenyewe akikupenda wazazi wake hawatakuwa kizuizi kwani yeye ni mtu mzima na ana haki ya kujichachagulia mpenzi.

 

Hisia zimepungua

Kwako shangazi. Nina mpenzi na tumekuwa tukiishi pamoja kwa miaka miwili sasa ingawa hatujaoana. Sasa tumeanza kupanga harusi lakini hisia zangu kwake zimepungua si kama hapo awali. Nahofia kuwa nikimuoa ndoa yetu haitakuwa na ladha. Nishauri.

Kupitia SMS

Sielewi ni kwa nini mliamua kuishi pamoja kabla hamjaoana. Hali ya kupungua kwa hisia zako kwake imetokana na mazoea ya muda ambao mmekuwa pamoja. Ninaamini yeye pia anahisi vivyo hivyo ingawa hajakwambia. Ni muhimu umfungulie moyo wako kuhusu suala hili kisha mshauriane na kufanya uamuzi wa busara.

 

Nitaanza vipi?

Vipi shangazi? Kuna msichana ambaye ninampenda lakini sijui nitaanzia wapi kuzungumza naye ili nipate nafasi ya kumwelezea hisia zangu kwake. Nishauri.

Kupitia SMS

Ukweli ni kwamba hakuna jinsi ambavyo msichana huyo atajua kuwa unampenda hadi siku utakapomwambia. Inaonekana unaogopa kumwambia na itabidi uondoe woga kama kweli unamtaka.

 

Ni mwembamba kama sindano

Shangazi moyo wangu umekwama kwa mrembo jirani yetu naye pia ameungama kuwa ananipenda. Tatizo ni maumbile yake kwani ni mwembamba kama sindano nami sipendi wanawake wembamba. Sijui nitafanya nini sababu amenizuzua kiasi kwamba sijali maumbile yake.

Kupitia SMS

Utakubaliana nami kuwa hisia za moyoni zina nguvu kuliko macho. Umesema kuwa penzi lako kwake ni zito kiasi kwamba hujali maumbile yake. Hayo ndiyo mapenzi ya dhati. Isitoshe, mwili si jiwe, unabadilika kulingana na wakati. Ukimuoa msichana huyo na kumtunza vyema atanenepa awe jinsi unavyotaka.

 

Bado ninampenda

Hujambo shangazi. Kuna mwanamke tuliyekuwa na uhusiano na tukaachana baada ya kuwa pamoja kwa muda mfupi tu. Ninahisi kwamba bado nampenda lakini naogopa kumwambia. Nishauri.

Kupitia SMS

Itabidi umtafute mwanamke huyo umwelezee unavyohisi kwa sababu hajui na hatajua hadi utakapomwambia. Kama kweli mlikuwa wapenzi, sielewi ni kwa nini unaogopa kumtafuta umwelezee unavyohisi. Wewe ndiwe uliye na haja naye, kwa hivyo mtafute.