Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mume wangu bado anafuatafuata mke wa zamani

March 5th, 2018 2 min read

Kwako shangazi. Nimeolewa na mwanamume ambaye alikuwa amezaa na mwanamke mwingine kabla hajanioa. Sasa nimegundua bado anamfuata mwanamke huyo. Tafadhali nishauri.
Kupitia SMS

Iwapo unayosema ni kweli, inaonekana wawili hao wamefufua uhusiano wao ama hata hawakuachana licha ya mwanamume huyo kukuoa. Ni muhimu ujue msimamo wa mume wako kuhusu suala hilo ndipo uchukue hatua unayohisi inafaa.

 

Aliyenipa mimba kahepa, nasumbuka

Vipi shangazi? Kuna mwanamume aliyenipa mimba kisha akanihepa na kuoa mwanamke mwingine. Sasa wazazi wananilaumu na wananifukuza nyumbani sijui nitaenda wapi. Kuna wengi wanaotamani kunioa. Nishauri.
Kupitia SMS

Ni kweli ulikosea, sio tu wazazi wako, bali wewe mwenyewe, kwa kuzaa kabla hujaolewa ingawa pia si vyema kwao kukufukuza nyumbani. Kama kuna wanaume wanaotaka kukuoa, chagua mmoja wao akuoe kwani baba ya mtoto wako tayari ana mke na hutarajii kuwa atakurudia.

 

Nashindwa kuacha tajiri huyu aliyeoa
Nina umri wa miaka 20 na nina uhusiano na mwanaume wa miaka 33 ambaye ameoa na wana watoto wawili. Nimejaribu kuachana naye lakini nimeshindwa kwa kuwa nampenda sana. Ameniwekea biashara na anataka kunioa mke wa pili lakini naogopa. Nishauri.
Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, ni dhahiri kuwa umekwama kwa mwanamume huyo na itakuwa vigumu kujitoa. Sasa huna budi ila kuendelea kuwa mpango wake wa kando ama ukubali kuolewa mke wa pili. Utaamua mwenyewe.

 

Nataka kutengana na mume mbanifu
Nimekuwa na mpenzi kwa miaka sita sasa lakini nahisi hanifai. Sababu ni kuwa tangu tujuane hajawahi kuninunulia chochote bila kumuitisha, hata pesa za matumizi ni lazima nimuombe. Nimejaribu kumrekebisha lakini nimeshindwa. Nishauri.
Kupitia SMS

Inawezekana kuwa mwanaume huyo hajui jinsi ya kujenga na kutunza uhusiano ama ni mkono gamu tu. Uhusiano ni chaguo la mtu binafsi kwa hivyo kama unahisi huyo siye mtu ambaye ungependa kuishi naye unaweza kujiondoa katika uhusiano huo.

 

Mchumba hataki nimlipie mahari
Hujambo shangazi. Nimekuwa na uhusiano na mwanamke fulani ambaye ana mtoto kwa miaka mitano sasa. Niko tayari kupeleka mahari kwa wazazi wake lakini amekataa. Nifanye nini?
Kupitia SMS

Hizo ni dalili kwamba mwanamke huyo hajaamua kwamba wewe ndiye utakuwa mume wake. Anajua vyema kuwa kupeleka mahari ni kuhalalisha ndoa na ndiyo maana amekataa. Kama unamtaka mke inaonekana haitawezekana.

 

Jamaa ninayempenda ni mkali kama chui
Hujambo shangazi. Nimepandana na kijana fulani lakini tatizo ni kuwa ni mkali sana hata namuogopa. Sasa sijui itakuwaje akinioa. Naomba ushauri wako.
Kupitia SMS

Kama tayari anakuonyesha ukali hata unamuogopa ilhali nyinyi bado ni wapenzi, nahisi kutakuwa na shida utakapokuwa mke wake. Itabidi uchukue hatua inayofaa kabla hamjaenda mbali.

 

Natamani mpenzi ila naogopa wanaume
Vipi Shangazi? Mimi ni msichana mwenye umri wa miaka 20. Natamani sana kuwa na mpenzi lakini huwa naogopa kuzungumza na wanaume. Nimejaribu kuondoa uoga huo nimeshindwa. Nishauri.
Kupitia SMS

Hiyo ni hali inayotokana na maumbile na watu wameumbwa kwa namna tofauti. Hata hivyo, maumbile hubadilika jinsi mtu anavyokuwa. Jaribu uwezavyo kutangamana na wanaume na hatimaye woga wa kuzungumza nao utakutoka.

 

Nina hamu kubwa ya kuwa na mume
Shangazi shikamoo. mimi ni msichana mwenye umri wa miaka na 23 sina mpenzi. Natamani sana kuwa na kwangu. Nishauri.
Kupitia SMS

Mapenzi hayanunuliwi dukani kama nguo mwanangu. Ni lazima kwanza mwanamume akuone, akupende, nawe pia umpende ndipo muwe wapenzi. Utaratibu huo unaweza kuchukua muda mrefu na itabidi uwe na subira. Isitoshe, wewe bado ni mchanga na huna haja ya kuwa na wasiwasi.