Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Mwenzangu amekatiza uhusiano wetu, naumia!

September 17th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nimekuwa na mpenzi na alikuwa ameniahidi kuwa atanioa. Mwezi uliopita alihamishwa kikazi hadi mji tofauti na akaniahidi kuwa atakuwa akinitembelea angalau mara mbili kwa mwezi. Licha ya ahadi zote hizo, mwenzangu ameniacha kwa mataa. Juzi alinipigia simu akaniambia uhusiano wetu umekwisha kwa sababu amepata mwingine. Nimevunjika sana moyoni, sijui nitafanya nini. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ni wazi kuwa mwanamume huyo hakuwa na mapenzi ya dhati kwako na ndiyo maana amemnyakua mwanamke mwingine kwa muda mfupi tu. Ingawa unasema unampenda, itabidi ukubali kuwa huna nafasi tena katika moyo wake kwa sababu amekwambia wazi kuwa amepata mwingine. Ondoa moyo na mawazo yako kwake ndipo uweze kuendelea na maisha yako.

 

Aniomba radhi baada ya miaka miwili

Salamu kwako shangazi. Mpenzi wangu ambaye nilikuwa nimempa moyo wangu wote alikatiza mawasiliano ghafla bila sababu na akabadilisha namba yake ya simu. Niligundua baadaye kwamba alipata mwingine. Huu sasa ni mwaka wa pili na nimeshindwa kabisa kumsahau na kufikia sasa sijafungua moyo wangu kwa mwanamume mwingine. Nilishangaa juzi aliponipigia simu kuniomba msamaha na kutaka turudiane. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hali kwamba kufikia sasa hujamtoa mwanamume huyo katika moyo wako ili kuweza kuendelea na maisha yako kimapenzi ni thibitisho kuwa unampenda kwa dhati. Huenda hali ni hiyo hiyo kwa upande wake kwani amekufuata baada ya miaka miwili ya uhusiano na mwanamke mwingine. Kama unahisi bado una nafasi yake katika moyo wako, msamehe kisha mrudishe uhusiano wenu.

 

Sijamwona tena baada ya kumzima

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 22. Miezi miwili iliyopita nilikutana na mwanamume aliyeniambia ananipenda na nikamuomba anipe muda ili nifikirie kuhusu ombi lake. Tuliendelea kuwasiliana kwa simu na hatimaye akateka hisia zangu. Hata hivyo, alinishangaza tulipokutana mara ya pili kwa kuniomba tushiriki mapenzi. Nilikataa na tangu siku hiyo sijamuona wala kumsikia tena. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ulifanya uamuzi wa busara kutoingia katika mtego wa mwanamume huyo na hufai kujuta. Hali kwamba alitaka mshiriki mapenzi muda mfupi tu baada ya nyinyi kujuana na ulipokataa akatoweka ni thibitisho kuwa hilo hasa ndilo lilikuwa lengo lake kwako. Muondoe kabisa katika mawazo yako.

 

Sidhani nitamwamini tena

Kwako shangazi. Nina mpenzi tunayependana sana, lakini nilikasirika sana juzi kuona ametumiwa ujumbe wa kimapenzi na mwanamke mwingine na nilipomuuliza akamkana akidai eti hamjui. Nimemwamini kwa miaka mitatu ya uhusiano wetu na sidhani nitaweza kumwamini tena. Nishauri.

Kupitia SMS

Wakati mwingine watu hukosea kwa kulaumu wenzao bila kuwa na hakika. Mpenzi wako alitumiwa ujumbe tu, hukumfumania na mwanamke huyo. Inawezekana ujumbe huo ulitumwa kimakosa kwa namba yake ama labda mwanamke huyo ana nia ya kuharibu uhusiano wenu. Tuliza moyo kwanza kisha uchunguze ujue ukweli ndipo uweze kufanya uamuzi wa busara.

 

Nilikuwa nimempa moyo wangu wote, lakini amenisaliti

Kwako shangazi. Nimekuwa katika uhusiano na mwanamume ninayempenda sana na ameniahidi kuwa atanioa. Hata hivyo, nimegundua kuwa nimedanganywa. Juzi mwanamke fulani alinipigia simu usiku akitumia simu ya mwanamume huyo akaniambia niachane na mpenzi wake. Tangu siku hiyo mwanamume huyo amekuwa akipuuza simu zangu. Nilikuwa nimempa moyo wangu na siamini kuwa amenitendea hivyo. Nishauri.

Kupitia SMS

Kisa hicho kinaonyesha wazi kuwa mwanamume huyo hakupendi na alitaka tu kukutumia kwa muda. Ndiyo maana alimtumia mwanamke huyo kukufahamisha kwamba ana mpenzi wa dhati na hakutaki tena maishani mwake. Ninaelewa kuwa tukio hilo limekuumiza sana moyoni lakini lisikukoseshe usingizi. Wanaume ni wengi na wakati ukiwadia utampata anayekufaa.