Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nahisi hana haja tuoane ilhali anadai kunipenda

October 11th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

VIPI shangazi? Nimekuwa na mpenzi kwa miaka mitatu sasa na ninampenda sana naye pia amekuwa akisema ananipenda. Hata hivyo, ninahisi kwamba nia yake katika uhusiano wetu si ndoa. Sababu ni kwamba nimejaribu mara kadhaa kumvuta kwa mazungumzo kuhusu ndoa kati yetu lakini kila nikifanya hivyo anatafuta namna ya kuhepa suala hilo. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Hatua ya ndoa kati ya wapenzi hutokana na maelewano kati yao. Ni muhimu ujue kuwa si kila uhusiano wa kimapenzi unaofikia ndoa. Huenda mwenzako ameamua kuwa huwezi kuwa mke wake na kama ndivyo huwezi kumlazimisha. Sasa ni juu yako kuamua iwapo unataka kuendelea naye.

 

Mpenzi wa mwaka 1 ameniwacha ghafla hata simu hapokei

Shikamoo shangazi! Nimekuwa na mpenzi kwa karibu mwaka mmoja sasa lakini ameniacha ghafla bila sababu na kukatiza mawasiliano. Nimempigia simu mara nyingi lakini hapatikani. Juzi nilikutana na rafiki yake akaniambia alibadilisha nambari yake ya simu. Tafadhali nisaidie.

Kupitia SMS

Sijui unataka nikusaidie namna gani kwa sababu mimi simjui huyo mpenzi wako wala sina nambari yake ya simu. Pili, hali kwamba amekatiza hata mawasiliano ya simu ni thibitisho kuwa hataki uhusiano wenu. Haina haja kuhangaika kuhusu mtu asiyekutaka. Achana naye na utafute mwingine.

 

Mume aliniwacha sasa jamaa zake wataka nirudi ila yeye hajanipa idhini

Kwako shangazi. Nilikuwa nimeolewa lakini mume wangu akaniacha bila sababu yoyote. Huu ni mwaka wa tatu na bado sijaolewa tena kwa sababu nilimpenda kwa moyo wangu wote na sidhani ninaweza kumpata mwingine kama yeye. Wazazi na jamaa zake wamekuwa wakinishawishi nirudi lakini siwezi kufanya hivyo bila idhini yake. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Unaungama wazi kuwa bado unampenda mwanamume huyo ingawa alikuacha bila sababu. Hata hivyo, sidhani ungetaka kumrudia ili kuwaridhisha wazazi wake tu ilhali yeye mwenyewe hakutaki. Utajiongezea majonzi kuishi nyumbani kwa mtu unayempenda ilhali yeye hakujali. Ushauri wangu ni kwamba uondoe mawazo yako kwake kisha uweke huru moyo wako ili uweze kutafuta mume mwingine.

 

Mimi ni mrembo ajabu, nikienda maskani za burudani wanaume hawatulii

Vipi shangazi? Mimi ni mwanamke mwenye umri wa miaka 24 na kusema kweli mimi ni mrembo. Tatizo ni kuwa kila nikienda katika maskani za starehe huwa sina amani kutokana na wanaume kunisimbua wakitaka uhusiano ilhali mimi bado sijawa tayari. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Sidhani kuna jinsi utaweza kuepuka kero za wanaume popote unapoenda hasa kwa sababu huna mpenzi tena unaungama kuwa wewe ni mrembo. Ni kawaida ya wanaume kuwaandama wanawake warembo. Jinsi pekee ya kuwaepuka ni kuwaambia wazi kuwa huna haja na mpenzi kwa sasa kwani hawawezi kukulazimisha.

 

Nimependa lakini ni mzee kwangu sijui nikimpeleka kwetu hali itakuwaje

Shangazi pokea salamu zangu. Nina umri wa miaka 30 na nimependana na mwanamke wa miaka 41. Alikuwa ameolewa lakini wakaachana na mume wake wakiwa na mtoto mmoja. Ninampenda kwa dhati na niko tayari kumuoa. Bado sijamtambulisha kwa wazazi na jamaa zangu na ninajua kwa hakika watashangaa ni kwa nini nimeamua kuoa mwanamke aliyenizidi umri tena aliye na mtoto. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Mapenzi na ndoa ni uamuzi wa mtu binafsi na haufai kuingiliwa na mtu yeyote. Ukitaka kuishi maisha mazuri, usijali wanayosema watu kuhusu mwelekeo unaochukua maishani bora tu unaamini ndio unaofaa. Kama umempenda mwanamke huyo na unahisi ndiye anayefaa kuwa mke wako usiogope watakayosema wazazi, jamaa au marafiki. Watasema wachoke na mwishowe watanyamaza.