Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nahisi maisha hayana maana bila yeye, nifanyeje?

August 29th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SHIKAMOO shangazi! Nina tatizo fulani na tafadhali nakuomba unishauri kuhusu jinsi ya kulitatua. Nina umri wa miaka 24 na nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani. Hata hivyo, tuliachana miezi kadhaa kufuatia tofauti kidogo kati yetu. Ninampenda sana na nahisi maisha hayana maana kwangu bila kuwa naye. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Unasema mliachana kutokana na tofauti kidogo na hiyo ina maana mnaweza kushauriana na kusuluhisha. Inawezekana pia mlipokuwa pamoja hujamwelezea uzito wa penzi lako kwake kwa hivyo hana habari kuhusu hali unayopitia bila kuwa naye. Ushauri wangu ni kuwa umtafute umwelezee unavyohisi uone kama atabadili nia yake.

 

Natafuta aliyenihepa baada ya kunipa mimba tulee mtoto

VIPI shangazi? Nilikuwa na mpenzi lakini akanihepa baada ya kunipa mimba. Ninatamani sana kumpata mwanamume ili tushirikiane maishani na nimekuwa nikimtafuta lakini sijafaulu. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Ulichangia hali yako hiyo kwa kukubali kubeba mimba nje ya ndoa. Kwa sasa huna lingine ila kuendelea kumlea mwanao huku ukitafuta mwenzako maishani. Ni muhimu ufahamu kuwa si jambo rahisi kumpata mwenza wa maisha kwa hivyo unafaa kuwa na subira.

 

Mume wa zamani ameoa, nami pia nina kipenzi ila hatujawahi kuzungumzia suala hili

Kwako shangazi. Nilikuwa nimeolewa lakini tukakosana na mume wangu na tukaachana. Nimepata habari kwamba ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamke mwingine. Mimi pia nimepata mchumba ingawa bado hatujazungumzia suala la ndoa. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Huna sababu ya kuhangaika moyoni kuhusu aliyekuwa mume wako kwa iwapo kweli ameshikana na mwanamke mwingine. Hatua yake hiyo inaonyesha kuwa ameamua kwamba ndoa yenu imekwisha. Kama umepata mchumba na unaamini anakufaa, usipoteze nafasi hiyo, kubali uolewe.

 

Nina mimba yake, nimeshangaa ana mke na watoto kijijini kwao

Kwako shangazi. Nimekuwa katika ndoa kwa mwaka mmoja na sasa nina mimba ya mtoto wetu wa kwanza. Tunaishi mjini na mume wangu na hajawahi kunipeleka kwao. Nimeshangaa sana kugundua kwamba ana mke mwingine na watoto wawili ambao wanaishi kwao mashambani. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ulifanya makosa kukubali kuolewa na mwanamume huyo kabla hajakupeleka nyumbani kwao kukujulisha kwa wazazi na jamaa zake. Kama ungechukua hatua hiyo mapema ungejua kuwa ana mke. Uamuzi wako sasa utategemea iwapo uko tayari kuwa mke wake wa pili kwani unasema umebeba mimba yake.

 

Nimepata ujauzito na mpango wa kando, sasa ataka niache mume wangu ili anioe

Vipi shangazi? Nimeolewa na tumejaliwa mtoto mmoja. Nimekuwa kwenye uhusiano wa kimapenzi na mwanamume mwingine kwa miaka mitatu na sasa nina mimba yake. Anataka nimuache mume wangu ili anioe na kusema kweli nampenda hata kuliko mume wangu. Tafadhali nishauri.

Kupitia SMS

Kulingana na maelezo yako, inaonekana moyo wako ulitoka kitambo katika ndoa yako ulipoanza uhusiano wa pembeni na ndiyo maana hata umeamua kubeba mimba ya mpango wa kando. Badala ya kuendelea kujidanganya eti uliye naye ni mume wako, ni heri umwambie ukweli ili muachane uolewe na huyo unayempenda.

 

Nilimfungulia moyo wangu ila amekimya tu hasemi lolote!

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 22 na kuna mwanamume ninayempenda sana. Juzi nililazimika kumwambia wazi kuwa nampenda lakini alinyamaza tu. Nahisi ananipenda lakini sielewi ni kwa nini amekawia kunifungulia moyo wake. Nishauri tafadhali.

Kupitia SMS

Inaonekana kuwa wewe ndiye unayempenda mwanamume huyo, labda yeye hana hisia zozote kwako. Sababu ni kuwa hajawahi kukwambia anakupenda hata baada ya wewe kuungama penzi lako kwake. Itakuwa vyema umuulize msimamo wake usije ukawa unapoteza wakati wako bure kwa mtu asiye na haja nawe.