Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nahitaji mpenzi lakini nahofia kuchezewa tena

May 22nd, 2020 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Nina umri wa miaka 28 na nilipata mtoto punde tu baada ya kukamilisha elimu ya shule ya upili. Mwanamume aliyekuwa mpenzi wangu akaniacha baada ya kunipa mimba. Nimeamua kuendelea na masomo ili niweze kujitegemea maishani. Kuna mwalimu wangu ambaye ananitaka kimapenzi na hata ananiahidi ndoa. Nahitaji mpenzi lakini nahofia kuchezewa tena. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Uamuzi ambao umechukua ni wa busara. Siku hizi ni jambo la maana sana kwa mwanamke kuweza kujitegemea maishani ili kuepuka kuhangaishwa na wanaume wenye nia mbaya. Kutokana na kwamba ulivunjwa moyo na mpenzi wako wa kwanza, naonelea kwanza uzingatie kilichokufanya urudi chuoni. Kumbuka kuwa huyo ni mwalimu wako na uhusiano kati yenu unaweza kuathiri vibaya masomo yako. Hata kama unampenda, mwambie akupe muda utimize lengo lako.

Nimsisimue vipi?

Hujambo shangazi? Wakati fulani nilisoma katika ukumbi wako huu ukisema kuwa mapenzi hukosa utamu kutokana na wahusika kukosa ujuzi wa kusisimua hisia. Je, unaweza kunielezea jinsi ambavyo ninaweza kusisimua kikamilifu hisia za mwenzangu kwa lengo la kumridhisha chumbani?

Kupitia SMS

Suala zima la raha ya mahaba linategemea ubunifu wa wahusika wala haliwezi kufundishwa kama somo darasani. Kuna namna nyingi za kuamsha hisia za kimapenzi, kuanzia jinsi unavyomtazama machoni na kumzungumzia mwenzako hadi jinsi unavyogusa ama kupapasa sehemu tofauti za mwili wake. Hizi ni baadhi tu za jinsi za kuchochea hali chumbani na ninasisitiza kuwa kufaulu kwake kunategemea ubunifu wa mtu binafsi.

Tabia yake yanikera

Vipi shangazi? Nimekuja kwako unisaidie. Kuna mwanamume ambaye tumekuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa miezi kadhaa sasa. Jambo linalonishangaza ni kuwa akiwa nyumbani kwake hawezi kupokea simu zangu na wakati mwingine hata anazima simu. Tabia yake hiyo inanifanya nishuku huenda ana mke. Nishauri.

Kupitia SMS

Una sababu nzuri ya kumshuku mpenzi wako kutokana na tabia yake hiyo. Kuna uwezekano mkubwa kwamba mwanamume huyo ameoa ama anaishi na mwanamke mwingine na ndiyo sababu anashindwa kuzungumza nawe akiwa nyumbani. Anza uchunguzi mara moja ili ujue ukweli wa jambo hilo kabla hamjaenda mbali na uhusiano wenu asije akawa ni tapeli wa kimapenzi.