Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nahofia ataniacha baada ya rafiki yake kunichongea

September 7th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

SALAAM shangazi! Nimekuwa na uhusiano wa kimapenzi na mwanamume fulani kwa miaka minne. Mpenzi wangu alinipigia simu juzi kuniambia kuwa mtu fulani amemwambia eti nina uhusiano na mwanamume mwingine. Tangu hapo hajanipigia simu na nikimtumia SMS hajibu. Hajaniambia kuwa hanitaki lakini nahofia kuwa ataniacha. Sijui nitafanya nini kwani nampenda sana.

ZAWADI MOHAMMED, Mazeras

Mpenzi wako atakosea iwapo ataamua kukatiza uhusiano wenu kutokana na udaku wa mtu mwingine. Hali kwamba amekatiza mawasiliano kati yenu ni ishara kuwa habari hizo zimemchoma moyoni na ameamua kunyamaza ili kuzitathmini. Ukiweza mtafute ili mzungumze ana kwa ana kutatua suala hilo.

 

Sitaki mimba wala mipira na dawa ingawa ninatamani sana kuonja utamu

Shikamoo shangazi! Nina umri wa miaka 24 na nilikamilisha masomo ya chuo kikuu mapema mwaka huu. Ningependa kuwa na mpenzi lakini naogopa sana kupata mimba kabla sijaolewa. Je, kuna jinsi nyingine ya kukinga mimba mbali na kondomu na dawa?

Kupitia SMS

Sijui namna nyingine ya kukinga mimba isipokuwa hizo mbili ambazo umetaja. Kama hutaki kuzitumia na pia hutaki kupata mimba, basi itabidi ujiepushe kabisa na tendo hilo.

 

Aliniacha eti mimi ni maskini sasa anataka nichangie katika kulea mtoto

Kwako shangazi. Mwanamke aliyekuwa mpenzi wangu aliniacha akiwa na mimba yangu akashikana na mwanamume mwingine kwa madai kwamba mimi ni maskini. Sasa amejifungua na anataka nisaidie kugharimia malezi ya mtoto. Je, hiyo ni haki?

Kupitia SMS

Umesema mwanamke huyo alikuacha kwa madai kuwa wewe ni maskini. Kwa sababu hiyo, hafai kudai msaada wowote kutoka kwako bali kutoka kwa mpenzi wake wa sasa. Ninaamini mwanamume huyo alimkubali akijua kuwa alikuwa na mimba kwa hivyo pia anafaa kukubali kubeba mzigo wa kulea mtoto huyo kama bado wako pamoja.

 

Nahisi niliolewa kwake sababu ya pesa, sasa simtaki

Kwako shangazi. Nimeolewa kwa miaka mitatu sasa na nimegundua kuwa sina mapenzi ya dhati kwa mume wangu. Tulipokutana alikuwa na pesa nyingi na ninahisi kuwa nilivutiwa na pesa zake wala si mapenzi. Kuna mwanamume mwingine ambaye amenasa moyo wangu na yuko tayari kunioa. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Ingawa unasema hukuolewa kutokana na mapenzi yako kwa mume wako, ni muhimu uelewe kuwa yeye hajui hayo. Anachojua ni kwamba wewe ni mke wake na ulikubali akuoe kutokana na mapenzi yako kwake. Iwapo kweli umeamua huwezi kuendelea kuishi naye, itabidi utafute namna ya kumuelezea jambo hilo na ikiwezekana uwahusishe jamaa wa pande zote mbili.

 

Nimegundua ana mpenzi wa kando; hakika inaniuma

Mambo shangazi? Nimegundua kuwa mwanamume mpenzi wangu ana uhusiano na mwanamke mwingine. Wazo la mwanamke mwingine kuwa karibu naye linaniuma sana moyoni kwa sababu nampenda sana. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Tabia ya mpenzi wako huyo imethibitisha kuwa si mwaminifu kwako ingawa unasema unampenda sana. Mwambie wazi kuwa huwezi kuendelea na uhusiano wa aina hiyo ili achague kati yako na huyo mwingine.

 

Ninayependa sana huwaambia rafiki zake eti hanipendi

Shikamoo shangazi! Kuna kijana ambaye tumekuwa na uhusiano wa kimapenzi kwa miezi kadhaa sasa. Nampenda kwa dhati lakini yeye amekuwa akiwaambia marafiki zake kuwa hanipendi. Naomba ushauri wako.

Kupitia SMS

Hujaelezea umepata wapi habari kwamba amekuwa akiwaambia marafiki zake kuwa hakupendi. Kama habari hizo ni za kweli, basi kuna hatari kwamba nia ya kijana huyo ni kukutumia tu huku akikuhadaa kuwa anakupenda. Ni muhimu umkabili umuulize kuhusu habari hizo na msimamo wake ili uchukue uamuzi unaofaa.