Makala

SHANGAZI AKUJIBU: Nahofia kukutana na ex wangu anipandishe mizuka

April 17th, 2019 2 min read

Na SHANGAZI

HUJAMBO shangazi? Kuna mwanamume tuliyekuwa wapenzi wa dhati tukiwa katika chuo kikuu na kwa wakati fulani tuliamini kuwa hatimaye tutaoana. Lakini baada ya kumaliza masomo nilipendana na mwingine na akanioa. Sasa mpenzi huyo wa awali amekuwa akinipigia simu akitaka tukutane. Mimi sasa ni mke wa mwenyewe na nahofia tukikutana kuna hatari ya kupandwa na hisia za awali nimkosee mume wangu. Nishauri.

Kupitia SMS

Kama kweli mlipendana jinsi unavyoelezea, ninaamini kuwa mwanamume huyo bado ana hisia kwako na ukimpa nafasi mkutane hata wewe zitakupanda na huenda ukamkosea heshima mume wako na ndoa yenu. Mwambie wazi kuwa wewe sasa ni mke wa mtu na huoni sababu yenu kukutana.

Mkewe alimtoroka ila hisia zake kwangu pia naona zimefifia

Kwako shangazi. Nilianzisha uhusiano wa kimapenzi na mwanamume aliyeoa na kwa bahati mbaya mkewe akagundua uhusiano wetu kisha akamuacha. Aliahidi kunioa lakini sasa hazungumzii tena jambo hilo na pia naona hisia zake kwangu zimepungua ikilinganishwa na hapo awali. Je, inawezekana kuwa anataka kumrudia mkewe? Nishauri.

Kupitia SMS

Mapenzi yanayohusisha mtu aliyeoa ama aliyeolewa huongozwa na tamaa wala huwa si ya dhati. Mapenzi ya mwanamume huyo kwa mke wake aliyemuacha kwa ajili yako ni ya dhati na ni lazima aliingiwa na baridi alipoachwa. Tabia yake ya sasa kwako ni ishara kuwa huenda anafikiria namna ya kumrudia mke wake. Usiweke imani sana kuhusu ahadi yake ya kukuoa.

Amebahatika kupata kazi, sasa ana dharau

Vipi shangazi? Mimi na mwanamke mpenzi wangu tulimaliza masomo ya chuo kikuu mwaka uliopita. Mapema mwaka huu mwenzangu alibahatika akapata kazi. Tangu aajiriwe, mpenzi wangu amebadilika ghafla, mara nyingi nikimpigia simu huwa hajibu ama anajibu kwa dharau. Nafikiri amepata mwingine na nina uchungu sana moyoni. Nishauri.

Kupitia SMS

Hizo ni dalili za kutosha kwamba mpenzi wako amebadili nia yake kwako, awe amepata mwingine au la. Haina haja ya kuendelea kuhangaika kuhusu mtu asiyekujali la sivyo utaendelea kuumiza bure moyo wako. Itabidi umsahau na uendelee na maisha yako.

Mfanyakazi wangu amesema waziwazi ananitaka kimapenzi

Kwako shangazi. Nimeoa na mimi na mke wangu tunafanya biashara ya kuuza nguo. Tumeajiri wanawake wawili na mmoja wao ananitaka kimapenzi. Ukweli ni kuwa ni mrembo sana kiasi cha kunasa moyo wangu lakini sitaki kusaliti ndoa yangu. Juzi alikuja ofisini mwangu akaniambia ni lazima tutakuwa wapenzi hata ikichukua miaka mingapi. Nifanye nini?

Kupitia SMS

Ushauri wangu ni kuwa ufanye juu chini kumuepuka mwanamke huyo la sivyo atavuruga ndoa yako. Njia pekee ni kumfuta kazi. Wewe ni bosi wake na sielewi ametoa wapi ujasiri wa kukufuata ofisini mwako kutangaza penzi lake kwako. Ukimpa nafasi hata mke wako atampiga.

Asema anataka kunioa ilhali hata kwao hajanipeleka

Shikamoo shangazi. Natumai wewe ni mzima na nimekuja kwako unipe ushauri. Kuna mwanamume ambaye tumekuwa wapenzi kwa miaka miwili sasa na amekuwa akiniambia atanioa. Pili, anataka nimzalie mtoto na nimekataa kwa sababu hata sijui kwao wala hajanitambulisha kwa jamaa zake. Nahitaji ushauri wako.

Kupitia SMS

Kabla ya watu kuoana ni lazima kwanza wafahamiane vyema wao wenyewe, wazazi wao na jamaa zao wengine. Kwa sababu hiyo si haki wala haifai kwa mwenzako kutaka umzalie ilhali wazazi wenu hawana habari kuhusu uhusiano wenu. Iwapo anatamani sana kuwa na familia, mwambie afuate utaratibu unaofaa.